Saturday May 7, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Samata kuikosa Malawi

17th May 2012
Print
Comments
Mshambuliaji wa timu ya soka ya Tanzania (Taifa Stars), Mbwana Samata

Washambuliaji wa timu ya soka ya Tanzania (Taifa Stars), Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu ambao wanaichezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wataikosa mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Malawi itakayofanyika Mei 26 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, imefahamika.

Samata na Ulimwengu wanatarajia kuwepo katika mechi ya kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Ivory Coast itakayofanyika Juni 2 jijini Abdijan.

Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema jana kuwa TP Mazembe imetoa ruhusa kwa nyota hao kwa kufuata kanuni za FIFA.

"Samata atawasili nchini Mei 27, hiyo ndio taarifa tuliyopata," alisema Wambura.

Wakati huo huo, jana asubuhi kocha mpya wa Stars, Kim Poulsen, alisema kuwa atabadili mfumo wa mawasiliano ambao hufanyika katika kuwaita wachezaji walioteuliwa kwenye kikosi hicho ambapo sasa watawasiliana nao moja kwa moja badala ya kupitia katika klabu zao hasa kwa wanaocheza hapa nchini.

Hatua hiyo ya Kim imefuatia changamoto aliyokutana nayo jana asubuhi alipoanza kibarua cha kuifundisha timu hiyo kwa kuwa na wachezaji 11 tu mazoezini badala ya 23 aliowatarajia.

Wachezaji ambao walifanya mazoezi ya kwanza chini ya Kim ni kipa mmoja, Juma Kaseja, ambaye alikuwa chini ya Juma Pondamali na wengine ni John Bocco, Shomary Kapombe, Mwinyi Kazimoto, Amir Maftah, Simon Msuva, Frank Domayo, Ramadhani Singano 'Messi', Jonas Mkude, Edward Christopher na Salum Aboubakar.

Kipa Deogratius Munishi kutoka Mtibwa Sugar ambaye ameshasajiliwa na Azam yeye aliwasili kwenye uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam jana saa 3:05 akiwa ameshachelewa na hivyo alishindwa kuwahi mazoezi ya kocha huyo mpya.

Baada ya kumaliza mazoezi hayo ya kwanza, Kim alisema kuwa ameelezwa kuwa wachezaji wameshindwa kuwahi kutokana na kuwa nje ya Dar es Salaam baada ya Ligi Kuu ya Bara kumalizika na wengine klabu zao zimechelewa kuwajulisha kuwa wanatakiwa kuripoti kambini.

Wachezaji ambao hadi jana jioni walishindwa kuripoti katika kambi ya timu hizo ni Erasto Nyoni na Shabani Nditi huku kiungo, Haruna Moshi 'Boban' akihudhuria mazoezi ya jioni pamoja na wachezaji wenzake.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles