Thursday May 5, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Mbowe: tunajiandaa kuchukua nchi

30th April 2012
Print
Comments
Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kinajipanga kuchukua dola mwaka 2015 na kwamba ndoto ya Watanzania iko karibu kutimia kutokana na tishio la hali ngumu ya maisha inayosababishwa na mfumuko wa bei za vyakula nchini chini ya uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kadhalika Chadema kimesema ili kuikamata dola mwaka 2015, chama hicho kina mkakati mkubwa wa kusisitiza nidhamu kwa wanachama wake wote nchini  itakayowapa imani wananchi wakati wa kushika dola.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, wakati akifungua Mkutano wa Baraza Kuu la chama hicho jijini Dar es Salaam.

Alisema ajenda kubwa ya mkutano huo ni kujipanga kuhusu namna ya kushika dola mwaka 2015 sambamba na nidhamu kwa wanachama wote itakayowapa imani Watanzania wakati wakiwa madarakani.

Alisema serikali iliyopo madarakani ina matumizi makubwa ya anasa na kusababisha upungufu wa fedha huku wananchi wakilia kwa ugumu wa maisha.

“Ndugu wajumbe ajenda kuu ya mkutano huu tunajipanga namna ya kushika dola mwaka 2015 pamoja na kuimarisha nidhamu katika chama ili wananchi wawe na imani na sisi... hali ya wananchi ni mbaya sana, mfumuko wa bei ya vyakula haukamatiki uko juu na wanashindwa kumudu maisha kutokana na serikali iliyoko madarakani kujali matumizi ya anasa ya vigogo wake,” alisema Mbowe.

Alisema serikali ya CCM imechanganyikiwa na  inashindwa kutimiza majukumu ya msingi, ikiwemo kuwatimizia wananchi mahitaji ya msingi pamoja na kupunguza mfumuko wa bei.

“CCM watupishe Chadema tuingie Ikulu kuwatumikia wananchi, mara ya pili sasa Baraza la Mawaziri linavunjwa tangu Rais Kikwete aingie madarakani. Watupishe jamani,”  alisema Mbowe huku akishangiliwa na wajumbe wa mkutano huo kutoka mikoa ya Tanzania Bara na Visiwani.

MAUAJI YA WANACHAMA

Akizungumzia mauaji ya wanachama wa chama hicho kwa sababu ya kuwa mstari wa mbele kulinda haki na kwamba mauaji hayo yametokana na nguvu ya dola kuingilia kati.

“Katika chaguzi ndogo zilizofanyika Igunga, umeya wa Manispaa ya  Arusha mwaka jana na sehemu mbalimbali nchini wamekufa wanachama wetu 16, na mpaka sasa hakuna aliyechukuliwa hatua yoyote za kisheria ... sisi Chadema tunasema CCM wapo kwenye jumba la vioo kwa hiyo wasianze kutupa mawe nje,” alisema.

Aliongeza: “Godbless Lema amepoteza ubunge kihuni japo mahakama ni chombo cha kutenda haki na tuna imani nayo, lakini tuko tayari kurudia uchaguzi na tutashinda tena Jimbo la Arusha Mjini kwa kura za aibu ... heri mtu ufe umesimama kuliko kufa umepiga magoti kwa aibu.”

KATIBA MPYA

Kuhusu Katiba Mpya, Mbowe alisema wabunge wa chama hicho waliibua suala hilo, lakini awali walibezwa na kutukanwa kwa sababu haikuwa ajenda ya CCM ya kubadili Katiba, lakini mwisho wa siku serikali ilikubaliana nao.

Alisema chama hicho kitatoa maelekezo kupitia vipeperushi kwa wanachama wake nchi zima vitakavyoeleza madai gani ya msingi wanayotaka yaingie kwenye katiba mpya.

“Kuhusu Katiba Chadema tutajadili tunavyotaka pamoja na kutoa elimu ya kutosha ili tuwe na sauti moja ikiwemo kupiga vita rushwa na sio kwa maelekezo ya Rais Kikwete,” alisema Mbowe.

NIDHAMU KATIKA CHAMA

Alisema wapo waliokuwa wanachama wa chama hicho ambao wamewavua uwanachama kwa utovu wa nidhamu wakiwemo madiwani na viongozi wengine na kuwa ikibidi hata wabunge wakifanya utovu wa nidhamu chama hicho hakiogopi mtu kitawachukulia hatua kali ili wakishika dola serikali yao iwe na maslahi kwa wananchi.

DK. SLAA AMSIFU SABODO

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibroad Slaa, alisema wafanyabiashara wakubwa nchini wanafanya shughuli zao kwa maelekezo ya CCM tofauti na mfanyabiashara Mustapha Sabodo ambaye ni mwanachana wa CCM, lakini anakisaidia Chadema kwa uwazi bila kuogopa mkono wa serikali kutokana na kufanya biashara halali.

Alisema Sabodo ni sehemu ya mafanikio ya Chadema kutokana na kuchangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha na kupata wabunge wengi kwa  katika Uchaguzi Mkuu uliopita.

“Tunamshukuru Mzee Sabodo kwa kutusaidia mara kwa mara katika chaguzi kuanzia ule wa mwaka 2010 hadi wa Arumeru Mashariki wa mwaka huu hadi sasa ametuachangia Sh. milioni 450 visima 210 katika majimbo yote yaliyoko chini ya Chadema,” alisema Dk. Slaa.

Naye Sabodo  aliyehudhuria mkutano huo kama mgeni mualikwa, alisema alichotoa Chadema ni asilimia moja ya yale aliyoyafanya kwa CCM na kwamba katika miaka 50 ambayo amekisaidia chama tawala hajawahi kupewa heshima kubwa na kuambiwa asante kama walivyofanya Chadema.

“Sijasema CCM wabaya, lakini wanapofanyiwa mazuri wanapaswa washukuru kama mlivyofanya ninyi Chadema, naamini vyama hivi viwili ni sawa na mtu na binamu yake... pia nataka kuahidi kwamba nitahakikisha najenga ofisi ya makao makuu ya Chadema  yenye hadhi badala ya ile mnayotumia sasa,” alisema Sabodo.

Aidha katika mkutano huo, baadhi ya wajumbe walishindwa kuhudhuria kutokana na kuwa na udhuru mbalimbali, akiwemo Edwin Mtei, Bob Makani na Zitto Kabwe  ambao walikuwa na matatizo ya kiafya, wakati Tundu Lissu na Profesa Abdallah Safari walikuwa nje ya Dar es Salaam kushughulikia kesi mbalimbali zilizopo mahakamani.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles