


Mpenzi msomaji, wiki iliyopita tulizungumzia kisa cha binti mmoja aliyeeleza jinsi alivyonyanyaswa akiwa hausigeli katika familia fulani.
Na zaidi akatoa siri kuwa kumbe wapo baadhi ya kinamama wanaowaendea wasichana hawa kwa waganga ili wasiondoke na badala yake ionekane kuwa wanajua kukaa na wasichana wa kazi kwa muda mrefu. Kumbe wanawafanyia ufrauni mtupu.
Naam. Leo hebu tuingie anga zingine. Mara nyingi tumekuwa tunashuhudia baadhi ya kinababa wakiwafanyia vituko wake zao kwa ama kuhama kwa muda au kuhama moja kwa moja majumbani mwao na kujichimbia kwenye nyumba ndogo(wake wadogo). Yaani wanamuacha mke wa ndoa na kwenda kuishi na mwanamama mwingine. Wapo walioishi nao kama kimada na wengine kuoa kabisa.
Taswira hiyo imezoeleka sana ndani ya jamii yetu. Lakini ipo taswira nyingine ambayo inachipuka kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni ambapo baadhi ya kinamama kwa sababu fulani fulani wanachepuka na kuzihama nyumba zao kwa kuvizia wakidai wanataka kujitegemea.
Wengi wa kinamama wa aina hii ni wale ambao ama bado wako kazini au wamestaafu na kujizolea mafao ambayo yanawapa kiwewe na kujiona kuwa wanaweza kuishi peke yao bila waume zao na maisha ya uzeeni yakasonga mbele bila vikwazo.
Kinachotokea ni kwamba, kwa zile familia zenye uwezo ambapo baba na mama ni wafanyakazi au wazazi hawa wote wana biashara zinazowafanya wawe bize muda mwingi, ndizo hasa zilizovamiwa na kirusi cha utengano na kuiacha jamii ikizitizama kwa jicho moja kuona mwisho wake. Kama nilivyoeleza hapo juu kwamba kinababa ndio wamekuwa na mchezo wa kuzihama familia hasa za ndoa na kujichimbia nyumba ndogo wanazoita wengine sabuni za roho. Upo hapo msomaji wangu? Lakini sasa kibao kimegeuka kinababa wanahaha ‘mbona wanaachwa kiana?’
Nikumegee mfano wa kimbembe kinachoendelea. Hivi sasa kinamama wengi wameamua kuingia ulokole wakiamini kuwa ndiyo njia pekee ya kumtumikia Mwenyezi Mungu. Waweza kumkuta mwanamama aliyekuwa mywaji wa kupindukia lakini sasa ameacha pombe. Ukimuuliza kwanini anakwambia “nimeokoka na kuachana na matendo ya shetani”.
Wengine wameziacha dini zao za asili(zile walizobatizwa nazo) na kujiunga na makanisa mengine wakiamini kuwa huko kuna wokovu zaidi. Hii sasa ni imani ya mtu na mtu na siyo vema kuingilia mambo haya kwani mahubiri yananukuliwa toka ndani ya Biblia Takatifu. Maandiko yanasisitiza umoja na siyo utengano kama ambavyo baadhi ya viongozi wa familia wanaendekeza.
Baadhi ya hawa wanaoingia ulokole, wamekuwa na vituko majumbani mwao ikiwa ni pamoja na kuhama chumba cha ndoa na ama kulala chumba cha watoto au kujiamulia chumba kingine kama nyumba ni kubwa. Kwanini, eti ameokoka hataki kusumbuliwa tena hadi uzeeni.
Mpenzi msomaji, wapo walioamua kujitenga kwa namna hii baada ya kugundua kuwa mume siyo mwaminifu na pengine alishapata tetesi au ushahidi kuhusu mahusiano ya nje ya ndoa. Akijiridhisha, basi taratibu huchepuka kuepusha shari.
Lakini kuna kujitenga kwingine ambako ndio hasa kiini cha makala haya. Wapo kinamama wasomi, waliokuwa na kazi nzuri, walioishi ndani ya ndoa kwa raha, tena miaka mingi, wakapata watoto, kazi nzuri, lakini wanaamua kuhama chumba cha ndoa na kwenda kujenga maskani mengine.
Kiumri, kinamama hawa ni watu wazima sana. Kwa mfano anapokuwa amefikisha zaidi ya miaka 60, kisha anaamua kwenda kujenga nyumba yake kwingine na kuhama mji wake wa ndoa, siyo maamuzi magumu hayo? Na baadhi wanaochukua maamuzi haya inawezekana hawajagombana na waume zao, au pengine upo ugomvi wa kitambo lakini unaendelea kimya kimya(huwezi kujua nyumba za watu) kwani masuala ya ndoa ni mtihani mkubwa.
Wengine ni kiburi tu, eti amestaafu, kapata kiinua mgongo chake kilichoshiba, kinamzuzua na kwenda kununua kiwanja, kisha kujenga nyumba yake, tena bila kumshirikisha baba watoto. Ukiona mtu anachukua maamuzi ya aina hii, ujue amemchoka mwenzake ila tu anashindwa kuweka bayana hisia zake. Au siyo msomaji wangu?
Inapotokea jambo kama hili, kinababa katika nyumba husika huanza kuhaha na kujiuliza mara mbili mbili kulikoni sishirikishwi katika mipango ya aina hii? Na kinamama wanaochukua maamuuzi ya aina hii siyo kwamba nyumba ya ndoa ni mbaya, la hasha. Wengine wanaishi kwenye mabangaluu(nyumba za kifahari) lakini bado wanaamua kuziacha na kwenda kuanza maisha kwingine japo ni katika dakika za majeruhi. Wameshapata watoto na wajukuu, kwanini watengane?
Ukiona hivyo, ujue lipo jambo. Labda mama kama mumewe ni mtu wa shughuli nyingi, basi huona hapati muda wa mawasiliano na mumewe vile atakavyo, au pengine mama huyu kashawishiwa na wapambe baada ya kujitosa ulokole kwamba akitaka amani akakae peke yake.
Jambo hili la baadhi ya kinamama wanazihama nyumba zao na kwenda kuishi kivyao, nililinasa hivi majuzi wakati kinamama wawili wakibishana kuhusu mwenzao ambaye amejenga nyumba yake maeneo ya Kiboriloni, huko Moshi na mwezi uliopita amehamia. Lakini hadi anakamilisha nyumba hiyo hakuwahi kumjulisha mumewe.
Mama huyo, inaelezwa kuwa japo ana wajukuu, lakini ameamua kujenga nyumba yake kwa fedha zake mwenye na kwamba hataki bughudha ya mume. Katika mazungumzo yale nikagundua kuwa mumewe mama huyo anashangaa kwanini mkewe amemficha, hata kama fedha za ujenzi ni mafao yake baada ya kustaafu.
Hakika, Maisha Ndivyo Yalivyo. Lakini zipo sheria zinazolinda maslahi ya familia. Ipo sheria ya ndoa ya mwaka 1971. Sheria ya ndoa inatambua kwamba mali za mke kabla ya ndoa ni zake na zile ndani ya ndoa ni za wote wawili.
Kwa mantiki hiyo, hata kama mama atajenga nyumba akiwa ndani ya ndoa maana yake ni kwamba mali hiyo imepatikana akiwa tayari ameolewa hivyo itakuwa ni mali ya familia. Hivyo, hakuna sababu ya mume kuwa na hofu pale mke anapojipatika mali akiwa ndani ya ndoa akidhani kuwa haimhusu. Hivi ndivyo binafsi ninavyoliona jambo hili ninapoitizama sheria ya ndoa inavyoainisha.(kama nimekosea nisahihishwe).
Mpenzi msomaji, baada ya kusema hayo, nikomee hapa ili nitoe fursa kwa mjadala tuweze kuelimishana zaidi. Na ukiwa tayari, kuwa huru kutuma ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 774268581(usipige), au barua pepe; fwingia@gmail.com
Kumbuka kama hutapenda jina au simu yako itajwe gazetini tamka hivyo na hilo litaheshimiwa.
Wasalaam.