Monday May 2, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Mwanamke atiwa mbaroni akidaiwa kumuua mpenziwe

26th April 2012
Print
Comments

Polisi mkoani hapa, wanamshikilia Sabina Shirima (29), kwa tuhuma za kumchoma kwa kitu chenye ncha kali hadi kufa mwanamume anayedaiwa kuwa ni mpenzi wake.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Thobias Andengenye, alisema jana kuwa chanzo cha tukio hilo ni ugomvi uliozuka kati yao.

Alimtaja aliyeuawa kuwa ni Abiud Lema, anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 60 na 65 na kwamba tukio hilo lilitokea juzi saa 5:00 usiku eneo la Sanawari jijini hapa nyumbani kwa mtuhumiwa huyo.

Kamanda Andengenye alisema polisi bado wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo, ingawa habari za awali zimeonyesha kuwa marehemu alichomwa na kisu upande wa kushoto wa mguu wake, hali ambayo ilimfanya atokwe na damu nyingi.

Alisema polisi aliyekwenda kwenye eneo la tukio, alikuta damu ya marehemu ikiwa imetapakaa chumba kizima.

“Bado tunachunguza tukio hilo na hatuwezi kutoa maelezo ya jumla tu kwamba kifo hicho kimetokana na kupoteza damu nyingi. Daktari aliyefanya uchunguzi wa maiti bado hajatoa taarifa yake,” alisema.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha maiti cha Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru.

Dada wa marehemu, Aluya Swai, alisema kaka yake alikuwa akifanya kazi kama dereva wa basi linalofanya safari zake kutoka Arusha hadi Moshi.

“Hatujui nini kilimtokea, kwa sababu ugomvi ulitokea kati ya wawili. Tunasubiri uchunguzi wa polisi watueleze kuhusu mauaji hayo,” alisema huku akilia.

Alisema marehemu alichomwa ndani ya nyumba iliyopo jirani na nyumba yake, na mtuhumiwa alitoa taarifa kwa uongozi wa serikali za mitaa, ambao waliuchukua mwili wa marehemu hadi hospitalini.

Mtoto mmoja wa marehemu, Anandumi alisema: "Sababu za kifo cha baba bado haijulikani na kwa maana hiyo hado haijamwingia akilini kama mwanamke huyo ndiye alimuua. Niliingia ndani ya nyumba na kuona damu sakafuni. Kitanda chake na mlango hakuna damu yoyote iliyoonekana.”

Aliongeza: "Mtuhumiwa huyo ni mgeni machoni kwangu na nasubiri ripoti ya polisi."

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles