


.jpg)
Mamia ya mashabiki wa Yanga ambao walijitokeza kwa wingi kwa mara ya kwanza jana tangu 'wapotee' Uwanja wa Taifa kuelekea mwishoni mwa msimu uliopita wa ligi kuu ya Bara, wangeweza kusamehewa kama wangedhani timu yenye jezi za njano uwanjani hapo ni Brazili kutokana na kiwango kikubwa kilichoonyeshwa na wenyeji, katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Express ya Uganda.
Katika mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa uliomalizika kwenye mwanga wa taa badala ya jua kufuatia kuchelewa kuanza, Yanga ilishinda kwa magoli 2-1.
Ikianza na wachezaji saba wapya waliosajiliwa kwa mara ya kwanza msimu huu; nane ukijumuisha na Jerry Tegete aliyerudi katika kikosi cha kwanza kwa mara ya kwanza baada ya kubaniwa nusu msimu na kocha aliyepita Kostadin Papic, Yanga iliburudisha. Kama Brazili.
Haikushangaza basi ilipokwenda mapumziko ikiongoza kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Tegete, lakini habari kubwa zaidi ni kwamba yote yalipikwa na mshambuliaji mpya Said Bahanuz.
Magoli hayo, na kiwango cha mchezo cha timu uwanjani kiliwafanya mashabiki wa Yanga kuishangilia wakati wote, lakini hoi hoi zilizidi pale wachezaji waliochukuliwa kutoka kwa mahasimu Simba walipogusa mpira.
Kelvin Yondani, aliyevaa jezi namba 22 iliyokuwa ikitumiwa na beki Chacha Marwa msimu uliopita, alikuwa kipenzi cha mashabiki hao wa Yanga. Ndivyo ilivyokuwa kwa Ali Mustapha 'Bartez' golini.
Wachezaji wapya wengine walioanza jana chini ya kocha wa muda Fred Felix Minziro ni Juma Abdul, Nizar Khalfan, Frank Domayo na Simon Msuva.
Bao la wageni lilikuwa la kujifunga la mchezaji mpya aliyeingia kutoka benchini kuchukua nafasi ya Yondani -Ladislaus Mbogo katika kipindi cha pili, katika harakati za kuokoa adhabu ndogo.
Kama ilivyo kawaida ya timu iloyoanza mazoezi, stamina iliikimbia Yanga katika dakika 20 za mwisho ambapo iliruhusu wageni kutamba.
Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa mashabiki wa Yanga kufika kwa wingi uwanjani, kuwaona wachezaji wapya, tangu waliposusia matokeo mabovu yaliyosababisha timu hiyo ishike nafasi ya chini zaidi kwa miaka 24, ya tatu ya kucheza hapa hapa.
Katika mchezo huo, mashabiki wa Simba walikuwa wakiwazomea kwa nguvu Yondani aliyecheza kipindi kimoja na 'Bartez' kila walipogusa mpira.
Simba inarudiana na Express leo kwenye uwanja huo baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 mjini Shinyanga wiki moja iliyopita.
Timu zilikuwa:
YANGA - Ally Mustapha 'Bartez', Juma Abdul, Oscar Joshua (Stephano Mwasika dk.45), Nadir Haroub 'Canavaro', Kelvin Yondani (Ladislaus Mbogo dk.45), Athumani Iddi 'Chuji', Nizar Khalfan (Shamte Ally dk.45), Frank Domayo, Said Bahanuz, Jerry Tegete, Simon Msuva.