Saturday May 18, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Kaseja: Tuna kazi ngumu kutwaa ubingwa

25th April 2012
Print
Comments

Kipa na nahodha wa klabu ya Simba, Juma Kaseja, amesema kuwa klabu yake bado haijajihakikishia ubingwa msimu huu kwani wana kazi kubwa ya kusaka ushindi katika mechi moja iliyobaki dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Yanga.

Akizungumza na NIPASHE muda mfupi baada ya kumalizika kwa mchezo wao dhidi ya Moro United juzi kwenye uwanja wa taifa ambapo Simba walishinda 3-0, Kaseja alisema kuwa bado wana kazi kubwa ya kufanya kabla ya kujitangaza mabingwa wa msimu huu wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

"Tumefurahi kupata ushindi dhidi ya Moro United, lakini hii haimaanishi kuwa tayari sisi ni mabingwa… ila ni wazi kwamba ushindi huu umetufanya tukaribie ubingwa. Wachezaji tunajua kwamba bado tuna kizingiti mbele yetu kabla ya kuwa mabingwa," alisema Kaseja.

Alisema kuwa kazi kubwa waliyo nayo ni kupata matokeo mazuri katika mechi yao dhidi ya Yanga na kwamba kinyume chake, watajiweka katika hatari ya kutotimiza lengo lao.

"Kama Azam watapewa pointi tatu katika mechi yao (iliyovunjika) dhidi ya Mtibwa, basi kazi kwetu bado ipo kwa sababu na wao bado wana nafasi ya kutwaa ubingwa kwa vile wamebakiza mechi mbili," aliongezea Kaseja.

Alisema kuwa kuwafunga Yanga katika mechi yao ya mwisho kutakuwa ni zaidi ya ushindi kwao, hivyo watajitahidi kuhakikisha kwamba wanaibuka na ushindi katika mchezo huo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa ili watwae ubingwa na pia kulipiza kisasi cha kufungwa katika mechi waliyokutana kwenye mzunguko wa kwanza.

Hadi sasa, Simba inaendelea kuongoza katika msimamo wa ligi baada ya kufikisha pointi 59 na kubakiza mechi moja dhidi ya Yanga.

Azam waliobakiza mechi mbili, wanawafuatia Simba katika nafasi ya pili wakiwa na pointi 50, lakini pia wakiwa na uwezekano mkubwa wa kupewa pointi tatu na mabao matatu dhidi ya Mtibwa baada ya kile kilichodaiwa kuwa wapinzani wao hao katika mechi iliyopita walisababisha mechi kuvunjika kufuatia uamuzi wao wa kugomea penati wakati matokeo yakiwa sare ya 1-1.

Hofu nyingine kwa ‘Wana Msimbazi’ juu ya hatma yao ya ubingwa inatokana pia na ukweli kwamba, licha ya kukabiliwa na mechi ngumu dhidi ya mahasimu wao Yanga, Azam wanaowafuatia katika nafasi ya pili watacheza mechi zao zilizobaki kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Chamazi dhidi ya Toto African na Kagera Sugar.

Wakati huo huo, Somoe Ng'itu anaripoti kuwa kiingilio cha chini katika mechi ya awali ya raundi ya pili ya mashindano ya Kombe la Shirikisho kati ya Simba na Al Ahly Shandy kutoka Sudan itakayofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kimetangazwa jana kuwa ni Sh. 5,000.

Hadi kufikia jana jioni, uongozi wa Simba ulikuwa haujapokea taarifa rasmi za ujio wa wapinzani wao ambao walifika hatua hiyo baada ya kuwang’oa Ferroviario de Maputo ya Msumbiji.

Akizungumza jana, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu', alisema kuwa maandalizi ya mchezo huo yanaendelea vizuri na kiingilio cha juu katika mechi hiyo ya kimataifa ni Sh. 30,000 kwa viti vya VIP A wakati VIP B ni Sh. 20,000.

Kaburu alisema kuwa tiketi za VIP C zitauzwa kwa Sh. 15,000 huku zile za viti vya rangi ya machungwa na bluu zikuzwa Sh. 5,000.

Aliongeza kuwa tiketi hizo zitaanza kuuzwa kuanzia keshokutwa kwenye vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Kaburu alisema kuwa tayari timu yao imeshaanza kujiandaa na mchezo huo kwa kuanza kujinoa jana jioni na kwamba, wamewaomba mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kujitokeza kwa wingi Jumapili kuwashangilia wachezaji wao.

Waamuzi wa mchezo huo kutoka Swaziland na kamisaa ambaye anatoka Rwanda wanatarajiwa kuwasili jijini Dar keshokutwa.

"Tayari macho yetu tumeshayaelekeza kwenye mechi ya kimataifa, maandalizi yameshaanza na wachezaji wote wako vizuri isipokuwa Kapombe (Shomary) ambaye alipata maumivu jana (juzi), kikubwa tunawaomba mashabiki wetu na hata watani zetu waje kutushangilia, uwepo wao kwa wingi utaongeza morari na ari ya kupata matokeo mazuri," alisema Kaburu.

Aliwakumbusha pia mashabiki watakaofika uwanjani kuhakikisha wanakuwa watulivu na kulinda miundombinu ya uwanja.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment