


Mwili wa aliyekuwa Mhariri Mkuu wa gazeti la Jambo Leo, Willy Edward Obunde, umezikwa jana nyumbani kwao katika kijiji cha Morotonga, nje kidogo ya mji wa Mugumu mkoani Mara.
Mazishi ya Mhariri huyo yalihudhuriwa na Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, waandishi wa habari, viongozi wa serikali wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Serengeti kapteni mstaafu James Ryamungu, viongozi wa vyama vya siasa, madhebu ya dini, pamoja na wananchi mbalimbali.
Aidha, mazishi ya mhariri huyo, pia yalihudhuriwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Shinyanga, Khamis Mugeja pamoja mkuu mpya wa wilaya ya Magu, ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari Bi. Jacquline Liana.
Ibada ya mazishi hayo iliongozwa na Askofu wa kanisa la Anglikana Dayosisi ya Mara, Hilkiah Omindo, ambaye aliwataka wananchi kujiandaa kwa kufanya matendo mema na kumtumikia mwenyezi Mungu.
Akitoa salamu kwa niaba ya CCM na wananchi wa mkoa wa Shinyanga, Mwenyekiti wa CCM, mkoani Shinyanga, Khamisi Mugeja, amesema kuwa waandishi wa habari wamepata pigo kubwa kwa kuondokewa na mwenzao ambaye alikuwa ni mchapakazi, mwadilifu na anayefuata maadili na weledi wa uandishi wa habari.
Willy Edward (38) alifariki dunia ghafla akiwa mkoani Morogoro, usiku wa kuamkia Juni 17, mwaka huu, wakati akiwa kwenye semina ya uandishi wa habari za Sensa ya watu na makazi.