Monday May 2, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Serikali yatangaza ajira mpya za madaktari

5th July 2013
Print
  Waliogoma mwaka jana nao waula
Madaktari kipindi cha mgomo

Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imesema sekta ya Afya inaupungufu wa madaktari kwa  asilimia 47 kwa kada zote za Afya, hivyo imeajiri wataalamu wa Afya wakiwamo madaktari waliopo katika mazoezi kwa vitendo waliosimamishwa kutokana na mgomo wa madaktari mwaka jana.

Hayo yalisemwa jana  na Msemaji wa Wizara hiyo, Nsacris Mwamwaja wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkakati wa Serikali katika utekelezaji wa utoaji huduma za afya kutoka ngazi ya kijiji hadi Taifa.

Alisema madaktari wote waliokuwa katika  mazoezi kwa vitendo na waliomaliza mafunzo yao (Interns) waliosimamishwa  mwaka jana kutokana na kushiriki katika mgomo wa madaktari na wao wamejumuishwa katika ajira hizo mpya.

Alisema  katika ajira hizo mpya, Wizara imeajiri madaktari 473 lengo likiwa ni kuboresha huduma za afya hapa nchini.

Mwamwaja alifafanua kuwa madaktari wa mafunzo kwa vitendo  wote waliosimamishwa kazi mwaka jana na Wizara walirudishwa kazini baada ya  Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT) kuwaita na kuwapa adhabu ambazo walizitumikia.

Aliongeza  kwasasa kada zote za afya zinawahudumu wa afya  kwa kiwango cha  asilimia  53 tu.

“Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kuzingatia Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (Mmam-2007/17) imejikita katika kutekeleza maeneo yakiwamo Rasilimali watu,ujenzi na ukarabati wa vituo vya huduma za Afya,” alisema Mwamwaja

Mwamwaja alisema kwa mwaka wa fedha 2012/2013 Wizara ilipata kibali cha kuwapangia vituo vya kazi wataalam wa  afya 8,869 ikijumuisha Halmashauri,Tawala za Mikoa,Hospitali za Mashirika ya kujitolea,Wizara.


Alisema wataalam hao ni wauguzi,wateknolojia viungo bandia, wateknolojia mionzi, wateknolojia macho, wateknolojia maabara, wateknolojia dawa, pamoja wasaidizi afya mazingira.

Zingine ni Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH),Taasisi ya Saratani Ocean Road, Hospitali ya Rufaa Bugando na  CCBRT.

Mwamwaja alisema katika kuongeza watumishi wa kada ya Afya katika mamlaka mbalimbali za ajira mwaka 2008/09 waliajiri watumishi 5,241,  2009/10 watumishi 6,257  2010/11 watumishi 7,471  2011/12 watumishi 9,391.

Sekta ya Afya nchini imekuwa ikikabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwamo migomo ya madaktari, ikiwa Agosti mwaka jana  madaktari waliokuwa mafunzoni wapatao 229 walifukuzwa baada ya kutokea kwa mgomo wa madaktari ambao na wao walishiriki.
 

SOURCE: NIPASHE

Articles

No articles