Wednesday May 22, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Bondia Cheka rumande kwa kugonga mtu

30th April 2012
Print
Comments
Bondia Francis Cheka

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni linamshikilia bondia Francis Cheka (30) mkazi wa Morogoro, kwa tuhuma za kumgonga mwendesha pikipiki.

Akiongea na NIPASHE jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa  huo, Charles Kenyela alisema kuwa ajali hiyo ilitokea juzi saa 8 alfajiri maeneo ya Manzese Tip Top, ambapo Cheka akiwa ndani ya gari namba T321 AAU, Toyota Corola akielekea Ubungo aliigonga Pikipiki namba T 507 BYR iliyokuwa ikiendeshwa na Hosea Mbaga.

Kenyela alisema kuwa Mbaga aliyekuwa na abiria, alikuwa akiendesha pikipiki hiyo upande wa watembea kwa miguu, alikuwa akitokea Ubungo kwenda Manzese aliigeuza ghafla pikipiki, jambo lililopelekea pikipiki yake kugongwa.

Kamanda Kenyela aliongeza kuwa abiria aliyekuwa kwenye pikipiki hiyo, amejeruhiwa na amelazwa kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, na Polisi inawashikilia Cheka, pamoja na Mbaga, na uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo unaendelea.

Cheka maarufu kwa jina la ‘SMG’ kutoka mkoani Morogoro, kwa mara ya tatu mfululizo Jumamosi usiku alifanikiwa kumpiga mpinzani wake, Mada Maugo kwa TKO katika raundi ya saba ya  pambano lililokuwa la raundi 12.

Pambano la mabondia hayo ambalo Cheka alijipatia zawadi ya gari lilifanyika kwenye ukumbi wa PTA, Saba Saba jijini Dar es Salaam.

Maugo baada ya kupigwa ngumi nyingi katika raundi tatu mfululizo, kiasi cha kutabiriwa kukaa chini wakati wowote, mwanzoni mwa raundi ya saba hakurejea ulingoni.

Msaidizi wake, Karama Nyilawila, alilazimika kutupa taulo ulingoni na kufanya hivyo alimaanisha kwamba Mada hataweza kuendelea na pambano hilo.

Refa wa pambano hilo kutoka Zambia, John Shipanuka ambaye alionekana kumudu kwa kiasi kikubwa alimuinua mkono Cheka na kumtangaza mshindi wa pambano hilo lililovutia mashabiki wengi wa mchezo huo wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani.

Refa huyo alionekana kumdhibiti Maugo tabia yake ya kukumbatia hivyo kutoa nafasi kwa mpinzani wake Cheka kuonyesha uwezo wake wa kumtwanga ngumi mara kadhaa.

Baada ya hapo, Maugo aliinuka kwenye kona yake na kwenda kumkumbatia Cheka na kocha wake, akisema kwamba amesalimu amri baada ya kuishiwa pumzi.

“Pumzi imekata, siwezi kuendelea,”alisema Maugo ambaye leo alionekana muungwana ingawa hakuwa tayari kusema kama atahitaji kupigana tena na Cheka kama ilivyokuwa inatokea baada ya mapambano mengine yaliyopita yanapomalizika.

Cheka alisema kwamba anamshukuru Mungu amemuwezesha kuendeleza ushindi dhidi ya Mada na hasa kwa mabondia wa Tanzania na sasa anageuzia makali yake kwa Japhet Kaseba ambaye naye ameomba pambano la marudiano.

Hata hivyo mwanzoni Maugo alilianza pambano hilo vizuri na katika raundi ya pili aliweza kumshinda Cheka na kama angeongeza juhudi huenda angeibuka na ushindi wa KO lakini haikuwa hivyo.

Raundi ya kwanza hadi ya tatu, Maugo alifanya vizuri, lakini baada ya hapo mambo yalikuwa magumu na tangu hapo wengi walijua angepigwa wakati wowote.

Katika mapambano ya utangulizi, mdogo wake Cheka, Cosmass Cheka alipigwa kwa pointi na Sadiki Momba katika pambano la uzito wa Light, wakati Hajji Juma alimpiga kwa pointi Emmilio Naffat uzito wa bantam.

Simba Watunduru alimpiga kwa KO raundi ya sita Mohamed Kashinde katika pambano la uzito wa Feather, wakati Amos Mwamakala alimpiga kwa pointi Said Muhiddin uzito wa Light.

Moro Best alimpiga Nassib Ramadhan kwa TKO raundi ya nne uzito wa Bantam na Salima Kabombora alimpiga Asha Ngedere kwa pointi uzito wa Bantam.
SOURCE: bongostaz.blogspot,com
 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment