


CWT kutoa tamko lake leo
Mahakama Kuu Tanzania, Divisheni ya Kazi imewaduwaza walimu nchini baada ya kutoa uamuzi wa kutaka mgomo ulioitishwa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) usitishwe mara moja na walimu warejee kazini kwa kuwa ulikuwa ni batili.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji wa Mahakama hiyo, Sophia Wambura, baada ya juzi kusikiliza madai ya upande wa Jamhuri na CWT.
Aidha, katika uamuzi wake jana, Jaji Wambura ameiamuru CWT kuwatangazia walimu kwamba hakuna mgomo hivyo warejee kazini.
Jaji Wambura alisema mgomo huo ni batili kwa sababu CWT ilitakiwa kutoa taarifa ya saa 48 kwa mwajiri wao (Serikali) ili alinde mali zake, lakini chama hicho kilitangaza mgomo Julai 27, mwaka huu siku ya mapumziko.
Jaji Wambura alisema mgomo huo ulianza Julai 30, mwaka huu siku ya Jumatatu kabla saa 48 hazijatimia na hivyo mwajiri ambaye ni Serikali, hakupata muda wa kulinda mali zake.
Jaji Wambura alisema sababu ya pili ambayo Mahakama imeona ni kuwa mgomo huo haukuwa halali, CWT hawakutangaza kikomo cha mgomo huo kwamba utakuwa wa muda gani na upigaji wa kura za kuunga mkono zoezi hilo haukukamilika kwa wanachama wote wa chama hicho.
“Mgomo uliotangazwa ni batili kwa sababu CWT kilikiuka sheria ambayo inawataka kutoa taarifa kwa muda wa saa 48,” alisema Jaji na kuongeza: “Mahakama inawaamuru viongozi wa chama hicho kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwatangazia kuwa hakuna mgomo na warejee kazini.”
Aidha, Jaji Wambura ameiamuru CWT ilipe hasara ambayo serikali imepata kutokana na mgomo huo pamoja na kuwafidia wanafunzi wote nchini tangu mgomo huo ulipoanza Julai 30, mwaka huu na kudumu kwa siku nne mfululizo.
CWT KUTOA TAMKO LEO
Baada ya uamuzi huo kutolewa, Kaimu Katibu Mkuu wa CWT, Ezekiah Oluoch, alisema chama chake kitaandaa taarifa na kuitoa kwa vyombo vya habari leo.
Uamuzi huo wa Mahakama umekuja siku moja baada ya Rais Jakaya Kikwete, kueleza kuwa madai yao ya walimu wanayoidai Serikali hayalipiki.
WALIMU WAMJIBU JK
Hata hivyo, kabla ya uamuzi wa Mahakama, CWT ilieleza kufurahishwa na kauli ya Rais Kikwete, kwamba serikali inayatambua madai hayo.
Oluoch aliiambia NIPASHE kuwa chama hicho kinampongeza Rais Kikwete, kwa kutowapuuza walimu kwani kauli yake imeleta matumaini kwao.
“Tunampongeza Rais kwa mambo kadhaa….kauli ya kutowapuuza walimu, maana huko nyuma tulikuwa tukipuuzwa sana na serikali. Pia tumefurahishwa na kauli yake ya kusema kwamba majadiliano yanaendelea kwani tangu Juni, mwaka jana tulitaka tuingie kwenye majadiliano, lakini haikuwezekana,” alisema Oluoch.
Hata hivyo, alimuomba Rais Kikwete, aonyeshe kwa vitendo kwa kuyapatia ufumbuzi madai ya walimu.
Aidha, Oluoch alipinga madai kwamba walimu waliogoma wanawachochea wanafunzi katika shule mbalimbali nchini kufanya maandaano na kwamba huko ni kuwapaka matope kwani waliogoma wapo majumbani.
Naibu Katibu Mkuu huyo alipinga madai kwamba Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kiko nyuma ya mgogoro huo.
“Mgogoro wa walimu hauna mkono wa Chadema wala chama chochote cha siasa. Serikali inataka kuhamisha ajenda yetu kwenda kwenye mambo ya siasa,” alisema Oluoch.
HAKI ELIMU YATAKA SERIKALI ISIBEZE WALIMU
Shirika la HakiElimu limeitaka serikali kushughulikia madai ya walimu badala ya kuwabeza na kuwapa vitisho.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Elizabeth Missokia, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, alisema hakuna sababu kwa serikali kutoa vitisho kwa walimu wakati CWT kilichukua uamuzi wa kuitisha mgomo baada ya suluhu kushindikana.
“Serikali inatakiwa kushughulikia haraka madai ya walimu pamoja na kuangalia vyanzo mbadala vya mapato vinavyoweza kutoa suluhu ya madai ya walimu yanayosababisha kuwepo kwa mgomo nchini badala ya kuwaeleza kuwa uwezo haupo, hatua ambayo inaweza kupunguza mori wa ufundishaji,” alisema Missokia.
Missokia alisema kauli ya serikali kwamba madai ya walimu hayalipiki, italeta athari kwani hata mgomo ukimalizika walimu wanaweza kurejea kazini wakiwa na kinyongo hali inayoweza kusababisha mazingira ya kuendeleza mgomo baridi.
Alisema inawekana kabisa kwamba serikali haina uwezo kuyatekeleza madai hayo kwa sasa, lakini madai ya walimu ni ya muda mrefu na ambayo yanahitaji kutatuliwa.
“Siyo kwamba walimu hawaoni ama kusikia mambo yanayoendelea nchini kuhusiana na ufisadi, madai yao ni haki yao ya msingi, serikali iweke malengo na mikakati ya kuyashughulikia kwa kuwa ndiyo njia mwafaka na ya haraka ya kuiletea nchi maendeleo,” alisema Missokia.
Kadhalika, shirika hilo liliwakumbusha walimu kutimiza wajibu wao wa kufundisha kwa bidii bila kinyongo kwa kuwa wasipofanya hivyo wanawaumiza wanafunzi kwani mgogoro uliopo ni baina ya walimu na serikali na na siyo wanafunzi.
SHULE ZAFUNGWA DAR
Mgomo wa walimu katika shule za msingi na sekondari katika Jiji la Dar es Salaam, bado ni tete kutokana na shule nyingi kuendelea kubakiwa na walimu wakuu na wakuu wa shule pekee huku nyingine zikifungwa.
Katika Shule ya Sekondari Kambangwa iliyopo katika Manispaa ya Kinondoni, NIPASHE jana ilikuta wanafunzi wakicheza mpira kutokana na walimu wao kugoma kuingia madarasani kufundisha.
Katika shule za msingi za Kinondoni na Msisiri, hali bado ni mbaya kutokana na shule hizo kutokuwa na walimu kabisa ikiwa ni siku ya nne tangu mgomo huo utangazwe.
Katika Shule za Msingi Ruvuma na Madenge, wilayani Temeke, NIPASHE ilikuta madarasa pamoja na ofisi za walimu zimefungwa na makufuli nyakati za mchana.
Shule nyingine zilizoonekana kuwa wazi ni pamoja na Shule za Msingi Bahati, Temeke, Muungano, Jeika, Tabata, Ndarara, Mtambani, ambazo wanafunzi wachache wa darasa la saba ndiyo walionekana wakijisomea.
Wanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Ruvuma, walisema tangu mgomo uanze wamekuwa wakitozwa fedha kwa ajili ya kufundishwa.
Kwa mujibu wa wanafunzi hao, katika kila somo moja wamekuwa wakitozwa Sh. 300 katika vipindi vya asubuhi ili wafundishwe.
262 BUNDA HAWAKUGOMA
Wakati mgomo wa walimu ukiwa umeingia siku ya tatu, walimu 262 wa shule za msingi wilayani Bunda mkoani Mara hawajashiriki.
Afisa Elimu wa Shule za Msingi wilayani hapa, Rabani Bituro, alisema katika wilaya hiyo walimu waliogoma ni 1,269 na 262 hawakugoma.
Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kwamba walimu ambao hawaingii madarasani hufika asubuhi kwenye vituo vyao vya kazi na kusaini kitabu cha mahudhurio na kisha kukaa ofisini.
UKEREWE WALIA SERIKALI KUTUMIA MAHAKAMA
CWT wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, kimeilaumu serikali kwa kushindwa kutimiza madai ya watumishi, badala yake inakimbilia mahakamani kuwaziba midomo ili wasidai haki na maslahi bora.
Katibu wa CWT wilayani Ukerewe, John Kafimbi, alisema wakati umefika sasa serikali kuacha kutumia mahakama kama kichaka cha kujificha kwa sababu zuio la mahakama na vitisho, ni suala la muda na si suluhu ya kudumu ya mvutano uliopo kati yake na watumishi wa umma.
Katika hatua nyingine, CWT kimedai kuwa kimenasa barua ya serikali waliyoandikiwa makatibu tawala wa mikoa na wilaya Tanzania bara ikitoa agizo kwa kutumia vyombo vya dola kudhibiti walimu.
Kafimbi amesema barua hiyo ya Julai 27, mwaka huu yenye kumb. Na. CHA.121/385/01/12 iliyosainiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, J.A . Sagini pamoja na mambo mengine, inawataka makatibu tawala wa mikoa na wilaya kuhakikisha kuwa hakuna mgomo wa walimu katika maeneo yao.
WALIMU MTWARA WATAFAKARI
Walimu katika shule za msingi za mkoa wa Mtwara, wamedai kuwa kauli ya serikali imewakatisha tamaa ya kuendelea kufundisha.
Imeandaliwa na Hellen Mwango, Jacqueliene Yeuda, Isaya Kisimbilu, Zainabu Ngambila, Elizabeth Zaya, Gwamaka Alipipi, Thobias Mwanakatwe, Dar; Jovither Kaijage; Ukerewe, Ahmed Makongo; Bunda na Happy Severine, Mtwara.