Tuesday May 3, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Hongera Simba ubingwa 2011/12, ligi 2012/13 isiwe ya mezani tena

7th May 2012
Print
Comments
Maoni ya katuni

Simba walitwaa ubingwa wao wa 19 wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara bila ya jasho Jumamosi kufuatia Mtibwa kuifunga Azam 2-1 katika mechi iliyorudiwa kwenye Uwanja wa Taifa kufuatia kutomalizika kwa mechi yao ya awali iliyovunjika katika dakika ya 88 kwenye Uwanja wa Chamazi.

Wekundu wa Msimbazi walitarajiwa kuuvujia jasho ubingwa katika siku ya mwisho ya msimu jana dhidi ya mahasimu wao Yanga, lakini maamuzi ya makubwa yaliyofanywa juu ya meza kuhusiana na mechi baina ya Azam na Mtibwa yalikuwa ni neema kwa Wekundu wa Msimbazi.

Vita vya panzi, Azam na Mtibwa, ilikuwa ni neema kwa kunguru Simba, baada ya Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), iliyo chini ya Kamanda Mstaafu wa Polisi, Alfred Tibaigana, kuamua mechi ya wapinzani hao ambayo haikumalizika irudiwe.

Maamuzi hayo yalikuwa ni kinyume na maamuzi yaliyotolewa awali na Kamati ya Ligi ya TFF kwamba Azam ndio wanaostahili kupewa pointi tatu kwa sababu waliosababisha kuvunjika kwa mechi walikuwa ni Mtibwa wakati wakipinga penalti iliyotolewa na refa Rashid Msangi kwa Azam katika dakika ya 88 wakati matokeo yakiwa ni 1-1.

Kamati ya Tibaigana ikaamua kwamba mechi hiyo irudiwe, kufuatia rufaa iliyowasilishwa na African Lyon, kwa sababu wachezaji wa Mtibwa hawakutoka uwanjani na wala hawakuvunja pambano na kwamba aliyekosea ni refa, kama ambavyo Kamati ya Ligi iliona pia na kumfuta katika orodha ya marefa wa ligi kuu.

Lakini cha kushangaza, maamuzi ya mezani, yakaamua kwamba mechi hiyo irudiwe kwenye uwanja tofauti na Chamazi. Mechi ikarudiwa kwenye Uwanja wa Taifa.

Swali linakuja hapa. Kwanini mechi hiyo ilihamishwa kutoka Chamazi na kupelekwa kwenye Uwanja wa Taifa?

Je kamati ya Tibaigana ilibaini nini hadi ikaamua kuihamisha mechi hiyo? Je Ilibaini kwamba rushwa ilitumika katika mechi ya awali ndio maana wakaihamisha?

Kama ilibaini kuna rushwa, kwanini hawakuishirikisha taasisi inayohusika na kupambana na rushwa (TAKUKURU) iingilie ili kukomesha suala hilo ? Kwani kuna gharama yoyote kuiomba TAKUKURU iingilie kuchunguza tuhuma za rushwa? Kwani TFF haitaki kuona soka la Tanzania linasonga mbele kwa kuzima kabisa mianya ya rushwa?

Na kama hapakuwa na rushwa na wala hawaihitaji TAKUKURU, kwanini waliihamisha mechi hiyo?

Je nani leo atashangaa kama Azam nao watarudi kucheza soka la mezani na kuwasilisha rufaa ya kupinga kunyang'anywa haki yao ya kucheza mechi yao ya marudiano kwenye uwanja wao wa nyumbani?

Hapa ndipo madhara ya ligi kuchezwa mezani yanapoonekana. Imefika wakati sasa klabu ziamke, zisiruhusu mianya yoyote ya kufanya mechi ije iamuliwe juu ya meza.

Maamuzi ya juu ya meza ndiyo yaliyoharibu kampeni za Yanga msimu huu na kuwafanya wapoteze mwelekeo.

Awali, baada ya mechi yao dhidi ya Azam, ambayo ilishuhudia mwamuzi Israel Nkongo akipigwa ngumi na beki wa Yanga, Stephano Mwasika, Kamati ya Ligi ya TFF ilitoa adhabu kubwa kubwa kwa wachezaji waliohusika na vurugu hizo, lakini kamati ya Tibaigana tena ikazipunguza.

Ugonjwa wa ligi za mezani ulionekana kuwaingia akilini Yanga ambao waliamua kumtumia beki Nadir Haroub 'Cannavaro' aliyekuwa amefungiwa mechi tatu katika mechi yao waliyoshinda 1-0 dhidi ya Coastal Union ugenini Tanga na kujikuta wakipigwa tena juu ya meza kwa kunyang'anywa pointi zao ambazo walipewa Coastal na kuwafanya wachanganyikiwe kabisa hadi kutema ubingwa waliokuwa wakiutetea.

Ni nani sasa wa kujipanga ili ligi isiathiriwe na maamuzi ya mezani? Ni kila mmoja. TFF, klabu, viongozi wa klabu hadi mashabiki. Kila mmoja anapaswa kutambua kwamba mechi inapaswa kumalizika uwanjani na sio juu ya meza.

Tumeshashuhudia mifano kutoka kwa wenzetu waliotutangulia katika mchezo huu unaopendwa kuliko michezo yote duniani, maamuzi ya uwanjani yanabaki kama yalivyo, kwa kuwa wanajua kwamba kama mshambuliaji nyota kabisa duniani anaweza kukosea na kushindwa kufunga katika goli tupu kwanini refa asikosee wakati wote ni binadamu?

Jambo la msingi linalochunguzwa hapo ni iwapo rushwa imeingia.

Taasisi husika inapaswa kuitwa kufanya kazi yake kwa ni ya kuokoa mchezo huu ambao unadidimia kila uchao huku kila tukiamka tunaikuta Tanzania imeanguka katika viwango vya FIFA vya ubora wa soka duniani.

Ni shabiki gani aliye tayari kulipa kiingilio chake uwanjani huku akijua kwamba matokeo ya uwanjani hapo sio ya mwisho kwamba kuna watu watakaokuja kukaa mezani na kutoa matokeo ya mechi hiyo?

Ni wakati sasa wa mabadiliko. Tusiwakatishe tamaa mashabiki kwenda viwanjani. Ni wakati wa kuwashawishi kwamba mechi ikimalizika uwanjani hapatakuwa na mechi nyingine mezani.
Hongera Simba kwa kucheza mpira uwanjani na kutwaa ubingwa 2011/12.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles