Saturday May 25, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Ngassa azigonganisha Yanya, Simba

1st August 2012
Print
Comments
Mshambuliaji wa Azam, Mrisho Ngassa

Mshambuliaji wa Azam, Mrisho Ngassa amezigonganisha Yanga na Simba baada ya klabu hizo zenye uhasama wa jadi kutuma kwa nyakati tofauti maombi ya kutaka kumsajili nyota huyo kwa dau la mamilioni ya fedha.

Taarifa ambazo NIPASHE ilizipata jana zilieleza kuwa walioanza kumuwania rasmi Ngassa ni ‘Wekundu wa Msimbazi’, Simba, ambao walituma ofa ya Sh. milioni 20 ili kumtwaa kwa mkopo.

Yanga ambayo Jumamosi iliyopita ilitetea taji lake la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) baada ya kuifunga Azam katika fainali kwa mabao 2-0, nayo pia iliandika jana barua ya kumuhitaji Ngassa kwa mkopo na kueleza vilevile kwamba iko tayari kulipa Sh. milioni 25 ili kumnasa nyota huyo anayeichezea pia timu ya taifa (Taifa Stars).

Hata hivyo, baada ya kujua kuwa watani zao wa jadi wametoa ‘ofa’ yenye ziada ya milioni tano zaidi ya fedha walizoahidi wao, Simba wameamua kuzidisha mashambulizi baada ya makamu mwenyekiti, Godfrey Nyange ‘Kaburu’ kuiambia NIPASHE jana jioni kuwa sasa wako tayari kuboresha ofa yao hiyo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Meneja wa Azam, Patrick Kahemele, alisema kuwa klabu yake imeshaanza kuyafanyia kazi maombi ya klabu hizo kongwe nchini na kwamba, uongozi utatoa maamuzi yake leo.

"Tulianza kupokea barua ya Simba, na leo (jana) asubuhi, Yanga nao wametuandikia barua wakimtaka Ngassa kwa Sh. milioni 25, tutatoa maamuzi yetu ndani ya saa 24 kuanzia sasa (jana jioni)," alisema meneja huyo ambaye ni miongoni mwa maafisa wanaoshiriki vikao vya kujadili usajili wa wachezaji wa Azam.

Kahemele alisema kuwa kama ni kumuuza, wataangalia klabu ambayo itawapa dau la juu zaidi.

Juzi, Azam ilitangaza kwamba iko tayari kumuuza Ngassa kwa  dola za Marekani 50,000 ( sawa na Sh. milioni 80) kufuatia nyota huyo kuonyesha wazi mapenzi aliyo nayo kwa klabu yake ya ya zamani ya Yanga, ambapo alibusu nembo ya klabu hiyo ya ‘Wanajangwani’ wakati akishangilia goli alilofunga katika mechi yao ya nusu fainali ya Kombe la Kagame dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, aliiambia NIPASHE jana kuwa klabu yao imepeleka maombi ya kumsajili Ngassa kwa mkopo baada ya kocha wao, Mserbia Milovan Cirkovic, kueleza kuwa anamuhitaji mshambuliaji huyo ili asaidie kuimarisha kikosi chao kitakachoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara na michuano inayowakabili mwakani ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment