Sunday May 1, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

TBS yapiga marufuku petroli kuchanganywa na ethanol

1st May 2012
Print
Comments
Shirika la Viwango Tanzania (TBS)

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limepiga marufuku uchanganyaji wa mafuta ya petroli na ethanol

 

 

Kwa mujibu wa tangazo la TBS kwenye vyombo vya habari mwishoni mwa wiki, ni marufuku uchanganyaji wa aina yoyote katika mafuta ya petroli yanayoingizwa nchini.

 

 

Kwa mujibu wa TBS, uchanganyaji wa ethanol/vinywaji vikali haukubaliki kwa mujibu wa sheria za nchi.

 

 

"TBS inapenda kuwafahamisha waagizaji wote wa mafuta kuwa viwango vya mafuta bora kwa Tanzania haviruhusu kuchanganya petroli na ethanol/vinywaji vikali. Shehena itakayopatikana ikiwa imechanganywa na ethanol haitaruhusiwa kuingia Tanzania," lilifafanua tangazo hilo.

 

 

Hatua hiyo imetangazwa huku kukiwa na mvutano mkali kati ya wafanyabiashara ya mafuta na mamalaka inayosimamia uagizaji wa mafuta kwa pamoja kwa madai kuwa shehena ya mafuta ya Januari - Machi, mwaka huu ilikuwa imechakachuliwa kwa kuchanganywa na ethanol, hivyo kusababisha mafuta hayo kukataliwa katika baadhi ya nchi.

 

Kutokana na mvutano huo, sampuli ya mafuta ilipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (Ewura) na TBS ili kupata ufumbuzi wa tatizo hilo.

 

Kana kwamba haitoshi, kampuni za uagizaji ziliamua kupeleka nje sampuli ya mafuta hayo.

Shehena iliyopelekwa nje kwa ajili ya kupimwa ni ile iliyoagizwa kuanzia Januari hadi Machi, mwaka huu, chini ya Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja.

Katika kipindi hicho, baadhi ya kampuni zililalamika kuwa shehena ya mafuta hayo yaliyoagizwa na Kampuni ya Augusta Energy ya Uswisi imechakachuliwa kwa kuchanganywa na ethanol.

Kwa mujibu wa baadhi ya wafanyabiashara wa mafuta nchini, lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha kunakuwa na matokeo sahihi na ambayo yatasaidia katika kuweka ubora wa mafuta nchini ili kuwanufaisha wao na watumiaji wengine.

Hivi karibuni, shehena ya mafuta ya baadhi ya kampuni za hapa nchini ilikataliwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Burundi na Rwanda kwa kudaiwa kuchakachuliwa.

Kampuni ambazo mafuta yake yamekataliwa ni Gapco, Engen, Mogas, Tipper, Natoil, Hass, Kobil, OilCom na Puma Energy (zamani BP).

Mapema mwezi huu, kampuni hizo ziliandika barua kwenda Ewura na nakala kutumwa kwa Wizara ya Nishati na Madini, Kampuni ya Augusta Energy, Kamati ya Kuratibu Uagizaji Mafuta kwa Pamoja na wanachama wa Taomac.

Kampuni ya Augusta ilishinda zabuni ya kuingiza mafuta nchini tangu Januari, mwaka huu.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles