Friday Apr 29, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Wasomi wanapolipuuza Baraza la Mawaziri, nani alaumiwe?

12th May 2012
Print
Comments

Nimesikia kupitia vyombo mbalimbali vya habari na kusoma kwenye baadhi ya magazeti kwamba kada ya wasomi wanabeza kufanyika kwa mabadiliko ya mawaziri kwa maana kwamba tatizo sio Baraza la Mawaziri bali ni Muundo wa Serikali yetu.

Tamko hili la kada ya wasomi limekuja siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kuridhia mapendekezo ya wabunge waliotoa bungeni ya nini kifanyike kurekebisha kasoro zilizojitokeza, ambapo ilitolewa rai Mawaziri wawajibike na kama wakishindwa wawajibishwe.

Itakumbukwas kwamba Rais Kikwete alitoa ahadi ya kutekeleza mapendekezo ya wabunge na kilio cha  jamii kilikuwa (Rais) awawajibishe mawaziri wote walioguswa na ripoti ya CAG.

Napata taabu kuelewa mukhtadha waliyojenga wasomi wetu hatimaye kutoa tamko la kuwepo marekebisho la muundo wa serikali, badala ya kung’ang’ania mabadiliko ya Baraza la Mawaziri.

Kwa sababu dhana ya muundo au mfumo wa serikali katika mukhatadha wa utekelezaji na uwajibikaji unategemea mihimili mikuu ya serikali kama ilivyoanishwa kwenye katiba.

Sijaelewa mantiki ya kada hii ya wasomi kwa sababu serikali nyingi za kiafrika baada ya kupata uhuru walianzisha muundo wa serikali ya uwakilishi. Mataifa mengine machache yalianzisha muundo wa utawala wa kifalme.

Serikali ya uwakilishi kwa uelewa wangu, ni ile ambayo serikali yake inatumia mtawanyo wa madaraka kupitia serikali za mitaa zaidi kuliko serikali kuu.

Huu ni muundo wa utekelezaji wa shughuli za serikali ulioanzishwa ili huduma za serikali ziwafikie walengwa wa chini kwa uepesi na kwa ufanisi.

Muundo mwingine wa serikali kisiasa ni ule wa uwakilishi wa Baraza la Bunge moja. badala ya Baraza la Bunge mbili. Nchi yetu inafuata mfumo wa Bunge moja.

Wakati baadhi ya wasomi wakikosoa uteuzi mpya eti tatizo siyo mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, bali ni mfumo mzima wa uongozi serikalini sijui wana maana ya mfumo gani kati ya hizo nilizotaja.

Nionavyo mimi, tatizo siyo mfumo serikalini bali ni kama wanavyodai wasomi wetu mabadiliko ya mfumo wa fikra/mawazo ya Watanzania wengi katika karne hii ya 21 hususani vijana wasomi ambao wengi wamepoteza dira na uzalendo, wakiamini kwamba serikalini ndiko kuna hela ya kutumbua haraka katika maisha ya sasa.

Napenda kutofautiana kidogo na maoni yaliyotolewa na baadhi ya wasomi wakati wakichambua mabadiliko ya Baraza jipya la mawaziri, eti ni mfumo ni mbovu, siyo sahihi, kwa sababu muundo unatumika serikalini hapa kwetu haina tofauti na muundo unaotumiwa na mataifa mengi barani Afrika na kwingineko katika mabara mengine duniani.

Isipokuwa baada ya kufanya utafiti kwa muda sasa ambayo yalijikita katika kutafuta kiini cha ufisadi unaoikumba mataifa mengi za kiafrika, nimebaini kwamba inatokana na mabadiliko ya mawazo ya watanzania walio wengi wakiongozwa na vijana wasomi ambao wameweka mbele zaidi maslahi binafsi kuliko uzalendo na utaifa.

Mabadiliko yaliyofanyika Zanzibar na kusababisha Azimio la Arusha kuvunjwa, yalizidi kuzika baadhi ya miongozo na maadili.

Hali hii ya kuzika miongozo hajakuishia kwa watendaji tu bali ilivuka na kutua vyuoni na kuambukiza wasomi ugonjwa wa kutafuta utajiri wa haraka kwa njia zozote za kihalali au kwa njia ya ufisadi uli mradi kwenda na wakati.

Ili kuweza kufanikisha azma ya kupata utajiri kwa muda mfupi, vijana wengi wasomi wanadiriki kukacha fani zao walizosomea, huku wakihaha kutafuta ajira kwenye maeneo ambako wanayoyaita mazuri ya kujipatia maisha kwa njia ya haraka, husasan Ubunge.

Kwa upande mwingine nakubaliana nao (wasomi) kimtizamo pale wanaposema kuwa hata kama mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yatafanyiwa marekebisho kila mara, bado tatizo litaendelea tu ya ufisadi. Mawazo yao ni sahihi kwa sababu vijana wengi wamekimbilia ubunge na kuacha taaluma zao.

Hawa vijana ndio wengi wanateuliwa katika nafasi hizo za uwaziri sasa utategemea nini kutoka kwa mawaziri wakati wengi wao ndio hao vijana wenye mawazo mapya ya kutafuta utajiri wa haraka. Kwa hali kama hii kwanini masuala ya ufisadi yasitokee.

Niseme tu kwamba, mabadiliko ya kisiasa katika karne hii ya 21, imeleta sura ya upendeleo kwa vijana zaidi. Matokeo yake, vijana wanatumia fursa hizi walizopata vibaya huku serikali ikibaki kulaumiwa na wananachi.

Mbaya zaidi ni kwamba, wengi wa vijana hawa wanaopewa nafasi za uwaziri, ni wale wanatoka katika familia hizo za wakubwa. Hawaogopi kwasababu wana kinga za wakubwa.

Kwa maana nyingine ni kweli kama wanavyodai baadhi ya wasomi kwamba, mabadiliko yaliyotangazwa la baraza jipya ya mawaziri haitakuja na jipya zaidi ya kuendeleza ufisadi mawizarani.

Ukweli huu unakuja kwa sababu vijana wengi wanaotoka vyuoni, hawataki kujiajiri. Wengi wanatafuta maeneo yenye maslahi kimaisha aidha serikali ni au kwenye makampuni makubwa kama Vodacom, Zain, mabenki, Tigo na mashirika mengine yenye maslahi.

Kama nchi ikiendelea kupata uzao huu ambao hawana uchungu wala uzalendo, aidha uzao ambao unaweka taaluma zao kwapani ilimradi waweze kupata kazi zenye kuleta utajiri wa haraka, ni wapi tutawapata hao mawaziri watakatifu ambao wangependa kuuliza wataifanyia nini nchi badala ya nchi kuwafanyia nini.

Ebu tujiulize waziri kijana anapata wapi hela ya 1.8 Bilioni ya kununua nyumba kwa fedha taslimu.

Tatizo hili la ufisadi siyo tu inaikumba nchi yetu la hasha. Rais Kikwete ataendelea kulaumiwa kwamba ameshindwa kuwashughulikia hao wanaoitwa mafisadi lakini kwanini sisi wenyewe hatujiulizi swali kwamba;

Je, mafisadi hawa wanatoka wapi kama siyo miongoni mwetu au kwenye familia zetu? Kwanini wananchi wasiisadie serikali kuwakemea hawa watu wakati tunakula nao, tunalala nao na tunaserebuka pamoja kila siku?

Kasumba hii ya kuitwisha serikali mzigo wa kupambana na mafisadi huku ikiacha majukumu yake ya kutoa huduma za lazima kwa wananchi, ingefaa ipatiwe ufumbuzi kwa ushirikiano wa pande zote mbili (serikali na wananchi).

Tusijidanganye mafisadi tunawajua na wengine ni baba zetu, wajomba, wakwe, mama, dada na wengine ni viongozi waandamizi serikalini.

Jamii inafanya nini kusaidia serikali kufichua hao wahalifu wa mali za umma. Nasema kwambas hata yafanyike mabadiliko ya baraza lote la mawaziri na wakaingia wapya wote, bado tutaendelea kuilalamikia serikali kwa sababu jamii ndio wanaochochea watu wa aina hii kuendelea kutafunas fedha za umma.

Jamii ifike mahala waseme basi, wasiwaonee aibu hawa watu wachache wanaoneemeka kupitia mgongo wa walalahoi.

Nasema bila kumumunya maneno kwamba, hata angekuja Rais mwingine ‘mtakatifu’ kutoka nje ya nchi au kutoka chama kingine mbadala ya CCM, kama vijana wasomi wetu hawa bado wataendelea kuendeleza ubinafsi, uroho wa madaraka na utajiri wa haraka, tusitarajie falsafa ya maisha bora kwa kila mtanzania ikitimia.

Tutaendelea kuilaumu Rais Kikwete na serikali yake, Rais atabadilisha Baraza la Mawaziri na watendaji kila kukicha, lakini bila sisi wananchi kufika mahala na kuamua kuwatolea uvivu hawa mafisadi wanaotoka kwenye familia zetu, hakika hatutakuwa tunaitendea haki serikali ya Rais Kikwete.

Hata  kama Baraza la Mawaziri litasheheni maprofesa au madaktari wa (PHD), lakini bila msaada wa wanainchi bado itakuwa ni kazi bure. Kikubwa ni vijana wasomi kubadilisha mfumo wa fikra ambazo zina mwelekeo wa kikaptalisti (utajiri wa haraka hata kama inaumiza walio wengi).

Vinginevyo tutaendelea kushuhudia mvutano na ombwe kubwa kati ya serikali na wananchi ikiongezeka huku majibu ya matatizo tukiyaacha kushughulikia.

Katiba yetu Ibara ya 8 (a) inaipa nguvu wananchi dhidi ya serikali yao. Inatamka hivi; “wananchi ndio msingi wa mamlaka yote na serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi.” Kifungu kidogo (c) kinasema; serikali itawajibika kwa wananchi (d) wananchi watashiriki katika shughuli za serikali yao.”

Kwa mujibu wa katiba, wananchi wamepewa jukumu la kusimamia serikali kupitia kwa wawakilishi wao (wabunge).

Ni vema basi wananchi wakaanzia kwenye majimbo yao kuwaadibisha wawakilishi wanaowajua ni mafisadi. Haipendezi pale wananchi wanapokubali kumchagua Mbunge mfisadi halafu kesho wanamyooshea Rais kidole kwamba amewateua mawaziri mafisadi.

Rais anateua mawaziri kutoka miongoni mwa wabunge waliochaguliwa kutoka majimboni Rais hana mawaziri kutoka mfukoni mwake. Inapotokea wananchi wakamchagua mbunge mafisadi na kwa bahati akateuliwa kuwa waziri, kosa la Rais inatoka wapi.

Lawama hizi anazotupiwa Rais Kikwete zinatoka wapi kama siyo wananchi pia wanashiriki katika kuchagua wabunge wabovu.

Njia pekee nyoofu ni wananchi kusaidiana na serikali kuwafichua wabunge mafisadi na watendaji wabovu serikalini. Vinginevyo kilio chetu kitaishia majini (kilio cha samaki machozi yote huishia majini). Nani alaumiwe kama siyo wananchi katika ngazi ya majimbo na vijana wetu wasomi.

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwenye simu namba 0713 399004 au 0767 399004 ama barua pepe; [email protected]

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles