


.jpg)
Kocha wa Simba, Mserbia Milovan Cirkovic, amesema kuwa ameshaanza kutoa 'dozi' maalumu ya mazoezi kwa wachezaji wake ambayo anaamini kuwa itawapa uwezo wa kufanya vizuri katika michuano ya klabu bingwa Afrika na pia kutwaa tena ubingwa wanaoushikilia sasa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Cirkovic alirejea nchini Jumapili usiki na Jumanne alianza kukinoa kikosi hicho kilichorejea jijini Dar es Salaam hivi karibuni baada ya kucheza mechi za kirafiki jijini Mwanza na Shinyanga huku nyota wapya, Salim Kinje na Patrick Kanu wakiwa ni miongoni mwa wachezaji wanaowavutia mashabiki wengi katika mazoezi yao kwenye viwanja vya TCC, Chang’ombe jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na NIPASHE jana, Cirkovic alisema kuwa Simba ya msimu ujao itaendelea kuwa bora na hivyo wapinzani wao wanapaswa kujiandaa vizuri zaidi.
Kocha huyo alisema kuwa uwezo wa wachezaji waliosajiliwa na uzoefu wake wa kukuza vipaji ndio vitakavyoisaidia Simba kuendeleza heshima yake katika msimu ujao wa ligi.
"Simba ndio timu itakayosumbua, Yanga na wapinzani wengine wakae tayari na kamwe wasifikiri kama wataweza kutamba, nina wachezaji wanaonifanya nijiamini kuwa tutafanya vizuri kwa mara nyingine," alisema Mserbia huyo.
Aliongeza kuwa muda alionao hivi sasa unatosha kukiimarisha kikosi hicho na kuwa tayari kukabiliana na timu yoyote kwenye mashindano yatakayoanza Julai 14 ya Kombe la Kagame.
"Msimu huu timu itakuwa tofauti kwa sababu naanza na wachezaji mwanzo wa msimu, nina muda wa kuwaandaa vizuri wachezaji na kuwasoma mapema ukilinganisha na msimu uliopita ambao niliikuta timu katikati ya msimu na usajili ulikuwa umeshamalizika," alieleza kocha huyo.
Alisema vilevile kuwa anavutiwa kuona wachezaji kutoka kikosi chao cha vijana (Simba B) kwani wanaonyesha wana kiu ya mafanikio na wanajituma kuhakikisha kuwa wanapata namba, jambo ambalo linainufaisha timu yao.
Katika kujiandaa na Kombe la Kagame, Simba tayari imeshacheza mechi mbili za kirafiki ambapo iliifunga Toto African 2-0 na kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Express ya Uganda.