


Hayo ninayokuletea leo hayatokani na mimi bali ni makala ya Prof. Joseph Mbele, Mtanzania anayeishi Northfield, Minnesota, Marekani na kwa mara ya kwanza yalitoka kwenye mtandao wa http://hapakwetu.blogspot.com
Kutokana na umuhimu wakenimeona nikushushie hapa anachosema Prof Mbele, huku nikipunguza baadhi ya mambo machache kulingana na nafasi yangu. Prof Mbele anaandika:
Ni muhimu kuelewa misingi ya mafanikio katika dunia ya leo yenye ushindani mkubwa. Ushindani huu uko ndani ya nchi na kimataifa.
Wapende wasipende, wafanyabiashara na watoa huduma mbalimbali wanajikuta katika mazingira ya mashindano ambayo yanaongezeka kwa kasi na yanazidi kuwa magumu. Katika hali hii, ni muhimu kwa kila mhusika kujua siri za mafanikio.
Siri moja ni ubora wa huduma. Kuna usemi kuwa mteja ni mfalme. Nimeona sehemu mbalimbali duniani ambapo dhana hii inazingatiwa sana. Wako watu wanaofahamu vyema umuhimu wa mteja. Wawe ni wafanyabiashara au watoa huduma, wanaonyesha kumjali sana mteja.
Hata kama mteja ni msumbufu wafanyabiashara na watoa huduma hao wako tayari kumsikiliza, kumvumilia na kumsaidia hadi aridhike.
Nchini Marekani, kwa mfano, mteja anaponunua kitu, anapewa risiti, na kama hataridhika na kitu alichonunua, ana uhuru wa kukirudisha na kurudishiwa pesa zake, au kubadilisha alichonunua akapata kingine, bora alete ile risiti.
Hali hii si ya kawaida Tanzania, ambako risiti mara nyingi huwa imeandikwa kwamba “bidhaa ikishauzwa haiwezi kurudishwa dukani”. Hata kwenye vyombo vya usafiri Tanzania, hali hii ni ya kawaida. Nimeona mara kwa mara tiketi za kusafiria zimeandikwa ujumbe kwamba tikiti ikishakatwa, haiwezi kurudishwa.
Nchini Marekani, nimeona kuwa wahudumu wanawaheshimu wateja. Wanafanya kila juhudi kumsaidia mteja. Kama mhudumu analegea katika kutoa huduma, labda kwa sababu ya kutoelewa, au kazidiwa na shughuli, mkuu wake wa kazi, hata meneja, yuko tayari kuja kutoa hiyo huduma.
Si ajabu nchini Marekani kumwona meneja akitoa huduma ambayo kwa kawaida inatolewa na mfanyakazi wake. Tanzania nimeona mambo tofauti. Meneja wa baa, kwa mfano, hawezi kuchukua kitambaa na kusafisha meza ya wateja. Atamtafuta mhudumu wa baa aje asafishe.
Meneja anajiona mtu bora kuliko wahudumu. Ni kawaida kumwona meneja amekaa kwenye meza na watu anaowajua yeye, na kazi yake ni kunywa pombe na kuongea nao!
Nikiwa kwenye baa za Tanzania, nimewahi kuwa na masuala ya kuwaeleza mameneja, iwe ni malalamiko au ushauri kuhusu huduma, lakini imetokea mara kadhaa kuwa meneja alishalewa, na hana uwezo wa kusikiliza na kuzingatia niliyokuwa nasema. Naamini kuwa, ili tuweze kufanikiwa katika dunia ya ushindani, tabia hizi lazima tuzibadili.
Watu wa nje watakuja na taratibu zao za kujali wateja. Kila mteja anafurahia huduma nzuri. Matokeo yake ni kuwa, wafanyabiashara na watoa huduma wasiozingatia suala la kumridhisha na kumfurahisha mteja watapoteza wateja.
Na katika ulimwengu huu wa ushindani, mtoa huduma nzuri ndiye atapata wateja wengi. Kutakuwa na wafanya biashara ambao wanauza kitu kile kile, kwa mfano nguo za aina ile ile, lakini baadhi watafanikiwa na baadhi watazorota, kutokana na kiwango cha ubora wa huduma kwa mteja. Mteja akiwa na hela yake, anaweza kuipata nguo hiyo kutoka sehemu yoyote.
Lakini anapoamua kuja sehemu moja, wahudumu wa sehemu hiyo wanapaswa kuelewa kuwa hii ni bahati ambayo hawapaswi kuichukulia kijuu juu.
Mteja anapoingia dukani, hotelini, au sehemu yoyote inayotoa huduma, ajisikie kuwa yuko mahali anapothaminiwa na kufurahiwa. Wako wahudumu ambao wanampokea mteja kama vile angekuwa mtu asiyetakiwa, adui, au mhujumu.
Wanampa maneno ya mkato, kuudhi, au kukatisha tamaa. Watoa huduma wa aina hii, au wenye biashara wa aina hii, wanahujumu wenyewe hizo biashara au huduma zao.
Fundisho hili, ingawa rahisi, halijaingia vichwani mwa wengi katika Tanzania. Wengi wanapoona biashara zao zinazorota au huduma zao hazivutii wateja, wanatafuta visingizio kama vile kulogwa na washindani.
Wengi wanaamini kuwa ili wafanikiwe katika biashara, lazima watumie mizizi na mambo ya kishirikina. Nchini Marekani, kuna vitabu vingi ambavyo vinafundisha masuala ya aina aina, likiwemo suala la kuendesha biashara na huduma mbali mbali.
Vitabu hivi vinafundisha mbinu, misingi na mikakati. Vinaelezea saikilojia ya wateja, umuhimu wa kuwajibika, kujenga mahusiano na wengine, na kadhalika. Sijawahi kuona kitabu hata kimoja kinachoelezea umuhimu wa kutumia mizizi. Swali linalonijia kichwani ni je, katika ushindani wa kimataifa, ambamo wenzetu wanatumia ujuzi, maarifa na elimu, sisi tutafanikiwa kwa kutumia mizizi?
Dunia ya leo inaendeshwa na ujuzi na maarifa. Hilo linafahamika sana duniani. Tanzania bado tuko nyuma. Suala la kutafuta ujuzi, elimu, na maarifa tumelipuuzia.
Hatutaweza kufanikiwa katika dunia ya leo iwapo tutaendekeza hali hii. Ushindani wa kimataifa utakuwa ni tishio kwetu. Wakati huu, tayari, uwoga wa ushindani wa kimataifa umeshaanza kujitokeza nchini mwetu tunapozidi kujiimarisha na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hayo ni matokeo ya kupuuzia suala la elimu, suala ambalo Mwalimu Nyerere alilizingatia tangu tulipopata uhuru, pale aliposema kuwa tuna maadui watatu: ujinga, umaskini, na maradhi.
Kwa upande wa huduma serekalini na taasisi zake kama vile mahakama na polisi ni kama hakuna huduma maana mara nyingi bila kutoa rushwa hakuna huduma utakayopata. Hili ni tatizo kubwa Tanzania.