Saturday Apr 30, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Wanafunzi waliofaulu darasa la saba wasitangazwe kwa awamu

10th January 2012
Print
Comments

Hivi karibuni Serikali kupitia kwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo ilitangaza matokeo ya mtihani wa darasa la saba. Waliofaulu wanatakiwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule mbalimbali nchini mwaka huu.
Baada ya  matokeo kutangazwa, Halmashauri zote nchini,  zimekwishatangaza majina ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule zilizo  kwenye Halmashauri husika.

Katika miaka ya karibuni, kumezuka utamaduni kwa Halmashauri kutangaza  kwa awamu majina ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari.


Mratibu Elimu wa Kata ya Ilungu iliyopo Mbeya Vijijini,  Mwl. Meshack Kapangeanasema kuwa, athari ya kwanza ya wanafunzi kuchaguliwa kwa mafungu kujiunga kidato cha kwanza, ni mzigo kwa mwalimu ambaye hutakiwa kuandaa maazimio yake ya kazi kwa kipindi cha siku 194 kwa mwaka.

Anasema kuwa Mwalimu anapokuwa ameanza utekelezaji wa maazimio yake, anapoletewa wanafunzi wapya huvuruga maazimio hayo na matokeo yake wanafunzi hawamalizi muhtasari na kujikuta wakipanda vidato wakiwa na upungufu wa elimu.

Alisema kuwa jambo hilo pia linachangiwa sana na Serikali kuongeza vyumba vya madarasa bila ya kuongeza idadi ya walimu na kwa kuwa hakuna malipo ya ziada, mwalimu anashindwa kujitolea kuwafundisha wanafunzi walioletwa kwa awamu ya pili katika muda wa ziada ili walingane na wale waliotangulia.

Mwl. Kapange anasema kuwa kwa wazazi wengi hasa waliopo vijijini matokeo ya kwanza yanapotoka na kuona watoto wao hawakufaulu, huanza kutumia akiba ya fedha walizoandaa kwa ajili ya kuwasomesha watoto wao, hivyo anapokuja matokeo ya awamu ya pili huwakuta hawana kitu na matokeo yake wanafunzi wengi hawaripoti shuleni.

Mwl. Kapange anapendekeza kwamba wanafunzi wote waliofaulu watangazwe kwa wakati mmoja hata kama watachaguliwa kwa awamu kujiunga na elimu ya sekondari, ili maandalizi ya msingi yaweze kufanyika mapema.

Anapendekeza ratiba za masomo katika shule za sekondari zirekebishwe ili wanafunzi wawe wanagawanywa katika makundi mawili ya  wanaosoma kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 6:30 mchana na wengine wanaingie darasani saa 8:30 mchana hadi saa 12:00 jioni, hali ambayo alidai kuwa itasaidia walimu kutorudia rudia mada walizokwisha fundisha na badala yake ataendelea na maazimio yao ya kazi.

Mwalimu Mstaafu, Alphoce Hillya, mkazi wa kijiji cha Nyakiswa, kata ya Kyanyari katika wilaya ya Musoma Vijijini, mkoani Mara, anasema uteuzi wa wanafunzi kwa awamu kujiunga na kidato cha kwanza unaleta kizunguzungu cha maisha kwa wazazi  wanaolazimika kuhakikisha kuwa watoto wao wanaendelea na masomo baada ya uteuzi.
Anasema baada ya watoto wao kufanya mihani wa darasa la saba, muda wa matokeo kutangazwa unajulikana ambapo wazazi wengi huanza kujiandaa au kuandaa fedha za kumpeleka mtoto shuleni punde matokeo yanapotoka.

Anasema sio lazima wazazi waandae fedha, bali wengi wao huandaa mifugo kama vile ng’ombe, mbuzi, kondoo na vinginevyo kwa ajili ya kuuzwa ili zipatikane fedha za kumsomesha mtoto.

Ili kuondokana na tatizo hilo  anasema  Serikali au Halmashauri zinapoteua wanafunzi wa kujiunga awamu ya kwanza, ni afadhali ikawatangaza katika orodha ya akiba (reserve list) wanafunzi wote waliofaulu ili wazazi wakae wakijua kuwa watoto wao wameshinda na wanaweza kuitwa wakati wowote kwenda shuleni hivyo wakajiandaa mapema.


Mariamu Ebunga naye mkazi wa Nyakiswa Musoma Vijijini, alisema watoto wasipochaguliwa kwenda sekondari kwa wakati hukata tamaa ya kuendelea na masomo na kujihusisha na shughuli nyingine za kuendeleza maisha yao, na kwamba  wanapokuja kuitwa kwenda shuleni huwa wamekwishasahau  masomo hali  inayosababisha  wasifanye vizuri katika taaluma zao.

Mkazi wa Jijini Mbeya, Zainab Hassan, anasema  utaratibu huo una madhara makubwa kwa wanafunzi hasa wale ambao majina yao yanachelewa kutangazwa kujiunga na kidato cha kwanza.

Alisema matokeo yanapotangazwa, wanafunzi ambao hawajachaguliwa,  baadhi yao huamini kuwa wamefeli, na kuanza kujihusisha na masuala ya  uraiani.

Zainab anasema, matokeo ya darasa la saba yanapotoka, watoto wa kume wanapoona kuwa hawakufaulu  mara nyingi baadhi yao huanza kujihusisha na mambo yasiyofaa  kama vile  utumiaji wa dawa za kulevya, uvutaji bangi na  kupiga debe kwenye vituo vya mabasi.

Alisema, kwa upande wa watoto wa kike, baadhi yao hutafuta kazi za ndani, kujiingiza kwenye ukahaba na  wengine kujikuta wakipata mimba.

Zainabu aliishauri Serikali kuwa uteuzi wa wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza ufanyike kwa pamoja ili watoto waweze kuendelea na masomo kwa pamoja kama walivyokuwa katika shule ya msingi.
Mkazi wa Ghana Jijini Mbeya, Gibson Mwakatwila, alisema kuwa zipo athari nyingi zinazoipata jamii kutokana na Serikali kufanya uteuzi wa wa  kidato cha kwanza kwa awamu.

Utaratibu huo huwaathiri wanafunzi kisaikolojia, kwani wale wanaochelewa kuchaguliwa wanapoona kuwa wenzao wemechaguliwa hujisikia vibaya na kuhisi kuwa safari yao ya kielimu imefikia mwisho, hivyo  wanapokuja kutangaziwa kuwa na wao wamechaguliwa huwa tayari wamepoteza morali wa kusoma.

Mwakatwila anasema kuwa, wazazi wa wanafunzi nao huathirika kiuchumi kutokana na kutokujiandaa kuwapeleka watoto wao shule kwa muda ambao hawakujulishwa mapema na Serikali kwa vile uteuzi wa awamu ya pili huja bila kutarajia.

Alisema wazazi wanatambua kuwa, Serikali inafanya hivyo kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa, lakini akashauri kuwa ili kuondokana na athari hizo, Serikali inapofanya uteuzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza pia itangaze orodha ya akiba ya wanafunzi waliofaulu lakini uteuzi wao unasubiri ujenzi wa vyumba vya madarasa ukamilike..

Beatrice  Ngalemi  ni mwanafunzi aliyehitimu darasa la saba mwaka jana na kuchaguliwa kujiunga na sekondari ya Ihanga Jijini Mbeya, alifurahi kufaulu katika awamu ya kwanza.

Alisema kuwa, wapo rafiki zake ambao hawajachaguliwa katika awamu ya kwanza na wanajisikia vibaya kiasi kwamba hata wanapomwona yeye kuwa, aliyebahatika kuchaguliwa huwa wanajificha wasikutane naye kwa kudhani kuwa angewacheka.

Anahisi kama asingechaguliwa katika awamu ya kwanza, na kuchaguliwa baadaye wenzake wangemcheka kuwa ufaulu wake ni wa alama ndogo na ndiyo sababu hakuchaguliwa katika awamu ya kwanza.

Mwalimu Flora Majembe ambaye anafundisha katika shule ya Sekondari Legico ya Jijini Mbeya anasema kuwa, athari za kuchagua wanafunzi kwa mafungu kuingia sekondari ni kubwa sana, kwani wapo wazazi ambao watoto wao wasipochaguliwa katika awamu ya kwanza huamini kuwa tayari wamefeli na kwa kuwa wanapenda watoto wao waendelee na masomo huenda kuwatafutia nafasi katika shule za watu binafsi.

Anasema kuwa athari nyingine ipo kwa wanafunzi wenyewe kwani wale wanaochaguliwa katika awamu ya pili na ya tatu huanza masomo kwa kuchelewa na wakati huo wanafunzi wenzao waliotangulia huwa wameshapiga hatua kubwa ya kimasomo, na hivyo kujikuta wamebaki nyuma.
Anasema kuwa kwa kawaida huwa ni vigumu kwa mwalimu kurudia mambo ambayo tayari ameshayafundisha kwa ababu akifanya hivyo huharibu maazimio yake ya kazi.

Mwalimu Stantony Lunyembe  anayefundisha katika shule ya Sekondari Isyesye ya Jijini Mbeya anasema kuwa, katika matokeo ya awali ya mtihani, mtoto anapaswa kuelewa kuwa amefaulu au ameshindwa.

Anasema kuwa mtoto anapokuja kufahamishwa kuwa ameshinda wakati wa matokeo ya awamu ya pili, kisaikolojia kwake na kwa wenzake inaonyesha kuwa amebahatisha, hana uwezo, amehurumiwa  au amefaulu kwa alama za chini sana.

Anasema kuwa athari nyingine ya kuteua kwa mafungu wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza ipo kwa mwalimu ambaye hulazimika kurudia kazi ambayo tayari imeshafanyika kwa wale waliotangulia.

Mwalimu Lunyembe anasema kuwa jambo ambalo  kwa mwalimu husababisha mzigo mkubwa wa mwendelezo wa masomo yake aliyoazimia kuwafundisha wanafunzi katika kipindi cha mwaka huo.

Aidha Mwalimu Lunyembe anasema kuwa mwalimu pia hutakiwa kujipanga upya na kuanza kuwatambua wanafunzi na uwezo wao ili aweze kuwafundisha vema wanafunzi waelewe.

Alipendekeza kuwa matokeo kwa wanafunzi wote waliofaulu yatolewe kwa awamu moja na wachaguliwe kwa wakati mmoja kuingia sekondari na baada ya hapo litakuwa ni jukumu la wazazi wa eneo husika kuafuta ufumbuzi ili wanafunzi waendelee kusoma.

Alisema kuwa upungufu wa vyumba vya madarasa kisiwe kigezo cha anafunzi kuchaguliwa kwa awamu.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles