



Wiki iliyopita, Watanzania walishtushwa na taarifa iliyotolewa bungeni na Mbunge wa Mbozi Magharibi, Godfrey Zambi (CCM), kwamba Malawi inadai kuwa Ziwa Nyasa ni mali ya nchi hiyo kwa asilimia 100.
Mbunge huyo alitoa kauli hiyo bungeni baada ya kuomba mwongozo wa Spika na kufafanua kuwa vyombo vya habari vya Malawi na vya Tanzania, vilimkariri mmoja wa makatibu wakuu wa Malawi, akieleza kwamba Ziwa Nyasa lipo nchini mwake kwa asilimia 100.
Zambi alisema hali hiyo inahatarisha uhusiano wa nchi hizo na kuitaka serikali kutoa maelezo juu ya hali ya Ziwa Nyasa ili wananchi wa Mbeya pamoja na wabunge waelewe.
Alisema kumekuwapo na mazungumzo ya muda mrefu kuhusu mpaka wa ziwa hilo lakini wabunge na wananchi kwa ujumla, hawajui kilichofikiwa.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, taarifa za katibu huyo wa Malawi, zimeleta wasiwasi na hofu kubwa miongoni mwa wananchi wa mkoani Mbeya ambao hutumia ziwa hilo kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge kwa siku hiyo, Jenister Mhagama, alisema suala hilo atalipeleka serikalini ili Waziri Mkuu au Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, alitolee ufafanuzi na taarifa kamili.
Hata hivyo, Kaimu Kiongozi wa Shughuli za Serikali bungeni, Samuel Sitta, alisema serikali imestushwa mno na taarifa hizo kwa kuwa mazungumzo kuhusu mpaka wa Ziwa Nyasa yanaendelea.
Alionya kwamba Tanzania ipo tayari kwa uchokozi wowote kwa kuwa inafuata sheria za kimataifa, hivyo akawataka wananchi wa mikoa ya Mbeya, Ruvuma na Iringa, ambayo inapakana na ziwa hilo kuendelea na shughuli zao za kiuchumi ziwani humo.
Jana, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa wa 2012/13, alisema Tanzania itahakikisha inalinda mipaka yake kwa gharama yoyote ile na kuzionya ndege zozote za makampuni yanayofanya utafiti wa mafuta na gesi katika ziwa hilo kuruka kwenye anga la Ziwa Nyasa kuanzia jana.
Membe alisema tatizo lililopo ni kwamba Malawi wanadai kuwa mpaka baina yake na Tanzania unapita pwani ya ziwa hilo; hivyo ziwa lote kutoka kwenye mpaka kati ya Malawi na Msumbiji hadi Kyela, Tanzania ni mali ya nchi hiyo.
Alisema Malawi wanajenga hoja kwa kuangalia mkataba uliowekwa na Waingereza na Wajerumani mwaka 1890 wa Anglo-German Agreeement ulioweka mpaka kati ya Tanzania na Malawi pwani.
Alisema Tanzania kwa upande wake inadai kwamba mpaka unapita katikati ya ziwa kutoka mpaka wa Malawi na Msumbiji usawa wa latitudi nyuzi tisa na 11 hivyo kufanya eneo lote la Kaskazini Mashariki kuwa mali ya Tanzania.
Alisema baada ya kuibuka kwa tofauti hizo, ilikubalika kwamba pande zote zikutane ili kumaliza mgogoro huo kwa njia ya diplomasia.
Itakumbukwa kwamba katika miaka ya 1960, Tanzania iliwahi kuingia mzozo kama huo na Malawi wakati huo ikiongozwa na marehemu Kamuzu Banda.
Hali hiyo ilizorotesha kwa kiasi fulani uhusiano kati ya nchi hizi mbili yaani Tanzania na Malawi kiasi kwamba vijana wa zamani, watakumbuka walikuwa wakiimba nyimbo shuleni wakati wa mchakamchaka za kumkashifu Banda kwa suala hilo.
Moja ya nyimbo hizo ni ule maarufu uliojulikana kama " Banda wa Malawi katuvalia ngozi ya chui kututisha Watanzania...Hatuwezi...hatuwezi...,".
Kwa hakika tunaona zipo dalili kwamba kama mgogoro huu wa mpaka hautashughulikiwa haraka, unaweza tena kuathiri uhusiano kati yetu na Malawi.
Lakini sisi tunadhani kwamba bado mgogoro huu unaweza kutatuliwa kwa njia za diplomasia kama viongozi wa pande zote mbili watakubali kuketi pamoja na kujadili kwa maslahi ya nchi zao na Afrika kwa ujumla wake.
Hata hivyo, tusingependa nchi jirani kutumia uungwana wetu wa Watanzania na kuamua kuchezea mipaka ya nchi yetu kwa namna yoyote ile.
Licha ya kwamba ni dhahiri Malawi inaonekana kukiuka mikataba ya kimataifa na mipaka ya wakoloni inaonyesha kwamba mpaka wa Tanzania na Malawi upo katikati ya Ziwa Nyasa na hivyo asilimia 50 ya ziwa hilo ipo nchini kwetu, bado tungeshauri kuwepo kwa mazungumzo ili suala hili limalizwe kindugu na kidiplomasia.
Kwa hakika, si vema kwa sasa Afrika ya leo kuzungumzia masuala ya mipaka kati ya nchi na nchi badala ya kuzungumzia namna gani Afrika iungane na kuwa taifa moja lenye nguvu kiuchumi.