Wednesday May 4, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Unamtimua mkeo mjamzito, kishaunakula maraha na vidosho mitaani

29th April 2012
Print
Comments

Mpenzi msomaji, leo tuwatizame vijana wetu na yale yanayowasibu katika harakati zao za maisha. Tumsikie kijana aliyechezea hazina yake ikaisha na sasa anahaha kuomba msaada arudi kijijini. Ilikuwaje? Fuatilia kwa makini.

Unajua vijana wengi hudhani kuwa maisha ni mchezo tu wa kuigiza bila kutilia maanani kuwa kile unachokijenga katika akili yako ndicho utakachovuna matunda yake.

Wakati mwingine mtu atasema ni laana ya babu au bibi na kadhalika, kumbe ni rahisi sana mtu kujilaani mwenyewe na laana ile ikawa hadharani na kumtia aibu isiyorekebika haraka machoni mwa jamii.

Naam. Yupo kijana mmoja alikuwa na biashara zake karibu na pale ninapoishi. Alikuwa na genge la mbogamboga, duka na magari mawili. Biashara hizi zilikuwa zinashamiri vizuri na kuonekana kijana mwenye juhudi za maendeleo. Hakika alikuwa mjasiriamali mzuri.

Lakini pamoja na mazuri hayo, mmoja wa marafiki zake akanidokeza mapungufu yake ambayo ndiyo baadaye yaliyomfilisi na sasa anatafuta nauli ya kwenda kumzika dadake na ikiwezekana akaishie huko huko kijijini kwake kuepusha aibu anayoendelea kuipata hapa mjini.

Unajua mtu unapokuwa na maendeleo wenzako hukuonea wivu, ule wivu wa maendeleo wakitamani pengine ingekuwa ni wao wangefanya hili na lile kwa mafanikio zaidi. Lakini kumbe kwenye miti hakuna wajenzi. Ndivyo walivyosema wahenga wetu.

Kijana huyo inaelezwa kwamba kabla biashara hazijashamiri alikuwa akiishi na mwanamama mmoja kama mkewe. Ikatokea bibie akapata ujauzito na ndipo jamaa alipoanza kumfanyia vitimbwi mara asiache hela ya matumizi, mara alale huko huko. Ili mradi tu anamvuruga bibie hasa baada ya kupata vidosho nje vinavyovutiwa na fedha zake.

Bibie akiwa karibu anajifungua, kijana huyu akamtimua kwao, tena kwa mikwara ya ajabu. Yaani hakumuona kama ni kitu mbele yake japo baadhi ya mali walizichuma kwa juhudi za pamoja.

Katika sheria bila shaka ya mirathi, lipo eneo linalosema kwamba mali zilizochumwa ndani ya ndoa ni kwa manufaa ya wote, mke na mume.

Pia kwamba hata kama mama ni mama wa nyumbani na baba ndiye mhangaikaji, ili mradi tu mama yupo pale kumhudumia mume huyo katika maandalizi yote ya nyumbani, kufua, kumpikia, kumpokea arudipo na kadhalika, ni lazima anufaike na mali za familia husika. Hili kwa kijana huyu halikuwepo kabisa. Alichojua ni kumtimua pamoja na ujauzito ule ili apate nafasi ya kutanua vizuri na vidosho wengine huko mitaani.

Vijana wa pale mtaani wakaanza kumuona kijana mwenzao huyo akibadilisha wadada na kuhama baa hadi baa. Katika genge na duka akaweka vijana wake wa kumuuzia.

Vijana hao nao kwa kuona jamaa kila akija anataka fedha na kuondoka, nao wakaanza kumega za kwao na kutia mifukoni. Fumba na kufumbua genge likafilisika, duka likafilisika na biashara zote hizi zikafa.

Yale magari mawili akaanza kuuza moja baada ya lingine na fedha zilipoisha akaanza kupita mitaani kwa aibu. Kumbuka vijana wenzake ambao walikuwa wakifurahia maendeleo yake bado wangali wanamtizama pale mtaani.

Hivi majuzi nikiwa naelekea kazini, nikiwa natembea nikasimamishwa na vijana wawili. Mmoja akiwa ameshikilia daftari na kalamu. Kulikuwa na manyunyu ya mvua, mmoja akanisimamisha na kunionyesha daftari akiashiria anataka mchango fulani.

Kwa kuwa vijana wale nawafahamu, nikawaambia nitawaona baadaye kwani wakati ule nilikuwa nalowa mvua. Kufika mbele kwenye duka la mama mmoja rafiki yangu, ndipo nikapata habari kamili kuhusu daftari lile nililokutana nalo.

Mama huyu akaniambia, “hujakutana na vijana wawili wakichangisha fedha? Nikamjibu ndio. Akaniambia kuwa wanamchangia kijana mwenzao ambaye amefiwa na dada yake lakini hana hata shilingi ya nauli ya kwenda kwao Kigoma kwenye msiba.

”Amefulia baada ya biashara zake za genge, duka na magari kuyeyuka baada ya kuzitumbukiza kwenye pombe na wanawake”. Kumbe wakati ule vijana wale wakipita na daftari kumchangia nauli, yeye(anayechangiwa) alikuwa anaambatana nao kwa nyuma ili ajue zimepatikana ngapi. Ama kwa hakika Maisha Ndivyo Yalivyo.

Mpenzi msomaji, maisha ni mpangilio na malengo, ukiyakosea tu unaharibu mtiririko mzima. Unatakiwa umuombe sana Mungu anapokuonyesha nuru ya mafanikio na siyo kumkufuru na kuwanyanyasa wengine ukitegemea Baraka.

Mama yule aliyemfukuza akiwa mjamzito huku akijua fika kuwa sehemu ya mali alihusika kuzifanikisha siyo ajabu alimuachia Mungu. Hata maandiko yake yanatuambia kuwa mwenzako anapokukwaza usilipize kisasi kwani kisasi anacho yeye mwenyewe Mola. Mtu akikufanyia baya mlipe kwa jema na Mungu atakufungulia yaliyofichika.

Mfano wa kijana huyu ndio unapaswa kutiliwa maanani na vijana wetu. Wanapaswa kwanza kumuomba Mungu abariki kazi za mikono yao.

Kisha wamuombe pia katika kuzisimamia kazi hizo ili ziweze kuzaa matunda, tena matunda ya kudumu. Kufilisika kwa kijana huyu niliyomzungumzia kulitokana na mipangilio mibovu ya matumizi ya mapato yake ambayo aliyaelekeza katika eneo ambalo halizalishi badala yake linateketeza mali(pombe na ufuska). Mtaji ule ulipomponyoka, naye akarudia kuwa ombaomba. Kwanini ufikie hapo?

Ukiona mwenzako ananyolewa, wewe anza kutia maji. Au siyo msomaji wangu? Kwa leo nikomee hapa kama utakuwa na maoni, ushauri kwa vijana wetu unakaribishwa sana katika safu hii ya Maosha Ndivyo Yalivyo.

Ukiwa tayari kuwa huru kuwasiliana nami kwa kutuma ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 0774268581(usipige), au barua pepe; [email protected]

.Kumbuka kama hutapenda jina au simu yako itajwe gazetini tamka hivyo na hilo litaheshimiwa.

Wasalaam.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles