


.jpg)
Viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa nyumba za makazi kutokana na nyumba nyingi za serikali kukabiliwa na uchakavu.
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, alisema hayo alipokuwa akizungumza na watendaji wa serikali baada ya kukamilisha ziara ya siku tatu ya kukagua shughuli za maendeleo katika Mkoa wa Kusini Unguja na kwamba tabia ya kutofanyia matengenezo majengo na nyumba za serikali imeanza kuleta madhara makubwa kwa serikali na viongozi wake.
Alisema viongozi na watendaji wakuu wakiwemo mawaziri, makatibu wakuu na majaji wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa nyumba za makazi.
Alisema wakati umefika kwa kila wizara kuwa na utamaduni wa kufanyia mategenezo majengo yake na nyumba za serikali ili kuondoa tatizo na kupunguza matumizi ya serikali ya kukodi nyumba kwa ajili ya matumizi ya viongozi wake.
Alisema kwamba yapo baadhi ya majengo ya serikali hayakaliki kutokana na kukabiliwa na uchakavu, lakini viongozi wameshindwa kuyafanyia matengenezo na kutishi usalama wa wafanyakazi.
Kutokana na hali hiyo, maofisa waandamizi wa serikali wanalazimika kuiishi katika nyumba za kukodi au nyumba zao binafsi na kulipwa kiwango kikubwa cha posho ya nyumba kila mwezi.
Tatizo hilo limekuwa kubwa baada ya Serikali ya awamu ya tano chini ya Dk. Salmin Amou, kuuza nyumba nyingi za serikali kwa bei poa.