Sunday May 1, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Angalizo latolewa vitambulisho vya taifa

26th April 2012
Print
Comments
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro

Kazi ya utoaji wa vitambulisho vya taifa inaweza kuwa ngumu kama jamii haitatoa ushirikiano wa kuwatambua watu ambao sio raia wa Tanzania wanaoishi nchini kinyume cha sheria hasa katika maeneo yaliyo mipakani.

Angalizo hilo lilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, wakati akifungua semina ya wadau wa masuala ya wakimbizi na wahamiaji haramu, iliyolenga kuwajenga uwezo wa kuzielewa sheria za kitaifa na kimataifa zinazohusiana na wakimbizi na wahamiaji haramu.

Semina hiyo iliyoandaliwa na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) tawi la Mpanda kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani, iliwashirikisha maofisa wa Idara za Uhamiaji, Polisi, Usalama wa Taifa na waandishi wa habari. “Taifa liko kwenye mchakato wa kuanza utoaji wa vitambulisho vya uraia, kazi hii itakuwa ngumu sana kama hatutakuwa waangalifu,” alisema Kandoro.

Kandoro alisema kuwa kuna raia wa nchi jirani ambao wamejipenyeza nchini na kujifanya raia wa Tanzania, huku baadhi yao wakiwa wamefanikiwa hata kupata uongozi katika ngazi za vijiji na kata. Alisema baadhi ya raia hao wa kigeni walikuwa ni wakimbizi kutoka nchi jirani, ambao baada ya kurejeshwa kwenye nchi zao wamerudi tena nchini na kujifanya ni raia.

“Wananchi tunaoishi maeneo ya mipakani na jirani na makambi ya wakimbizi tuwe wepesi wa kuwatambua na kuwaripoti wanaotoka kwenye makambi na kuja uraiani kujifanya ni Watanzania,” alisema Kandoro.

Kwa upande wake, Ofisa wa UNHCR, Godlove Kifikilo, alisema lengo kubwa la semina hiyo ni kuwawezesha wadau wa masuala ya wakimbizi kumtambua mtu anayestahili kupewa hadhi ya ukimbizi, anayeomba hifadhi na muhamiaji haramu.

Alisema kumekuwepo na mkanganyiko juu ya kuwatambua wahamiaji haramu na wakimbizi, hali ambayo imekuwa ama ikisababisha kuwepo kwa wakimbizi wasiostahili hadhi hiyo au baadhi kunyimwa hadhi hiyo ambayo wanastahili.

Naye Kaimu Mkuu wa Idara ya Uhamiaji Mkoani Mbeya, Remigius Pesambili, alisema taifa linakabiliwa na tatizo kubwa la wahamiaji haramu kutoka nchi za Somalia na Ethiopia wanaopita nchini kwenda Afrika Kusini.

Alisema mwaka jana pekee, Idara ya Uhamiaji Mkoani Mbeya iliwakamata wahamiaji haramu zaidi ya 700 na kuwafikisha mahakamani na kuwa hadi sasa wahamiaji haramu zaidi ya 150 wamefungwa gerezani mkoani humo.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles