Wednesday Jun 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Bunge linapokuwa upenyo wa rushwa!

29th July 2012
Print
Comments
Spika wa Bunge, Anne Makinda

Spika wa Bunge, Anne Makinda, ametangaza kuivunja Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, ikiwa ni matokeo ya shinikizo la wabunge waadilifu, wanaoishutumu imekithiri kwa rushwa.

Hoja iliyowasilishwa na Mbunge wa Namtumbo (CCM), Vita Kawawa, ikiwa ni mwendelezo wa kilio cha wabunge waadilifu, ikaungwa mkono na Makinda kupitia kanuni ya 5(1) inayompa mamlaka hayo, akatangaza hivyo.

Kwa hali hiyo, Makinda anaweza kuonekana shujaa na kiongozi imara mwenye dhamira ya kuimarisha heshima na hadhi ya Bunge, hasa aliposema ‘wabunge wakihusishwa na rushwa, hawawezi kuisimamia vyema serikali.’

Kuukubali upepo wa mabadiliko unaovumishwa na baadhi ya wabunge wanaojitoa nje ya ‘blanketi la umoja ndani ya chama cha siasa’ ni hatua ya kupongezwa, vinginevyo Makinda anaweza kukutana na shinikizo la kupigiwa kura ya wabunge kutokuwa na imani naye.

Lakini kwa tukio karibu na shughuli za Bunge na wanafuatilia mwenendo wa wawakilishi hao wa wananchi, wanatambua uwepo wa tuhuma za rushwa dhidi ya wabunge.

Tatizo hilo ni sugu, limedumu muda mrefu kiasi cha kuwa mazoea katika kuomba na kupokea rushwa ili ushawishi ndani ya Bunge ufanikiwe.

Hivi karibuni, niliwahi kuzungumza na aliyekuwa Mbunge wa Karatu na Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAT) Dk Wilbroad Slaa, akasema suala la rushwa kwa wabunge limedumu kwa muda mrefu.

Akatoa mfano kuwa akiwa Mwenyekiti wa kamati hiyo, aliwahi kupata malalamiko kutoka kwa baadhi ya watu wakiwemo Wakurugenzi Watendaji wa wilaya kadhaa, kwamba wajumbe wake walikuwa wanaomba rushwa.

Dk Slaa akiwataja kwa majina, alisema baadhi ya wabunge walifikia hatua ya kutumia jina lake, ili kushawishi kutolewa rushwa. Akawaonya.

 

Mwaka 2010, nilikuwa miongoni mwa waandishi wa habari walioshiriki ziara ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, iliyoongozwa na Job Ndugai ambaye hivi sasa ni Naibu Spika.

Tuhuma kama zinazozungumzwa sasa bungeni zilisikika wakati wa ziara ile, ilipokwenda kushughulikia mgogoro wa kuchomwa makazi ya wafugaji wa Kimasai, maarufu kama maboma.

Wapo miongoni mwa wajumbe wa ‘kamati ya Ndugai’ walifikia hatua ya kuwakaripia, kuwasuta na kuwaonya Wamasai waliokuwa wanamshutumu mwekazaji, kampuni ya Ortello Business Corporation (OBC).

Walipotokea Wamasai walisadikiwa ‘kupandikizwa’ ili waelezee mazuri ya mwekezaji huyo na kukanusha madai ya kushiriki kuwachomea makazi yao, miongoni mwa wajumbe wa ‘kamati ya Ndugai’ waliwapongeza, wakawapigia makofi.

Hapo ilijengeka hisia ya kimazingira zilizoashiria kuwepo ‘harufu ya rushwa’. Hata sasa ninapoandika makala haya, ripoti ya ‘Kamati ya Ndugai’ haijawasilishwa kusomwa na kujadiliwa bungeni. Kuna nini?

Nilipowasiliana na Mbunge wa Ludewa (CCM), Deo Filikunjombe, akasema binafsi alifuatwa na Mbunge ‘dalali’ wa rushwa, akimuahidi Dola 10,000 za Marekani ikiwa atakubali kuchangia, akimshutumu Profesa Muhongo na Maswi.

Kwamba angepewa Dola 5,000 kabla ya kuchangia na baada ya kutoa mchango angemaliziwa Dola 5,000! Filikunjombe akakataa.

Mifano hiyo michache inaweza kuwa sehemu ya mlolongo wa tuhuma zilizowahi na zinazoendelea kutolewa dhidi ya baadhi ya wabunge wasiokuwa waadilifu, wale walioweka kando maslahi ya umma, badala yake wakajineemesha.

Kwa kujineemesha kwao, wabunge wasiokuwa waadilifu wanalifanya kuwa upenyo wa kupitisha rushwa, ili maslahi binafsi yafikiwe.

Kupitia hoja iliyosababisha kuvunjwa kwa Kamati ya Nishati na Madini, Bunge linapaswa kujipambanua kwa umma, liudhihirishie umma kwamba katika muundo wa kitaasisi, halihusiki na rushwa, isipokuwa kwa Mbunge binafsi.

Uamuzi uliotolewa na Makinda kulipeleka suala hilo kwa Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge, ifungue ukurasa mpya, kwanza kwa kutimiza nia za wabunge waadilifu, kwamba waliowachafua watajwe.

Watajwe kwa majina yao matatu, watajwe kwa uanachama wa vyama vyao vya siasa na watajwe kwa majimbo yao ya uchaguzi.

Wakishatajwa na umma ukawatambua, mamlaka husika ambazo hata hivyo zinaonekana ‘kulala’, zitekeleze wajibu wake.

Kwa maana inakuwaje tuhuma za rushwa ambazo kimsingi zingepaswa kuibuliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ziwasubiri wabunge wenye ‘roho ngumu’ ya kutetea maslahi ya umma, wayasema hayo bungeni?

Tena katika mazingira ambayo tuhuma hizo zimefanyika mjini Dodoma, palipo na taasisi zote zikishiriki kwa karibu katika mkutano wa Bunge la bajeti!

Kwamba maofisa wa usalama wa taifa walishindwa kujua kinachoendelea katika kushamirisha rushwa kwa wabunge!

Kama walijua, walitimiza wajibu wao kupata taarifa waliziwasilisha wapi? Ikawaje?

Maofisa wa Takukuru ambao hivi sasa wanajinasibu kwa kuwa na vitendea kazi vinavyoimarisha mtandao wa kuzuia na kupambana na rushwa, walikuwa wapi? Umma uwaeleweje?

Wakati umefika kwa upepo wa mabadiliko ‘kuisafisha’ nchi, uzembe kama unaonekana kwa baadhi ya wabunge kuchafua hadhi ya Bunge ushughulikiwe kwa haraka na ukali.

Ingawa rushwa ni tatizo mtambuka, kwamba linaweza kutokea kwa watu wa kada zote, lakini inapokuwa kwa wabunge kama ilivyo kwa taasisi nyingine muhimu katika maamuzi, inakuwa balaa!

Kushamiri kwa rushwa katika chombo kinachoisimamia serikali ni pigo kwa nchi, ni fedheha, ni aibu, ni gharama inayokiangamiza kizazi cha Tanzania na taifa kwa ujumla wake.

Tunapaswa tuthubutu katika kukemea, tuweze katika kuwataja wahusika, na tusonge mbele katika kuwachukulia hatua.

Hapo ndipo Tanzania yenye neema itakapowezekana.

Mashaka Mgeta ni Mwandishi wa Habari za Siasa wa NIPASHE. Anapatikana kupitia simu namba +255 754 691540, 0716635612 ama barua pepe; mgeta2000@yahoo.com.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment