Sunday May 1, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Mawaziri waingiwa kiwewe kutimuliwa

29th April 2012
Print
Comments
Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi Omar Nundu

Baada ya Kamati Kuu (KK) ya CCM kubariki mpango wa Rais Jakaya Kikwete kulisuka upya Baraza la Mawaziri na kuwawajibisha mawaziri wanaotuhumiwa kwa ubadhirifu wa fedha za umma baadhi yao wameanza kuingiwa kiwewe na kugeuka bubu baada ya kupigiwa simu na kukata huku wengine wakijibu kwa mkato.

Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi Omar Nundu, alijibu kwenye simu kuwa hazungumzi na mwandishi kwa namna yoyote. "Siwezi kuongea na mwandishi wa habari wa gazeti lolote lile," alisema na kukata simu.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Mkuchika, alipohojiwa juu ya maamuzi hayo ya Kamati Kuu ya CCM alisema’ ‘’sina cha kusema”. Kaandike “no comments”.

Wakati mawaziri hao wakionyesha msimamo huo, Waziri wa Nishati na Madini , William Ngeleja, simu yake iliita muda mrefu bila kupokelewa licha ya kupigiwa mara kadhaa.

Kwa upande mwingine wanataaluma, wabunge na viongozi wa Azaki mbalimbali wamesifu hatua ya Rais ya kulisuka upya Baraza la Mawaziri, lakini baadhi wakimtetea ama kuhoji sababu za kutozungumziwa hatma ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Akitoa uchambuzi wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba alisema Rais alitakiwa kueleza hatma ya Waziri Mkuu ambaye wabunge 75 walitia saini za kukosa imani naye kwa vile ameshindwa kutimiza wajibu wa kuwasimamia mawaziri na kusababisha uzembe na ubadhirifu wa fedha za umma.

Alisema Kamati Kuu ilitakiwa pia itoe maamuzi ya kupiga kura ya kukosa imani na Waziri Mkuu, kwa kuwa kama zilivyo hoja za matumizi mabaya ya fedha na uongozi dhaifu wa mawaziri hoja ya kukosa imani na Pinda nayo ililitikisa Bunge.

Kibamba alishauri kulisuka baraza hilo kuende pamoja na kulipunguza ukubwa kwani kulihudumia kunasababisha matumizi makubwa ya fedha za umma.Tanzania ina mawaziri 30 pamoja na manaibu 21 hivyo kuwa na baraza kubwa la watu 51.

Profesa Criss Peter Maina naye alipongeza hatua ya kulisuka upya aliyoieleza kuwa inaonyesha serikali inayowajibika. Kwa upande wa Waziri Mkuu alimtetea kuwa wabunge hawana nia ya kumuondoa bali walitaka kupitia kura ya kukosa imani naye wawaondoe mawaziri waliotuhumiwa.

“Waziri Mkuu anasimamia mawaziri, lakini hawateui, wala kuwawajibisha yeye anatoa mapendekezo. Wabunge hawawezi kuwaondoa mawaziri lakini wanaweza kuondoa imani kwa Waziri Mkuu ili kuwezesha kuwaondoa mawaziri wasiowajibika.” Alisema Profesa Maina, Mhadhiri wa Sheria.

Mtaaluma mwingine Dk. Magdalena Ngaiza aliisifu hatua ya kulisuka upya baraza na kusema Rais amewaonyesha Watanzania kuwa mawaziri wanaotuhumiwa wanachofanya sicho alichowaelekeza ama alichotarajiwa wakifanye.

Alisifu kuwa ni utawala bora ambao unalenga kuweka mbele maslahi ya umma na siyo ya wachache. Lakini pia alitetea hoja ya Waziri Mkuu na kusema kuwa licha ya wabunge kueleza nia ya kumuondoa Waziri Mkuu ili kuwawajibisha mawaziri wadhaifu, anayebakia na dhamana ya kuwawajibisha ni Rais.

Akizungumzia hatua hiyo, Mbunge wa Ludewa (CCM) , Deo Haule Filikunjombe, alisema licha ya kusikia ahadi hiyo, umma unataka kuona hatua ikichukuliwa na mawaziri hao wakiwajibishwa, “Tunasubiri tuone utekelezaji.“

Hata hivyo, aliponda tabia ya kulindana ndani ya CCM aliyosema imeigeuza nchi kuwa shamba la bibi. Alisema kuwawajibisha kuendane na kuhakikisha kuwa mambo haya hayatokei tena kwa kuwachukulia hatua stahili watuhumiwa na kuleta utashi wa kisiasa unaosimamia na kuhakikisha uwajibikaji na utumishi wa uadilifu.

Ijumaa wiki hii Kamati Kuu ya CCM ilibariki dhamira ya Rais Kikwete ya kulisuka upya Baraza la Mawaziri na kuwawajibisha wote waliotuhumiwa kuhusika na ubadhirifu wa fedha za nchi kwenye ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Pia Mawaziri na watendaji wa serikali waliotajwa kwenye ripoti za Kamati za Kudumu za Bunge na kujadiliwa bungeni kuwa wanahusika na ubadhirifu na matumizi mabaya ya pesa wananchi.

Bunge liliwachagiza Mawaziri nane kujiuzulu kufuatia udhaifu wa uongozi uliosababisha upotevu mkubwa wa fedha za umma. Walitakiwa kuachia ngazi ni pamoja na Waziri wa Madini na Nishati, Mali Asili na Utalii, Mawasiliano na Uchukuzi, Afya na Ustawi wa Jamii, Kilimo , Chakula na Ushirika, Fedha, Viwanda na Biashara, na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa).

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles