Thursday Jun 20, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

JK amzungumzia Dk. Ulimboka

2nd July 2012
Print
Comments
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka.

Rais Jakaya Kikwete amesema kuwa anatambua kuwa Serikali inatajwa katika orodha ya wanaotiliwa shaka katika kuhusika na sakata la kutekwa, kuteswa na kujeruhiwa vibaya kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka.

Akihutubia taifa katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi wa Juni jana, alisema ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi haraka kuhusu sakata hilo.

“Mimi nimeshangazwa sana na hisia hizo kwani siioni sababu ya Serikali kufanya hivyo.  Dk. Ulimboka alikuwa mmoja wa kiungo muhimu katika mazungumzo baina ya Serikali na Madkatari.  Ni kweli kwamba yeye si mtumishi wa Serikali, hivyo hakustahili kuwa sehemu ya majadiliano haya.  Kulikuwa na rai ya kutaka asiwepo, lakini nilisema wamuache maadam Madaktari wanamuamini kuwa anaweza kuwasemea vizuri zaidi kuliko wao wenyewe walioajiriwa na Serikali,” alisema.

ONDOA WINGU


Alisema anataka uchunguzi huo ufanyike ili kuondoa wingu baya la kutiliana shaka linakoendelea hivi sasa kwamba serikali imehusika katika tukio hilo.

Dk. Ulimboka, Juni 26 mwaka saa 6:00 usiku alitekwa na watu wasiojulikana waliokuwa na silaha za moto ambao walimpiga na kumjeruhi sehemu mbalimbali za mwili ikiwa ni pamoja na kumng’oa meno na kucha, kisha kumtupa katika msitu wa Mabwepande jijini Dar es Salaam.

Agizo hilo la Rais limekuja siku moja tu baada ya Dk. Ulimboka kusafirishwa na madaktari wenzake kwenda nchini Afrika Kusini kwa matibabu baada ya kukosekana kwa vifaa vya kuweza kumfanyia vipimo hapa nchini kutokana na kujeruhiwa vibaya.

Kadhalika, Rais Kikwete alisema anaungana na Watanzania kuelezea masikitiko makubwa na kuhuzunishwa na kitendo cha kinyama alichofanyiwa Dk. Ulimboka ambacho ni kinyume kabisa cha mila na desturi za Kitanzania.

“Nimeelekeza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina ili ukweli ujulikane,  Nimesema kuwa ningependa ukweli huo ujulikane mapema ili tuondoe wingu baya la kutiliana shaka na kulaumiana kunakoendelea hivi sasa,” alisema Rais Kikwete.

Alisema anatambua kuwa Serikali nayo inatajwa katika orodha ya wanaotiliwa shaka kuhusika na tukio la kupigwa Dk. Ulimboka

MAZUNGUMZO MAZURI

Alisema mazungumzo kati ya serikali na madaktari yalienda vizuri na mafanikio makubwa yamepatikana japo yapo maeneo machache na hasa eneo la mshahara ambalo halikufikiwa makubaliano. 

Aliongeza kuwa mazungumzo yalipofikia walikubaliana na kurudi kwenye mkondo wa Sheria kusaidiwa hivyo kwa hatua hiyo hakuna sababu kwa serikali kumdhuru Dk. Ulimboka wakati tayari Mahakama Kuu imekwishatoa amri ya kusitisha mgomo.
 
Alisema anayekaidi amri ya Mahakama ananunua ugomvi na mhimili huo wa dola ambao wenyewe una mamlaka ya kumtia adabu mtu huyo.

“Hivi baada ya kufika hapo Serikali iwe na ugomvi na Dk. Ulimboka kwa sababu ipi na jambo lipi hata iamue kumdhuru? Kama kuna mtu wa Serikali kafanya, itakuwa kwa sababu zake binafsi na siyo za Serikali au kwa kutumwa na Serikali,” alisema.

SALAMU ZA POLE

Rais Kikweta alisema kwa niaba ya Serikali anatoa mkono wa pole kwa Dk. Ulimboka na kumwombea apone haraka ili aungane na familia yake na Watanzania wenzake katika ujenzi wa Taifa. 

 ULIMBOKA AENDELEA VIZURI

Wakati huo huo, Katibu wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Edwin Chitage, ameiambia NIPASHE kuwa Dk.Ulimboka amewasili salama Afrika Kusini alikopelekwa kwa ajili ya matibabu na ameanza kutibiwa hivyo hali yake inaendelea vizuri.

"Taarifa nilizopata ni kwamba anaendelea vizuri, tunaendelea kufuatilia afya yake kwa ukaribu kabisa," alisema.

Tukio la kutekwa na kuumizwa vibya kwa Dk. Ulimboka limezua taharuki kubwa nchini, huku serikali ikibebeshwa lawama za kuhusika kwake na kadhia hiyo ambayo imezidi kuvuruga mgomo wa madaktari ambao ulianza Juni 23, mwaka huu.

Makundi mbalimbali ya kijamii yametoa wito wa kuundwa kwa tume huru kuchunguza kadhia hii, huku kile kikosi kazi kilichoundwa na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, ikipingwa vikali kwa madai kuwa Polisi ni sehemu ya tatizo na haiwezi kujichunguza yenywe.

Kumekuwa na madai kuwa ofisa mmoja wa polisi alikuwa miongoni mwa watesi watano waliomteka Dk. Ulimboka na kwenda kumtesa kwa kumng’oa meno, kucha na kubanwa sehemu za siri katika msitu wa Mabwepande.

Dk. Ulimboka mbali ya kung’olewa meno, pia amevunjwa mikono yote, mbavu na vipimo vilionyesha kuwa na ubongo wake ulitikisika bila shaka kutokana na kugongwa na kitu kizito kichwani.

 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment