



Wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya ya Kombe la Shirikisho, Simba, wanatarajia kucheza mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo itakayochezwa Aprili 22 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mfadhili wa zamani wa Simba, Azim Dewji, alisema kuwa mpango wa kuileta TP Mazembe ni kutaka kuimarisha kikosi cha ‘Wanamsimbazi’ kinachoshiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho.
Mwishoni mwa wiki, Simba ilitinga raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho kwa kuitoa ES Setif ya Algeria na sasa itashuka tena dimbani Aprili 29 kucheza nyumbani dhidi ya Al Ahly Shandy ya Sudan.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Dewji alisema kuwa ataileta TP Mazembe kwa ajili ya kuipa makali Simba kabla wawakilishi hao pekee wa Tanzania katika michuano ya kimataifa hawajakutana na wapinzani wao kutoka Sudan.
Dewji aliyeifadhili Simba kwa miaka mingi, alisema kuwa ziara hiyo itaandaliwa na kampuni yake ya Simba Trailers na kwamba hadi sasa, tayari ameshazungumza na kuafikiana na rais wa TP Mazembe, Moise Katumbi Chapwe na pia uongozi wa Simba.
“Pamoja na kuwazawadia fedha, nimeona nitoe mchango zaidi kwa kuwaletea mechi ya kujipima nguvu na timu bora ya Mazembe ya Kongo,” alisema Dewji ambaye hivi karibuni alitoa Sh. milioni 15 kwa Simba baada ya kuitoa Setif.
Aliongeza kuwa, Mazembe itakuwa kipimo sahihi kwa Simba kutokana na kuwa na kikosi chenye wachezaji wenye hadhi ya juu, wakiwemo mwanasoka bora wa zamani kwa wachezaji wa ligi za ndani Afrika, Tresor Mputu, mfungaji wa penati iliyoipa Zambia ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika, Stophila Sunzu na washambuliaji nyota kutoka Tanzania, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.
Mazembe waliotwaa ubingwa wa Afrika mara nne, ikiwa ni pamoja na mara mbili mfululizo katika miaka ya 2009 na 2010, inajivunia pia utajiri mkubwa wa fedha na pia vipaji vingine kama Muteba Kidiaba, mfungaji bora wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa ligi za ndani, Given Singuluma, Rainford Kalaba na mchezaji wa zamani wa Simba, Mganda Patrick Ochan.
Simba imesonga mbele kwa faida ya goli la ugenini baada ya kutoka sare ya 3-3 na Setif kutokana na ushindi wa nyumbani wa 2-0 na kipigo cha ugenini cha mabao 3-1. Mazembe pia wataitumia mechi yao dhidi ya Simba kuimarisha kikosi chao baada ya kutinga raundi ya pili ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika kwa kupata ushindi wa jumla wa mabao 7-1 dhidi ya Power Dynamos ya Zambia.