


.jpg)
Taifa Stars inakabiliwa na mechi ngumu dhidi ya wenyeji Ivory Coast ya michuano ya awali ya Kombe la Dunia kanda ya Afrika huku ikifahamu kuwa iliwahi kutoka nayo 1-1 mwaka 1980 nchini Nigeria, lakini
matumaini ya sare nyingine muhimu leo yatategemea kama mbinu za kocha Kim Poulsen zitafanya kazi.
Akizungumzia pambano hilo litakalochezwa kwenye uwanja wa Houphouet-Boigny Poulsen alisema hana mpango maalumu wa kudhibiti mchezaji mmoja mmoja wa Ivory Coast.
Ivory Coat ina wachezaji wengi nyota wa kulipwa wa Ulaya lakini itaongozwa na mshambuliaji hatari Didier Drogba na Salomon Kalou ambao wametoka kutwaa taji la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
Pia ina Yaya Toure na kaka yake Kolo Toure ambao timu yao ya Manchester City ilitwaa ubingwa wa kwanza wa Uingereza katika miaka 44 mwezi uliopita.
“Tutacheza kwa nidhamu katika ulinzi na tutakuwa tunaangalia namna ya kubadilika kadri mechi inavyokwenda,” alisema.
Inaweza kuwa mbinu ya hatari kwa Taifa Stars ambayo rekodi zinaonyesha imecheza na Ivory Coast mechi mbili za kimataifa zinazotambuliwa na FIFA.
Katika michezo hiyo, zilitoka sare hiyo ya bao 1-1 Machi 15, 1980 katika hatua ya makundi ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika lakini ikafungwa 1-0 nyumbani Januari 4, 2010 wakati wenyeji hawa wakiwa njiani kwenda Afrika Kusini kucheza fainali za Kombe la Dunia.
Stars na Ivory Coast zipo katika Kundi C la michuano ya awali ambapo Jumatano itaikaribisha Gambia katika mchezo wa pili Dar es Salaam.
Washindi wa makundi 10 ya michuano ya awali watacheza hatua ya mtoano kupata timu tano zitakazoiwaklisha Afrika kwenye fainali za Kombe la Dunia za Brazili 2014.
Poulsen aliseme kikosi chake hakitishiki na majina makubwa ya Ivory Coast.