Wednesday May 22, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Tusimame kama taifa, tuilinde mipaka yetu

5th August 2012
Print
Comments
Maoni ya Katuni

Hivi sasa vyombo vya habari vya ndani, ukanda wa Afrika na duniani, vinaandika na kutangaza kuhusu mzozo wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi, eneo la Ziwa Nyasa.

Serikali ya Malawi imekaririwa mara kadhaa, ikielezea kuwa mpaka unaotambulika hata kwa Umoja wa Afrika (AU) ni ule unaolifanya Ziwa Nyasa ambalo upande wao wanaliita Ziwa Malawi, ni mali yao.

Kwa karne na karne sasa, sehemu ya mpaka unaojulikana katika mzozo huo, ni eneo la katikati ya Ziwa Nyasa. Ndivyo ilivyo hata kwa sheria za kimataifa, ingawa Malawi kupitia wasemaji wake kadhaa, imekaririwa ikikaidi kuzitambua.

Si nia yetu kutaka mzozo huo uzidi kushamiri, tunatambua nafasi ya Tanzania katika kuhimiza na kufanikisha njia za mazungumzo katika kupata suluhu ya matatizo yaliyozikabili na yanayoendelea kuzikabili baadhi ya nchi barani Afrika.

Hivyo kwa kutumia uwezo huo, tunaamini kwamba serikali kupitia mamlaka husika, itachukua na kutumia njia za kidiplomasia, kuhakikisha kuwa mzozo wa mpaka unaoweza kutishia usalama na uhusiano kati ya Tanzania na Malawi, unapatiwa suluhu ya kudumu.

Wakati wa tawala za marais wa kwanza, Kamuzu Banda wa Malawi na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania (wote ni marehemu na Mwenyezi Mungu azidi kuwalaza mahali pema peponi-AMINA), mzozo wa mpaka kati ya pande mbili hizo uliotokea.

Serikali ya Banda ilitangaza kuchukua Ziwa Nyasa na sehemu ya mkoa wa Ruvuma, kuwa eneo la nchi yake. Mwalimu Nyerere alitumia kauli thabiti, akalitangazia taifa na ulimwengu, kwa kauli ambayo iliheshimika, kwamba eneo lote la Ruvuma na sehemu ya kufikia katikati ya Ziwa Nyasa, ni mali ya Tanzania.

Sasa Malawi imeibuka na madai hayo yanayogusa hisia za taifa kwamba sehemu ya eneo la nchi, inataka ‘kuporwa’ ili ihamishiwe nchini Malawi.

 

Hapo hakuna sababu ya kutoamini kwamba, maslahi ya nchi yanaguswa. Rasilimali ya nchi inachezewa kwa nia ya kutaka kuwadhoofisha Watanzania.

Ziwa Nyasa linatoa samaki wa aina tofauti, wanaovuliwa na Watanzania na kuuzwa na Watanzania, wakinunuliwa na Watanzania kwenye masoko mbalimbali yaliyopo Tanzania.

Ziwa Nyasa linatoa maji yanayotumika kwa shughuli mbalimbali za kibinadamu. Sehemu ya Ziwa hilo ni mali ya Tanzania, ukweli usiotakiwa kupewa mwanya wa kupotoshwa.

Kwa hali hiyo, inapotokea Malawi inachochea hisia za kutaka Ziwa Nyasa linalosadikiwa pia kuwa na gesi chini yake, Watanzania wanapaswa kusimama pamoja na kusema-Hapana.

Tuseme hapana kupitia njia za kidiplomasia na kuiambia Malawi iachane na mzaha inayoufanya, ili amani ipate kudumu katika ukanda wa Kusini mwa Afrika.

Katika hali inayoashiria lipo jambo, hata ofisi ya Ubalozi wa Malawi nchini ilipotakiwa kuthibitisha juu ya madai ya serikali yake kuwa , madai kuwa imewafukuza Watanzania wanaoishi kwenye mwambao wa Ziwa Nyasa, kwa madai kuwa ziwa hilo ni mali ya taifa hilo kwa asilimia 100, ilikwepa kwa kueleza kuwa haina la kusema juu ya taarifa hizo.

Chokochoko hizi zinajitokeza baada ya kuwepo taarifa kuwa Malawi imeanza utafutaji wa gesi na mafuta kwenye ziwa Nyasa na kusababisha nchi hiyo inayopakana na mikoa ya Ruvuma , Iringa na Mbeya kudai kuwa ziwa hilo ni mali yake.

Taarifa ya Serikali juu ya mgogoro huo inasubiriwa kutolewa bungeni kesho na Waziri wa Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Wakati tukisubiri msimamo huo wa serikali yetu, tunaungana nao Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Samweli Sitta kuwataka wakazi wa mikoa ya mpakani na Malawi ambayo ni Iringa, Mbeya na Ruvuma kuendelea na kazi zao kwa serikali iko imara. Tusimame imara kama taifa kulinda mipaka ya nchi yetu kwa nguvu zetu zote. Mungu ibariki Tanzania, Ibariki Afrika na watu wake.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment