Monday May 2, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Meseji za simu zazidi kutesa ndoa!

15th April 2012
Print
Comments

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita nilijadili ujumbe wa simu ambao mume aliunasa kwenye simu ya mkewe.

Ujumbe ule ukisomeka hivi: Nilinukuu maneno ya ujumbe huo kama ifuatavyo; “Nimetoka nje ya ndoa yangu nikitegemea kupata faraja lakini ikawa tofauti nimeachwa kwenye mataa nikiwa mkiwa’’.

Mama huyo alipatwa na butwa baada ya kuulizwa na mumewe kuwa ujumbe huo alikuwa amemtumia nani, naye alisita kutaja lakini baada ya kibano kikali alikubali kuwa aliyemtumia ujumbe huo alikuwa na mahusiano kabla ya kuoana na hivi sasa wameamua kuendeleza mapenzi yao.

Mpenzi msomaji, wakati bado tunasubiri maoni kuhusu makala ile, hebu nikumegee kituko kingine nilichonasa wiki hii kuhusu meseji zinavyoendelea kutesa ndoa. Nyumba zingine hakukaliki ni moto mbele kwa mbele. Naam. Hebu msikie jamaa huyu aliyenitafuta tukakaa kitako akisimulia mtafaruku wa dadake.

Dada wa rafiki yangu aliolewa ndoa nzuri tu lakini takriban miaka miwili mumewe akamzingua mwishowe wakaachana kabisa. Hakuna cha mahakama wala nini. Kilichofanya waachane ni kwamba alimfumania ‘live’.

Wakati bado nikiwa natafakari tatizo hilo, nami yakanikuta ambapo dadangu naye ndoa yake inawaka moto. Kisa dada alifuma meseji za mapenzi kwenye simu ya mumewe(shemeji). Suala hili limemchanganya sana dadangu.

Yule dada wa rafiki yangu niliyedokeza awali, baada ya kumfumania mumewe, aliamua kuondoka kisha kikao kikafanyika kujadili mgogoro huo lakini bibie hakutaka tena mahusiano ya bwana yule, wakaachana moja kwa moja hadi leo hii kutokana na kuvunja uaminifu.

Naam. Dadangu yeye alimpenda sana mumewe. Na mume alipoulizwa kuhusu malalamiko ya dada kuhusiana na meseji, mengine alikiri mengine hakukiri.

Shemeji huyu mara tu baada ya dada kujifungua mtoto wa kwanza, ndio akaanza vitimbwi, mara anarudi saa nane za usiku mara alifajiri. Akiulizwa anajibu mkato au hajibu kabisa.

Siku moja akaja amelewa chakari. Mke akamvizia akachukua simu yake moja na kufungua meseji, aliyoyakuta alistaajabu. Alichofanya akachukua namba ya zile meseji, lakini kabla ya kumpigia aliyetuma meseji, akamuuliza mumewe. Kuulizwa akakiri na mengine kukataa. Kisha kesho yake dadangu akampigia yule mwanamke.

Yule mwanamke akakiri ni kweli ana mahusiano na mumewe na kwamba yeye ang’ang’ane na ndoa wakati wenzako(huyo kimada) tunafaidi. Mume aliporudi nyumbani akamuuliza akaona aibu akatulia kama siku tatu, nne hivi, baada ya hapo mchezo ule ule wa kurudi majogoo ukaendelea.

Baada ya hapo mume huyu akajua dada kamshtukia kwenye simu, akaamua kununua simu mpya zile za ku-slid vidole ambazo dada hajui kuzitumia. Na isitoshe, kila alalapo anaziweka chini ya mto usawa wa kichwa ili mtu akigusa hapo ajue.

Mkewe alipombana kuhusu huyo hawara yake akajitetea kuwa ni mfanyakazi mwenzake tena bosi. Naye akamwambia kama ni bosi wako basi nitakwenda kumuuliza. Kusikia vile akamwambia hakuna kwenda usije kuniharibia kazi tukose hela ya kula. Kumbe hiyo ni geresha tu.

Huyo bwana taarifa zilipofika kwa wazazi wake akaitwa lakini akagoma. Huko aliitwa ikiwa ni pamoja na kula sikukuu ya Pasaka. Mamake akataka aende na mkewe lakini huyo jamaa hakumjibu mamake(mkwe) ikabidi awasiliane na mkamwana(mke wa jamaa). Naye akawa anamwambia mama mkwe kwamba hataweza kuja. Ndipo mamamkwe akajua kuna tatizo hapo.

Ikabidi upande wa mwanamke ukaandaa kikao na upande wa jamaa ili kujua kulikoni. Na kweli pande zote zikaitwa mambo yote yakawekwa hadharani na upande wa mwanamke ukaamua binti yao maadam alishakamata vidhibiti na bwana akakiri kuwa na mahusiano nje ya ndoa, akae kando wakati taratibu za talaka zinaandaliwa. Hakika Maisha Ndivyo Yalivyo.

Mpenzi msomaji, si unajua ndoa za siku hizi nyingi ni mfano wa mchezo wa kuigiza? Watu wanataka umaarufu kwamba nilioa au niliolea baada ya hapo mchezo umekwisha. Kwa mtu ambaye ndio kwanza amefunga ndoa, akabahatika kupata mtoto mmoja, kwanini aanze vituko ikiwa ni pamoja na kulala kona na washikaji wengine?

Hili ni tatizo kubwa sana. Na mara nyingi inakuwa kwamba yule aliyeoa au kuolewa kisha akaendelea kuchepuka kona, maana yake penzi haliko pale ndani liko huko vichochoroni. Au siyo?

Mfumo huu wa maisha ndio umechangia ndoa nyingi kuvunjika na kama bado zipo basi hazina amani na ndio maana pia maradhi yanazidi kuteketeza familia kwa kuwa maradhi yale husombwa huko nje ya ndoa.

Watu mmepima virusi, mkaoana kwa raha zenu lakini kutokana na tamaa mnasomba maradhi toka nje mnakandamiziana. Kwanini? Kile kiapo cha ndoa kiko wapi? Hivi tunamdanyanya Mungu madhabahuni?

Ndio maana kwa wale wasiotaka usumbufu, baada ya mwenzake kuonyesha makucha na rangi za tabia, huamua kutengana au kutalikiana mapema ili kila mtu akafe kivyake. Yupo rafiki yangu aliwahi kuniambia “Kuliko mwanaume aniletee virusi au mimi nimletee afadhali tuachane ili kila mmoja akafe kivyake kuepuka aibu ndani ya ndoa”.

Tulikuwa tunazungumzia wale wanaowaacha wake zao wazuri au waume zao, kisha kwenda kujikumbusha na wachuchu(marafiki) wa zamani, bila kujali kuwa ni wazima au walishajeruhiwa. Utasikia wanajipa moyo eti ‘mavi ya kale hayanuki’, ebo! Labda huko zamani, lakini siku hizi usidanganyike, yananuka tena uvundo usioisha. Au siyo msomaji wangu? Maisha Ndivyo Yalivyo, kaa chonjo!

Upo ushahidi ambao umethibitika kwa baadhi ya ndoa zenye mtikisiko kwamba kwa upande wa wanaume wanaotoka nje ya ndoa na kisha kunyanyasa wake zao, wakati mwingine siyo makosa yao.

Kule nje kama ni mtu mwenye kazi na fedha za kutosha, akakutana na mwanamke shangingi anayejua vichochoro vya waganga, basi ajue amekwisha. Hakuna wanawake wabaya kama walioegemea ushirikina, watampumbaza mwanaume hata kufikia hatua ya kuhamia kwake mzima mzima.

Wanaume wa aina hii ndio wale utasikia anamfanyia visa mkewe ili amtibue ahame nyumba kisha amlete huyo dungaembe anayemzuzua huko nje. Matokeo yake analeta msononeko ndani ya familia kama ambavyo tumeona hapo juu.

Waliofanya kituko kama hiki wamejikuta katika majuto na wakati mwingine hata yule aliyeletwa naye huamua kutimua kwa nyumba kumshinda hasa akijua kuwa ilikuwa ni nyumba ya mwanamke mwenzake. Mwisho wa siku lijamaa linabaki lenyewe na kuanza tena kutafuta njia ya kumrejesha mkewe aliyeondoka bila mafanikio.

Mpenzi msomaji, kama mtu ameamua kuingia kwenye ndoa(labda awe alilazimishwa) kwa hiari yake, kwanini aanze vituko ikiwa ni pamoja na kutafuta mahusiano ya nje? Hata kama zipo kasoro baada ya wawili kuingia kwenye mkataba wa ndoa, ni vema zikajadiliwa ili kama ni kuachana ijulikane lakini siyo kufanya visa kumtibua mwenzako kwa tamaa za fisi.

Msomaji wangu, kwa leo niishie hapa upate nawe kuchangia maoni. Ukiwa tayari kuwa huru kuwasiliana nami kwa kutuma ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 0774268581(usipige), au barua pepe; [email protected]

Kumbuka kama hutapenda jina au simu yako itajwe gazetini tamka hivyo na hilo litaheshimiwa.

Wasalaam.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles