



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Terezya Huvisa, juzi alidai amekuwa akipokea vitisho vya kuuawa kutoka kwa watu wasiofahamika.
Waziri Huvisa, alitoa madai hayo mbele ya waandishi wa habari mjini Dodoma ambapo alisema vitisho hivyo vinatokana na hatua yake ya kuagiza nyumba zilizojengwa kwenye ufukwe wa bahari kinyume cha sheria zivunjwe.
Lengo la vitisho hivyo ni kufifisha mpango wa bomoa bomoa ya nyumba zilizojengwa kinyume na Sheria ya Mazingira.
Kwa mujibu wa Dk. Huvisa, alipata vitisho hivyo baada ya kutangaza kupitia bungeni kuhusu bomoa bomoa, mtu asiyejulikana alimpigia simu na kumtishia kumuua kama utekelezaji wa mpango huo utafanyika.
Alisema mtu huyo alimpigia simu na kumweleza kuwa: "Wewe unajifanya kuwa kinara wa kutaka kubomoa nyumba zetu, elewa kuwa ukifanikisha nia hiyo tunakuua.”
Vitisho hivyo vimetolewa ikiwa ni siku chache tu tangu ofisi ya waziri huyo kwa kushirikiana na Wizara za Maliasili na Utalii na ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kubomoa nyumba 17 na kuta nane za uzio zilizojengwa kwenye maeneo ya fukwe za Mbezi na Kawe jijini Dar es Salaam.
Waziri Huvisa alisema tayari amekwisha kutoa taarifa za vitisho hivyo polisi ingawa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema hajapata taarifa hizo.
Mbali ya Waziri Huvisa, pia alidai kuwa Mwanasheria wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc), ambaye hakumtaja jina, alipewa vitisho kama hivyo kwa njia ya simu.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, vitisho hivyo pia viliripotiwa polisi na kwa Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal.
Huyu si waziri wa kwanza kutoa madai ya kutishiwa kuuawa katika kipindi cha kati ya mwaka jana na mwaka huu.
Awali, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, alitishiwa kuuawa ambapo baada ya vitisho hivyo, Februari 8, mwaka jana, alikwenda Polisi kuzungumza na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema.
IGP Mwema, alimtaka Dk. Mwakyembe, kuweka kwenye maandishi madai hayo ambapo naye alifanya hivyo na kuwasilisha kwa maandishi siku iliyofuata.
Hata hivyo, hakuna mtu aliyekamatwa kutokana na taarifa hizo.
Mbali ya Dk. Mwakyembe, mwingine ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
Profesa Tibaijuka aliwahi kutishiwa kuuawa baada ya kuendesha zoezi la ubomoaji wa nyumba zilizojengwa kwenye maeneo ya wazi jijini Dar es Salaam.
Tukiangalia vitisho walivyopewa Mawaziri Dk. Huvisa na Profesa Tibaijuka, kiini chake ni baadhi ya watu kuamua kujenga nyumba zao katika maeneo yasiyoruhusiwa kisheria kama vile kwenye viwanja vya wazi, fukwe na hifadhi za barabara.
Hata hivyo, ukichunguza kwa makini, wengi wa watu hao hujenga nyumba hizo baada ya kupewa vibali na maofisa ardhi wasio waaminifu ambao bila shaka ni baada ya kupata kitu `kidogo'.
Kwa hili, ni wajibu wa serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria maafisa ardhi wanaochangia ujenzi katika maeneo yasiyoruhusiwa, kwani ndiyo wanaowapotosha wananchi.
Aidha, wizara husika iendeleze kwa kasi utaratibu wa kupima maeneo na kuyagawa kwa wananchi kwa gharama ndogo. Hii itapunguza uvamizi holela wa maeneo yasiyoruhusiwa kujenga.
Lakini pia inashangaza kuona kwamba mtu anaanza kujenga tangu msingi mpaka anakamilisha nyumba yake eneo lisiloruhusiwa bila hata maafisa ardhi kumsimamisha na badala yake husubiri amalize na kubomoa.
Inapofikia mtu kuvunjiwa nyumba yake aliyoigharimia fedha nyingi, lazima atakasirishwa na matokeo yake ni kutoa vitisho kwa mawaziri wanaosimamia zoezi hilo.
Tunaamini kwamba hao wamekuwa wakifanya kazi zao kwa mujibu wa sheria lakini huponzwa na watu wachache wenye tamaa ambao hugawa vibali vya ujenzi kwa misingi ya rushwa.
Tunasema mawaziri hawa waachwe wafanye kazi yao na wale wanaowatishia kifo, waache kabisa tabia hiyo.
Hatutakuwa tumekosea kuwafananisha watu wa namna hiyo na wahalifu wakubwa kwani wanavunja sheria za nchi halafu wakichukuliwa hatua, wanawatishia wale wanaosimamia sheria.
Hata hivyo, tungeiomba serikali kutopuuzia madai ya mawaziri hao na kama ikibidi, basi wapewe ulinzi wa ziada ili watekeleze majukumu yao ipasavyo na bila woga.