


.jpg)
Waziri wa Uchukuzi, Dk.Harrison Mwakyembe, ameapa kuwa hataogopa vitisho vyovyote kuwafukuza kazi watumishi wa mashirika, taasisi na idara za serikali zilizopo chini ya wizara yake wanaokwenda kinyume cha utendaji kazi kwani kama ni suala la kufa alishaonja kufa kipindi alipougua.
Alisema hayo juzi wakati akizungumza na wafanyakazi wa Chuo cha Bahari kilichopo jijini Dar es Salaam baada ya kukitembelea ikiwa ni siku moja baada kutembelea Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).
“Nawahakikishia bandari itanyooka, nitapigana hadi dakika ya mwisho, sitaogopa kufa maana kama ni suala la kufa tayari nilishaonja kufa nilipougua sana,”alisema Dk.Mwakyembe.
Alisema nchi hii haisongi mbele kimaendeleo kutokana na maneno kuwa mengi na kwamba katika ziara yake aliyoifanya katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) amekuta kuna uozo mwingi na kuahidi kusafisha wale wote ambao wanatuhumiwa kuhusika na kashifa mbalimbali bandarini hapo.
Dk.Mwakyembe alisema wakati anachukua hatua za kusafisha kwa kuwang’oa watumishi wabadhirifu katika taasisi, idara, mashirika yaliyopo chini ya Wizara ya Uchukuzi, wanafunzi waliomaliza darasa la saba, kidato cha nne na sita wakae mkao wa kula kwa ajili ya kuziba nafasi hizo.
“Na katika hili sitanii, hapa nitaomba kabisa wale wanafunzi waliomaliza darasa la saba, kidato cha nne, sita na chuo kikuu waanze kujioorodhesha kabisa majina yao maana nitawafukuza kazi watu wengi sana katika wizara hii,” alisema Dk.Mwakyembe.
Aidha waziri huyo aliutaka uongozi wa Chuo cha Bahari kuwa wawazi kwa wafanyakazi wao kwa kuwaeleza mapato na matumizi ili watumishi wasiwe wanajenga hoja kwamba fedha zao zinaliwa.
Aliutaka uongozi kukipatia ofisi tawi la Chama cha Wafanyakazi haraka na kwamba hakuna sababu ya kuviona vyama hivyo kama vyama vya upinzani katika sehemu za kazi.
Dk.Mwakyembe alisema kama uongozi wa chuo hicho utashindwa kukupatia Chama cha Wafanyakazi ofisi wasishangae atakapochukua maamuzi kwa kugawa sehemu ya Mkuu wa Chuo hicho kuwa ofisi ya chama cha wafanyakazi.