Thursday May 5, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Mwongozo tasnia ya habari wasainiwa

4th May 2012
Print
Comments
Waziri wa Habari,Utamaduni na Michezo, Dk.Emmanuel Nchimbi(katikati), akishuhudia wakati Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini (Moat), Dk. Reginald Mengi (kulia) na Muasisi na Afisa Mtendaji Mkuu wa African Media Initiative (Ami), Amadou Mahtar Ba (kushoto), wakisaini Mwongozo kwa wamiliki na Mameneja wa vyombo vya habari barani Afrika jijini Dar es Salaam jana.

Wamiliki na Mameneja wa vyombo vya habari nchini wamesaini mwongozo na kanuni za uongozi kwa tasnia hiyo kwa lengo la kujenga utamaduni wa kukuza maadili katika ngazi za juu za uongozi wa vyombo hivyo.

Mwongozo huo ulisainiwa jana jijini Dar es Salaam baina ya Mwenyekiti wa Chama Cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini (Moat), Dk. Reginald Mengi na Mkurugenzi Mtendaji wa Mradi wa Mpango wa Vyombo vya Habari Afrika (AMI), Amadou Mahtar Ba, na kushuhudiwa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi.

Akizungumza kabla ya kusainiwa kwa mwongozo huo, Waziri Nchimbi alisifu jitihada zilizofanywa na Moat pamoja na wadau wa tasnia ya habari nchini ya kukubali mpango wa kujitathmini wenyewe kwa kujiwekea kanuni na mwongozo.

Alisema azma ya wamiliki na wahariri wa vyombo vya habari kukubali kuweka mwongozo huo inaonyesha dhamira ya dhati waliyonayo katika kuihudumia jamii kwa weledi na uadilifu na kwamba imedhihirisha kuwa tasnia hiyo inafanya kile ambacho inataka jamii ifanye.

“Tunathamini sana dhamira hii. Waangalizi wa masuala ya kijamii wanaamini kwamba njia hii ya kujitengenezea mwongozo ni nzuri zaidi kuliko miongozo inayotoka nje ya taaluma husika, tambueni ya kwamba serikali inaungana nanyi na itashiriki kikamilifu kutekeleza mpango huu,” alisema.

Aliongeza: “Azma hii inaonyesha kuwa mnatembea kwenye maneno yenu, serikali inaamini ni jambo la busara kuona mmeamua kujitathmini wenyewe kwa hiari yenu.”

Akimkaribisha Waziri Nchimbi, Dk. Mengi alisema kanuni hizo zinalenga kuhakikisha utawala bora, uwajibikaji, uwazi na uaminifu ambapo wamiliki wa vyombo vya habari wanatoa fursa pana zaidi kwa wahariri kutekeleza majukumu yao bila shinikizo zozote.

Alisema kanuni hizo ni muafaka kwa kuwa mara nyingi waandishi wa habari na wahariri wamekuwa na kanuni zinazowaongoza kitaaluma lakini hakukuwa na zinazowagusa wamiliki.

“Wakati watu wanazungumza kuhusu waandishi wa habari, hawawagusi wamiliki mara nyingi inapotokea habari ikakosa weledi anayelaumiwa ni mwandishi...mpango tuliosaini leo utasaidia kuboresha maadili kwa pande zote kuanzia wanataaluma hadi kwa wamiliki,” alisema.

Alisema ni jukumu la wadau wote wa tasnia ya habari wakiwemo wahariri, mameneja, waandishi na wamiliki kushirikiana kikamilifu ili kuhakikisha kanuni hizo zinatekelezwa kwa nia ya kuboresha na kuimarisha taarifa zinazotolewa kwa wananchi.

Mahtar Ba alisema pamoja na kwamba kanuni hizo hazisimamiwi na sheria; zinalenga kuwapa viongozi wa vyombo vya habari mwongozo wa kufanya maamuzi kwa kuzingatia maadili na kanuni zinazosimamia taaluma ya habari.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles