Sunday May 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

`Wabunge EALA wasiende kujaza nafasi`

8th April 2012
Print
Comments
Profesa Samuel Wangwe

Wabunge watakaochaguliwa kuiwakilisha Tanzania kwenye Bunge la Afrika Mashariki (EALA), wametakiwa kuwa na uelewa mpana wa masuala ya mtangamano wa jumuiya hiyo na siyo kuchaguliwa kujaza nafasi zilizopo.

Hayo yameelezwa na wanataaluma na wadau washiriki wa mchakato wa masuala ya mtangamano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Samuel Wange, Mkurugenzi Mtendaji wa asasi ya utafiti wa masuala ya kupunguza umaskini ya REPOA.

Kwa upande wake, Profesa Wange alisema jumuiya hiyo inaingia katika awamu ngumu ya kutekeleza mchakato wa kuunda soko la pamoja hivyo taifa linategemea kuona wabunge wanaokijua na kukileta kile ambacho Tanzania inataka na inakitegemea kwenye ushirikiano wa soko.

Aliwakumbusha pia kuwa baada ya Soko la Pamoja unafuata mtangamano wa sarafu ya pamoja na wakumbuke kuwa makini kwenye mijadala na hatma zake kwa kuangalia maslahi ya taifa kwanza.

Profesa Wangwe aliwakumbusha wabunge kuacha masuala ya ukanda na vigezo vingine vinavyoibuliwa kwenye uteuzi ama uchaguzi na kuwaeleza kuwa wanaochaguliwa ni Watanzania wanaowakilisha taifa na si wajumbe wa kanda wala kundi fulani.

“Watakaochaguliwa EALA wapimwe uwezo na uelewa wao kwanza. ”

Alisema kama kutakuwa na kupeleka washikaji ama ndugu za wanasiasa nao wawe na uelewa wa masuala ya mtangamano na waweze kuibua na kutetea maslahi ya taifa.

Kwa upande wake, Profesa Kabudi alisema wabunge watakaochaguliwa wiki ijayo wawe wanajua kuwa nchi zote tano zina maslahi yao na kwa Tanzania wawakilishi ni lazima wayaelewe ili kulinda mahitaji ya wanaowatuma.

Alisema wabunge watakaochaguliwa wafahamu kwa dhati juu ya mkataba wa utangamano na vipengele vyake pia wayalinde na kuyatetea maslahi ya taifa ukiwemo ulinzi wa rasilimali za nchi, kudumisha umoja na amani ya Watanzania na kulinda amani katika ukanda. “Wabunge hao waelewe mkataba wa mtangamano na vipengele vyake vya kuundwa kwa soko la pamoja, umoja wa forodha, sarafu ya pamoja na kuundwa kwa shirikisho la Afrika Mashariki.”

Aliwataka wazijue hatua hizo na kuhakikisha kuwa zinatekelezwa kwa maelekezo ya mkataba na siyo kuruka nyingine na kukimbilia hatua ya mwisho. Alionya kuwa iwapo watabadilisha taratibu za mkataba watakuwa na jumuiya dhaifu yenye uchumi, soko, forodha na shirikisho duni lisilo na misingi imara iliyokusudiwa.

“Wabunge hawa washirikiane na Serikali, Bunge, sekta binafsi, asasi za kiraia lakini pia wajifunze sana kuwasikiliza Watanzania,” alisisitiza Profesa Kabudi.

Akitoa maoni yake Dk. Magdalena Ngaiza wa Taasisi ya Taaluma ya Maendeleo (IDS) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alipendekeza kuwa na vigezo vya uwakilisha EALA.

Alisema taifa linahitaji kuwa na vigezo ili kuwapima na kuwachuja wagombea wa ubunge wa Afrika Mashariki kwa ajili ya kuwapata washindani halisi.

Alishauri ndani ya vigezo hivyo pawepo na nafasi ya vyama vikubwa vya siasa kutoa wagombea watakaoshindana kwa pamoja na hatimaye kuwapata wabunge wenye uwezo, uzoefu na uelewa wanaoweza kutetea maslahi ya nchi.

Dk Ngaiza Mhadhiri wa masuala ya taaluma za maendeleo alisema inashangaza kuona baadhi ya watu wenye uzoefu na upeo wa masuala ya utangamano hawakuhusishwa na ubunge huu.

Alisema wakati umefika wa kuwatumia wataalamu hao ambao wangeweza kuiwakilisha vyema nchi katika bunge hilo.

Alionyesha wasiwasi wake kwenye baadhi ya majina yaliyotangazwa hivi karibuni akionya kuwa wengi hawana uwezo wa kukabiliana na hoja za masuala ya mtangamano wa Afrika Mashariki ikilinganishwa na wenzao wa nchi wanachama.

Jumuiya ya Afrika Mashariki huundwa na Burundi, Kenya, Tanzania, Rwanda na Uganda.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment