


Idadi ya watu wanaoshikiliwa kwa tuhuma za kuanzisha vurugu kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) imefikia 13 na chanzo cha vurugu hizo kimedaiwa kuwa ni watu wa kuja waliongia wilayani hapa na kutumia nguvu kuchimba mgodi huo.
Hatua ya kukamatwa kwa watu hao inafuatia mmoja kati ya watu wanaoshikiliwa na polisi juzi mbele ya waandishi wa habari katika kituo cha polisi cha wilaya kufichua kuwa yeye alikuwa anatoka nje ya mikoa wa Mwanza na Geita na amekuwa anatumia jina la uongo la Athuman wakati jina lake halisi ni Paul Anatory.
Kijana huyo aliyedai kuwa na umri wa miaka 23 alisema alikamatwa akiwa ndani ya mgodi huo na polisi baada ya kushawishiwa na watu wengine aliodai wengi wao siyo wakazi wa wilayani Geita kwenda kuvamia mgodi huo kwa lengo la kuiba mawe yenye dhahabu kwa nguvu lakini bahati mbaya yeye akawa miongoni mwa walionaswa na polisi katika vurugu hizo.
Mtuhumiwa huyo ambaye jeshi la polisi lilimhudumia maji ya kunywa na juisi alifichua baadaye kuwa tatizo halikuwa kujeruhiwa kama yeye na wenzake walivyokuwa wanadai isipokuwa kilichokuwa kinamsumbua ni njaa na alikuwa ameamua kusema ukweli kutokana na urafiki waliouonyesha polisi akiwa kituoni ikiwa ni kumpa uhuru na msaada na kuapa kama ataachiwa huru asingeweza kurubuniwa tena.
Hatua hii imekuja baada ya jeshi la polisi wilayani hapa kudai kuwa wengi wa wanaohamasisha kufanya uvamizi huo hawakuwa wakazi wa Wilaya ya Geita hoja inayoungwa mkono pia na wananchi wengi wakazi wa hapa kuwa hatua hiyo inalenga kuharibu mahusiano mazuri yaliyoanza jengeka kati ya mgodi huo siku za karibuni.
Katika mahojiano yake jana Mkuu wa Wilaya ya Geita, Filleom Sheluetete, alisema kuwa serikali ya wilaya tayari inazo taarifa rasmi kuwa wanaohamasisha kufanyika uvamizi na vurugu hizo wengi wanaotoka nje ya Wilaya na Mkoa wa Geita na kuwa mikakati kabambe inafanyika kuhakikisha inawadhibiti waliohusika.
Juzi mapamabano makali yalitokea na kudumu zaidi ya saa tano na kusababisha mtafaruku mkubwa katika mji wa Geita kati ya polisi na watu zaidi ya 200 zilizomalizika kwa magari manne ya mgodi kuvunjwa vioo kwa kupigwa mawe huku moja kati ya hayo likichomwa moto na kuteketea huku walinzi wa mgodi wakiwajeruhi watu wawili kwa risasi ili kujihami kabla hali ya utulivu na amani kurejea baada ya saa tano za mapambano.
Sakata hilo lilianza saa 1.45 asubuhi juzi baada ya watu zaidi ya 100 kuingia ndani ya mgodi huo kwa kupitia njia za uchochoro na kuwashambulia walinzi wanne ambapo wawili wamejeruhiwa vibaya kabla ya polisi kuitwa kutoa msaada na katika kukabiliana nao walinzi hao katika kujilinda waliwajeruhi watu wawili kwa kuwapiga risasi miguuni.