Wednesday Jun 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Kujiuzulu mawaziri utata

24th April 2012
Print
Comments
  Zitto: Ya Pinda yametimia
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda

Siku tano za kelele za wabunge za kutaka kujiuzulu kwa mawaziri wanane, huku kukiwa na habari kwamba baadhi yao wameridhia kuachia ngazi, jana Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, hakutaka kuingia kwa undani katika suala hilo isipokuwa alisema: “Serikali inaahidi kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa ushauri na mapendekezo yaliyomo katika taarifa hizo.”

Pinda alisema hayo jana wakati akitoa hotuba ya kuahirisha Mkutano wa saba wa Bunge la 10 mjini hapa, na kusisitiza kuwa: “…Wabunge wameonyesha hisia zao katika kujadili masuala yote haya muhimu na mengineyo na hasa katika Mwenendo wa Matumizi ya Fedha za Serikali kwenye Wizara, Taasisi za Umma, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.”

Kinyume na ilivyokuwa ikitarajiwa kwamba Pinda angetamka lolote kama kweli kumekuwako na maamuzi ya kujiuzulu kwa mawaziri hao, alijielekeza tu kuahidi kuwa watafanyia kazi ushauri wote uliotolewa na wabunge wakati wakijadili ripoti za kamati za Bunge, hasa zile za Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Hesabu za Serikali (PAC) na Serikali za Mitaa (LAAC).

Alisema anawashukuru wabunge wote kwa kazi nzuri walizofanya katika siku zote za mkutano huo zikiwemo kujadili na kupitisha miswada mbalimbali.
 
Aliwapongeza wenyeviti  na  wajumbe  wa  kamati  za Bunge  zilizowasilisha taarifa mbalimbali bungeni na kueleza kuwa: “Wabunge wameonesha hisia zao katika kujadili masuala yote haya muhimu na mengineyo na hasa katika Mwenendo wa Matumizi ya Fedha za Serikali kwenye Wizara, Taasisi za Umma, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Nawashukuru sana kwa kujadili Taarifa zote kwa uwazi na hatimaye kutoa mapendekezo kwa Serikali namna ya kushughulikia matatizo yaliyojitokeza kwenye maeneo mbalimbali.”

Pia alisema mapendekezo ya wabunge yako katika makundi ya uimarishaji wa uongozi na utendaji katika wizara, taasisi za serikali, mashirika ya umma, mikoa na serikali za mitaa; usimamizi wa sheria, kanuni na taratibu zinazohusu masuala ya mapato na matumizi ya fedha; uimarishaji wa hatua za kupambana na rushwa, ubadhirifu na wizi wa mali za umma; uendelezaji wa hatua za kubana matumizi yasiyo ya lazima ndani ya serikali na vyombo vyake; na ulinzi wa rasilimali za nchi kwa maslahi ya taifa.

“Siku  zote  Serikali imekuwa tayari kupokea ushauri wa Bunge lako tukufu na baada ya kusikiliza mjadala na mapendekezo ya waheshimiwa wabunge, serikali inaahidi kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa ushauri na mapendekezo yaliyomo katika taarifa hizo.

Niwahakikishie waheshimiwa wabunge kwamba serikali itachukua hatua stahiki kuimarisha usimamizi na utendaji ndani ya wizara na serikali za mitaa na vyombo vyake na kuhakikisha viongozi na watendaji wake wanafanya kazi kwa umakini na uadilifu zaidi,” alisema.

Tangu kuanza kujadiliwa kwa ripoti ya PAC, POAC, LAAC wiki iliyopita na ya jana ya Kamati ya Maliasili na Mazingira, kumekuwa na wito wa kuwataka mawaziri wa wizara zilizoguswa na ubadhirifu na uzembe kuachia ngazi.

Miongoni mwa waliotajwa ni pamoja na Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, ambaye anadaiwa kuhusika katika ubadhirifu wa Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC). Alitajwa kuwa amepotea uaminifu na uadilifu kiasi cha kusema uongo bungeni ili kuficha maslahi binafsi katika ofisi za umma.

Katika moto huo uliowashwa kwa nguvu na wabunge wa vyama vyote, pia Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami, alitajwa kuhusika katika kumkingia kifua Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango la Taifa (TBS), Charles Ekelege, kutokana na kusema uongo katika kazi ya ukaguzi wa magari nje ya nchi.

Ekelege anadaiwa kusema uongo kuwa kuna kampuni zimepewa kazi ya kukagua magari yanayokuja nchini nje ya nchi, ambayo yanalipwa mamilioni ya fedha, lakini kamati ya wabunge iliyokwenda nchi za Singapore na Hong Kong, hawakukuta kampuni hizo.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda,  naye anadaiwa kushirishindwa kusimamia matumizi bora ya fedha za umma kiasi cha kuruhusu nyumba yake kukarabatiwa kwa mamilioni ya fedha.

Wengine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, George Mkuchika, ambaye anadaiwa kushindwa kusimamia fedha katika halmashauri mbalimbali nchini ambako ufisadi wa kuwango kikubwa umegundulika.

Yupo Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, anayetuhumiwa kwa kushindwa kusimamia sekta ya madini na umeme, kuweko kwa manunuzi makubwa ya mafuta ya kuendesha mitambo ya IPTL ambayo yameongezwa bei.

Pia yumo Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, ambaye atauhumiwa kushindwa kudhibiti ubadhirifu katika wizara yake kama ulivyobainika katika ugawaji wa vitalu vya uwindaji wa kitalii na usafirishaji wa wanyama hai nje ya nchi.

Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu, anatuhumiwa kuingilia mchakato wa kumpata mzabuni wa kujenga gati namba 12 na 13 katika Bandari ya Dar es Salaam; Profesa Jumanne Maghembe, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, anadaiwa kushindwa kudhibiti ununuzi wa pembejeo na ulipaji wa fedha za mdororo wa uchumi.

Pinda pia hakusema lolote juu ya jaribio la kutaka kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye, ambayo inaratibiwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, ambalo jana Spika wa Bunge, Anne Makinda alikabidhiwa majina ya wabunge 75 wanaotaka kumng’oa kutokana na kushindwa kuwasimamia mawaziri hao.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment