


Leo Watanzania wenzetu katika jimbo la Arumeru Mashariki wanapiga kura kumchagua mbunge watakayempa jukumu la kuwawakilisha bungeni kwa kipindi cha miaka mitatu, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Uchaguzi wa Arumeru Mashariki unafanyika ili kujaza nafasi ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, marehemu Jeremia Sumari aliyefariki dunia miezi mitatu iliyopita, baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Sambamba na uchaguzi huo, pia kuna chaguzi nyingine ndogo za madiwani katika kata takribani nane nchini, ambako pia madiwani wake waliondoka madarakani kwa sababu mbalimbali vikiwemo vifo.
Kama ilivyo kwa chaguzi nyingine zote zinazofanyika nchini, uchaguzi wa Arumeru na Mashariki na nyingine zinazofanyika katika ngazi ya kata, zilitanguliwa na kipindi cha kampeni ambacho hutolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili kuwapa fursa wagombea pamoja na vyama vyao kunadi sera na kuwaomba kura.
Kipindi cha kampeni, wagombea pamoja na vyama vyao wanapaswa kukitumia vema kwa ajili ya kuwashawishi wapigakura kuwaamini, wawakubali na hatimaye kuwapa dhamana ya kuwa wawakilishi wao bungeni kwa kuwapigia kura nyingi.
Faida nyingine ya uwepo wa kipindi cha kampeni ni kutoa na kueneza elimu ya uraia kwa wananchi ambao hawakubahatika kuipata, ili waweze kujua haki na wajibu wao katika utekelezaji wa demokrasia huru na ya haki.
Hata hivyo katika hali ya kusikitisha mwenendo wa kampeni katika chaguzi mbalimbali nchini umeanza kupoteza muelekeo kwa kugeuzwa kuwa vijiwe vya rushwa, mipasho, matusi, fujo, kudhalilishana majukwaani na mengine mengi yasiyokuwa na staha kwa jamii.
Jambo la kusikitisha ni kwamba mambo mengi yanayoendelea katika kipindi cha kampeni ni yale yasiyoendana na utamaduni wa Watanzania ambao siku zote wamezoea kuishi kwa amani, upendo, undugu na mshikamano.
Mbaya zaidi ni pale viongozi wa ngazi za juu serikalini, tena wanaoheshimika sana kwenye jamii kama vile mawaziri na marais wastaafu, wanapokuwa waasisi na vinara wa kampeni chafu za kupakana matope huku wakitanguliza matusi, kejeli, vijembe na propaganda zisizokuwa na mashiko.
Mambo hayo hayakuanza leo katika kampeni za uchaguzi wa Arumeru Mashariki au kwenye kampeni za udiwani zilizomalizika jana katika kata mbalimbali nchini, bali yamekuwa yakijitokeza katika takribani kampeni zote za chaguzi za hivi karibuni tangu taifa lilipokubali kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi.
Kwa uchache naweza kutaja baadhi ya chaguzi ndogo zilizotokea katika majimbo ya Tarime, Busanda, Biharamulo, Igunga na sasa Arumeru Mashariki ambako vitendo hivyo vimeripotiwa kwa kiwango cha juu.
Inasikitisha kuona kwamba licha ya kuwepo kwa vitendo visivyoendana na maadili ya uchaguzi na vile ambavyo ni kinyume cha sheria za nchi kujitokeza mara kwa mara katika chaguzi zetu, bado Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imelala usingizi na haijawahi kuchukua hatua za kukomesha hali hiyo.
Natambua uwepo wa sheria na kanuni mbalimbali zilitungwa mahususi kwa ajili ya kusimamia uchaguzi ili uwe huru na wa haki lakini naweza kusema kuwa Nec wamekuwa sehemu ya tatizo la utekelezaji wa sheria hizo.
Nasema hivyo kwa sababu ni kawaida kwa Nec kutangaza kanuni na sheria hizo katika kila uchaguzi kwa ajili ya kuvionya vyama vya siasa na wagombea, kutojihusisha na vitendo vinavyokwenda kinyume na maadili ya uchaguzi, lakini mara zote suala la usimamizi na utekelezaji wa sheria hizo huwa ni hasi.
Kwa wale tunaofuatilia utendaji wa Nec tunaelewa ni wapi ambapo tume hiyo huwa inakwama na kushindwa kukomesha vitendo vya ukiukwaji wa sheria katika chaguzi zetu.
Nec imekuwa ikikosa meno ya kukomesha vurugu na utovu wa nidhamu ya wagombea na vyama vyao kwenye chaguzi zetu.
Lakini naamini kwamba ikitokea siku moja Nec ikaweka kando aibu kwa wagombea na ikakunjua makucha kwa kuwaadhibu ipasavyo, ikibidi kumuengua mmoja wao hata kama atakuwa wa kupitia CCM, itakuwa mfano mzuri na vyama vingine vitafyata mkia na kufuata sheria na kanuni za uchaguzi.
Lakini kwa sasa jinsi hali ilivyo kwenye chaguzi zetu, ninaamini kuwa Nec imefikia ukomo wa kufikiri mbinu za kuendesha kampeni za kistaarabu na imeamua kunyamaza ili kila chama na wagombea wafanye wanavyotaka!
Athari zake ndizo tunazoziona hivi sasa za watu kutishiana kupigwa risasi za bastola kama ilivyotokea wiki hii pale Kiwira wilayani Rungwe, DC kupigwa na kudhalilishwa kama ilivyotokea pale Igunga, wagombea wa kiume kuchorwa wakiwa wamevishwa heleni kama ilivyotokea Arumeru Mashariki.
Sitaki kuamini kuwa sheria zilizopo hazijitoshelezi kukomesha vitendo vya aina hiyo kwenye kampeni, isipokuwa naamini tatizo lipo Nec. Haing’ati!
Mungu Ibariki NEC!
Mungu Ibariki Tanzania!
**************
Emmanuel Lengwa ni Mwandishi wa Habari Mwakilishi wa Nipashe mkoani Mbeya. Anapatikana kupitia barua pepe: emmanuellengwa@yahoo.com.
Simu: 0713 993 498.