


Wakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wameendelea kulia na Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kutokana na kukatikakatika kwa umeme bila kutoa taarifa.
Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa, umebaini kuwa baadhi ya maeneo ya mji wa Songea yanapata huduma hiyo kwa kiasi kidogo ikiambatana na mgawo ambao Tanesco haijauweka bayana huku baadhi ya maeneo mengine yakipatiwa umeme usiku wa manane na kukatwa alfajiri.
Uchunguzi huo pia umebaini kuwa katika taasisi za afya ikiwemo hospitali ya serikali ya mkoa na kituo cha afya cha Mjimwema, zimelazimika kutafuta namna nyingine ya kupata nishati hiyo.
Moja ya njia hiyo ni kwa uongozi wa taasisi hizo za tiba ni kuwa na jenereta kwa ajili ya kuwezesha kuendelea kutoa huduma pindi Tanesco inapokata umeme.
Baadhi ya mashine za kusaga nafaka ambazo zipo katika baadhi ya maeneo ya manispaa, zimeshindwa kutoa huduma kwa muda mwafaka na kusababisha wananchi wengi kulazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo nje ya Manispaa ya Ruvuma ambako hutumia dizeli.
Hali hiyo pia imewafanya wamiliki wa mashine hizo za kusaga kupandisha bei ya huduma hiyo tofauti na ilivyokuwa awali.
Baadhi ya wamiliki wa mashine za kusaga na kukoboa nafaka wamesema kitendo cha Tanesco kushindwa kutoa huduma hiyo kwa wakati, pia huwakosesha mapato na hivyo kutolipa kodi kwa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA).
Mmoja wa wafanyabiashara hao, Julius Mlawa, alisema huenda akalazimika kusitisha kwa muda usagaji na ukoboaji wa nafaka kama tatizo la umeme wa uhakika halitafanyiwa kazi.
Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk. Daniel Malekela, alisema wamelazimika kutafuta jenereta kubwa kwa ajili ya kuendelea kutoa huduma hiyo muhimu katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma kwa sababu huduma za upasuaji na maabara zinahitaji nishati ya umeme muda wote.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea, Nachowa Zakaria, alisema halmashauri hiyo iliangalia uwezekano wa kutatua tatizo hilo kwenye kituo cha afya cha Mjimwema mjini hapa kwa kununua jenereta ambalo linasaidia kwa kiasi kutoa huduma hiyo.
Meneja wa Tanesco mkoani Ruvuma, Mhandisi Monica Kebara, alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na kueleza kuwa hivi sasa huduma hiyo ya umeme inatolewa kwa mgawo kwa sababu uwezo wa ufuaji wa umeme umepungua sana kutokana na kuharibika kwa mitambo iliyopo Kibulangoma mjini hapa.
Alisema kituo hicho kina mashine saba za kuzalisha umeme lakini kwa hivi sasa ni mashine tatu ndizo zinazofanya kazi hiyo kwa kutoa megawati 2.6 wakati mahitaji ni megawati tano hasa ikizingatiwa kuwa katika mji wa Songea shirika hilo lina wateja 12,000.