Friday May 24, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Mume katimka na hausigeli akaniachia watoto!

8th July 2012
Print
Comments

Mpenzi Msomaji, wiki iliyopita nilizungumzia mahausigeni na kutoa rai kwamba wasichana hawa japokuwa ni muhimu katika nyumba zetu, lakini yafaa kuwa na tahadhari kubwa kwani baadhi yao ni hatari, hivyo wachunguzwe kabla ya ajira.

Wapo ukiwaona kwa mara ya kwanza utafarijika sana kwamba umepata lakini kumbe baada ya kipindi kifupi unapatikana. Utawaona watulivu, wanyenyekevu na lafudhi nzuri kwa maneno watamkayo midomoni kumbe ndani yake ni sumu ya Mamba.

Naam. Wapo baadhi ya wasomaji wa safu hii ambao wametoa maoni yao kuhusiana na mada ile, huku mmoja akieleza kilichomsibu yeye baada ya kumkaribisha msichana wa kuletewa bila kujua kuwa ni mke mwenzie. Ilikuwaje? Anasimulia kupitia ujumbe mfupi wa simu ya kiganjani.

“Anti, nimesoma mada yako kwenye gazeti wiki iliyonipita imenigusa sana kwani nami yalishanikuta. Hawa mahausigeli wa kuletewa ni balaa tupu.

Huwezi kuamini mimi nimenyang’anywa mume na hausigeli hivi hivi natizama kwa macho. Hii mambo ya kuletewa achana nayo kabisa.

Binti huyo aliniongopea mama yake alishakufa hivyo mama wa kambo akawa anamnyanyasa. Eti kwao ni Singida lakini nimekuja kugundua ni Mmbulu kutoka Karatu huko Arusha. Nawashauri wenzangu wasipende kuletewa msichana bila kujua anakotoka.

Mwenzenu nimeachiwa watoto wawili na ni mume wa ndoa. Nasikia ameshamzalisha.(Naomba jina langu lisitajwe)”.

Mpenzi msomaji, nilipomuuliza kama mumewe alisharejea kuona watoto akajibu; “Alihama kabisa na huu ni mwaka wa tano. Kuna siku alikuja kusalimia watoto lakini hakulala kwangu alifikia gesti. Hata matumizi hakuna. Naamini mwisho wa ubaya ni aibu. Mungu yupo nimemuomba wakati wote anitetee, nilishamuomba talaka hakunipa ananipiga kalenda tu”, anamaliza ujumbe wake msomaji huyu.

Mpenzi msomaji, bila shaka umemsikia msomaji wetu ambaye huruma yake ya kukubaliana na binti yule kwamba hana mama na hata yule wa kambo amekuwa akimsulubu, imemgharimu mume.

Mchezo huu wa baadhi ya kinababa kuwageukia mahausigeni upo sana katika familia zetu. Kama hausigeli hakuvunja ndoa, basi anakuwa nyumba ndogo ya baba mwenye nyumba. Baba asiye na haya(aibu) hudiriki kumtafutia nyumba na wengine wamewanunulia viwanja na kuwajengea au kuwanunulia nyumba kabisa. Uroho huu wa baadhi ya wanaume ni tatizo kubwa sana japo wanaokumbana na dhahama hii hugumia rohoni bila kupiga kelele.

Kinamama wengine huamua kuwa wapole wakihofia kupoteza hadhi zao za ndoa na kufikiria jinsi ya kuanza tena maisha endapo wanazihama nyumba zao za ndoa, wanashindwa. Wanavumilia. Hawa nawasifu sana.

Nawasifu kwa sababu, kinababa wengi wanaodanyanywa na penzi la wizi iwe kwa mahausigeli au kwa wanawake wa nje ya ndoa, wengi wamejikuta katika dhiki baada ya ile raha aliyoikimbilia kuchujuka kama nazi iliyokamuliwa tui na kuanza tena kutamani penzi lake la awali.

Wapo waliokimbilia penzi la nje na hamu ilipoisha wakazitamani tena nyumba zao. Baadhi hurudi kwa aibu, wengine hufia huko huko baada ya kuvuruga kabisa boma lake ikiwa ni pamoja na kuhamisha mali ambazo baadaye huyeyuka kama theluji.

Mpenzi msomaji, Kinababa hawa wanaozipiga kisogo ndoa zao, haiwezekani kwamba wanafanya hivyo kwa makusudi au bahati mbaya. Wapo wanaovutwa na tamaa zao za mwili. Lakini wengine kutokana na kutopata kile walichotarajia kutoka kwa wake zao.

Kwa mfano, na hili nilishaliongelea sana katika safu hii. Wakati wawili wanapotafuta mahusiano, yapo mambo mengi wanayoonyeshana kuthibitisha kuwa endapo watafunga pingu za maisha wataishi maisha yaliyo bora kabisa.

Lakini baada ya kuoana, yapo mambo mengine ambayo hayakujitokeza wakati wa mahusiano lakini sasa kila mmoja kati ya wawili hao huanza kuyakunjua. Mfano baba alikuwa mnyawaji kiasi lakini sasa ni mlevi wa kutupwa. Alikuwa anamthamini sana mkewe kwa kumwachia fedha za matumizi nyumbani lakini baada ya familia kuongezeka, watoto anaanza ubahili.

Baba alizoea arudipo kazini mama kama yupo ndiye anayempokea, humpa pole na pia kumwandalia chakula, maji ya kuoga na hata chumbani. Alizoea kuandaliwa nguo za kazini na kadhalika. Lakini kazi hizi, nyingi anazifanya hausigeli.

Sasa baba anapoona mama anakwepa majukumu yake ya msingi ndani ya nyumba na majukumu hayo anayafanya hausigeli, hapa lazima tutegemee tatizo. Baba huyu atavutwa na hisia kwamba huyu binti ndiye anayemjali kuliko mkewe. Sasa akianza kumkonyeza, naye akajibu, nani alaumiwe? Hapa kuna tatizo kubwa. Kina mama wengi wamesahau wajibu wao kwa waume zao, hivyo kutoa mwanya kwa waume hawa kuchepusha hisia na kuanza kuparamia mahausigeli. Au siyo msomaji wangu?

Lakini pia utakuta familia iko vizuri, kipato kizuri, watoto wanasoma lakini baba au mama kuanza kupepesa macho kama siyo humo humo ndani hata nje. Ukiuliza kwanini, eti “nimechoka kula wali maharage, au wali michuzi nataka kula kuku chipsi au pilau biriani. Ebo! Kimbembe huanzia hapo.

Wengine ni hulka tu, uroho wa kimwili, japo wanajua ni kosa au dhambi ya mauti ila wanasema potelea kwa mbali, liwalo na liwe, matokeo yake baba anahama nyumba na kwenda kuanzisha maskani mapya. Hii si bure kipo chanzo.

Kama ni mama, baba awe huru kumweleza hivyo ajirekebishe. Na hii inapaswa kufanyika kabla ya uamuzi kufanyika. Baba ni muhimu aweke wazi udhaifu wa mkewe.

Hata hivyo, kwa wale kinababa wenye viburi vya mali, pesa, niwaambie kwamba kusaliti ndoa iliyokufuta vumbi kwenye kope ni dhambi kubwa. Na dhambi hii itakuandama hadi basi hasa kutokana na kilio cha mkeo na watoto. Ndio maana wengi wanaosaliti ndoa huishia mahali pabaya. Wapo wanaoondoka hata kama ni kwa kuwarubuni mahausigeli lakini huko wanakumbwa na dhoruba wanafukuzwa kama wahalifu hata kama mji huo wameujenga kwa gharama kubwa.

Mpenzi msomaji, nimezungumza vya kutosha kwa leo, pengine nikuachie nawe utoe maoni yako katika jambo hili tuelimishane. Swali kuu likiwa kwanini mume atimue na hausigeli akuachie watoto?

Karibu changia maoni. Na ukiwa tayari, kuwa huru kutuma ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 774268581(usipige), au barua pepe; fwingia@gmail.com

.Kumbuka kama hutapenda jina au simu yako itajwe gazetini tamka hivyo na hilo litaheshimiwa.

Wasalaam.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment