


Tembelea eneo maarufu jijini hapa la Kaloleni, nyakati za usiku, utashuhudia jinsi lilivyochangamka. Ni eneo lenye nyumba nyingi za kulala wageni na baa pengine kuliko maeneo mengi ya jiji la Arusha.
Ni eneo la biashara ya haramu ya ngono, inayowavuta wanawake wanaofanya biashara ya kuuza miili yao maarufu kama ‘machangu doa’ wanaowahudumia wanaume waliobatizwa jina la ‘machangu papa.’
Miongoni mwao unawakuta wanaume na wanawake za watu, wenye vipato vikubwa na vidogo, wenye kazi nzuri na za kubangaiza. Kakoleni!
Kwa ujumla naweza kusema hii ni biashara haramu inayopendwa na `machangu papa’, uthibitisho ukiwa ni kuendelea kushamiri kwake na inalipa kwa `machangu doa’.
Pamoja na watu kwenda eneo hilo kupata kinywaji, wakazi wa hapa wakisema kwenda ‘kutoa loku’ wapo baadhi ya wasichana wa umri tofauti ambao huvinjari eneo hilo wakiwa wamepiga mavazi ya aina tofauti.
Kutokana na baridi iliyokuwepo, wengi wao wanapenda kuvaa suruali za Jeans, masweta na jacket.
Baadhi yao wanaomudu kuwa na kianzio cha kinywaji, wanakaa baa, wakiweka mitego ya kuwanasa `machangu papa’, lakini wengi wasiokuwa na uwezo wa kununua bia ya mwanzo, wanalazimika kujipanga kwenye kingo za nyumba kuanzia majira ya saa moja usiku na kuendelea.
Utawaona mara wakikatiza barabara na kwenda upande wa pili, au wakienda kununua vocha au wengine wakienda kuagiza chips, huku wakipepesa macho huku na kule kama abiria anayekwenda kupata chai huku akiliaangalia basi lisimuache.
Wakiwa wamesimama kwenye kingo za nyumba hizo, wanaonekana kama vile ni wanafunzi wanaosubiria kukaguliwa usafi, lakini tofauti na wao, hawa husubiri ukaguzi wa `machangu papa’ ambao ndio wateja wao wakuu.
Neema Sekiano, (sio jina lake kamili) ni msichana mkazi wa eneo la makazi duni la Unga Ltd, akiwa anaishi kwenye chumba kimoja katika nyumba ya udongo yenye wapangaji wengi.
Akitokea mkoa wa Singida, anasema alikuja kutafuta maisha baada ya kumaliza darasa la saba wilayani Iramba.
Alianza kwa kufanya biashara ndogondogo na baadaye akawa anafanya kazi katika mgahawa mmoja jijini Arusha, akiwa kama mpishi.
Lakini baada ya shughuli zake za kazi, anajivinjari katika mitaa ya Kaloleni kufanya mawindo ya kuwasaka ‘machangu papa.’
Arusha kama inavyojulikana na wengi kuwa ni ‘Geneva ya Afrika’ ni jiji ambalo wakazi wake wanatoka makabila na mataifa tofauti.
Ni ngumu kusema jiji hili ni la Wamaasai/Waarusha pekee, ingawa hao ni wenyeji asilia wa mji huu.
Kutokana na hali hiyo, tabia ya wakazi wa jiji hili ni ya mchanganyiko na hivyo kumekuwepo na watu ambao kwa asilia ni wachangamfu, wapole, wenye upendo na huruma na wachapa kazi lakini wapo pia ambao kwa upande mwingine wana tabia ya ukatili, wizi, ujambazi, uhuni na ufisadi.
Kukua na kupanuka kwa jiji hili, kumetokana na idadi ya wahamiaji kutoka mikoa ya jirani kama vile Kilimanjaro, Singida, Manyara, Tanga na hata ile ya mbali na hivyo kuongeza shughuli za kichumi na kijamii.
Shughuli za kisiasa za ndani na nje ya nchi, mahusiano ya kimataifa kama ile ya kutafuta amani na pamoja na ushirikiano wa kikanda ni moja ya mambo ambayo yanachangia kulichangamsha jiji hili na hali ambayo imefanya ughali wa maisha kwa wakazi wake wengi kuwa ya juu zaidi kuliko majiji yote nchi.
Ingawa ugumu wa maisha upo kwa watu wote, ukali zaidi unakuwa kwa watu wenye kipato cha kawaida na kipato cha chini.
Ufumbuzi wa hali hii, umewafanya wasichana wengi wakitumbukia kwenye biashara isiyo rasmi ya ukahaba, ingawa hapa na pale wapo wasichana wenye vipato vya kutosha wanaofanya shughuli hiyo wakitaka kujiongezea kipato wakisukumwa na hulka waliyonayo.
Mbali na Kaloleni, mtaa mwingine maarufu ni Levolosi, ambao kama ilivyo Kaloleni kuna nyumba nyingi za kulala wageni na baa wengi wakirandaranda mitaa hiyo kutafuta wateja wakiwemo watalii.
Neema akiwawakilisha wasichana wa ngazi yake, huwawakilisha pia wasichana au wanawake wanaofanya kazi katika mashirika binafsi, taasisi za umma ambao wanaonekana kuwa ni watu wenye kipato cha mshahara mzuri.
Wanawake hao baadhi wakiwa wake za watu hujikita katika mitaa mbalimbali kutafuta wateja, hususan, watalii, wafanyabiashara wakubwa, wafanyakazi wa mashirika ya nje au wengine wenye fedha zao.
Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE Jumapili, kwenye baadhi ya maeneo umebaini kwamba kwa wastani, msichana anaweza kupata Sh. 40,000 kwa usiku mmoja au zaidi ya hapo kutegemeana na maumbile, umri na mvuto aliokuwa nao.
Shirika lisilo la kiserikali la Jitegemee Vijana Foundation (JVTF), la mjini hapa, limezindua mpango maalum wa kuwawezesha wasichana wanaoishi katika mazingira duni na wale wanaojishughulisha na biashara haramu ya ukahaba jijini hapa.
Chini ya mpango huo, wanawake na wasichana wa aina hiyo watapewa mafunzo ya ujasiriamali na mbinu za kufanya biashara ili hatimaye waweze kuishi maisha mazuri.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Raymond Mashambo, anasema mradi huo wa miaka miwili unawajumuisha washiriki 40 ambao kati yao 20 watahudhuria mafunzo kwa awamu ya kwanza na wengine 20 kwa awamu ya pili. Hata hivyo, anasema kundi la kwanza tayari limekwishapata mafunzo hayo ya kuwajengea ujasirimali na mbinu za biashara.
Katika mafunzo ya siku mbili yaliyofanyika jijini hapa, Mashambo anasema washiriki walipewa mafunzo kuhusu masuala mbalimbali ya ujasiriamali, ambapo kila mmoja aliweza kubaini aina ya biashara ambayo anatarajia kuifanya baada ya kupata mafunzo.
“Baada ya kupata mafunzo kila mshiriki aliweza kubaini miradi midogo midogo itakayoianzisha kumwingizia kipato na baadae kuendesha biashara zao. Na wote waliokuwa na miradi ya biashara kabla walifundishwa namna ya kuiboresha,” anasema.
Anasema mbali na mafunzo hayo, JVTF iliwapa mtaji wa kianzio cha Shilingi 300,000 kila mmoja, fedha ambazo watatakiwa kuanza kuzirejesha baada ya miezi mitano kwa kiasi cha Shilingi 15,000 kila mwezi na kwa wale waliokuwa na biashara kabla walipata mafunzo ya kuboresha biashara zao.
Wasichana hao wataachwa wakifanya miradi ya biashara yao kwa uhuru bila kuwaingilia lakini wakifuatiliwa maendeleo yao kwa miezi mitano na baada ya hapo watatakiwa kuchangia Shilingi 15,000 kila mwezi kwa muda wa miezi 12 na fedha ambazo wanaweza kujikusanyia ni Shilingi 180,000 na kutokana na kiasi hicho watakatwa Shilingi 60,000 kama mtaji wa kuanzia kwa kundi lingine la watu 20.
Anabainisha kwamba lengo la mradi huo ni kuwawezesha wanawake 40 wanaoishi katika mazingira magumu na wanaojihusisha na biashara haramu ya ukahaba jijini hapa na katika maeneo ya jirani.
Chini ya mipango ya mradi huo, wanawake wa umri tofauti walichukuliwa kutoka kwenye mitaa katika uzinduzi wa kampeni hiyo kama njia mojawapo ya kuwafanyia ukarabati wa tabia na hatua za kuwarejesha kwa lengo la kupunguza makali ya maisha kwa wasichana wanaokabiliwa na ukosefu mkubwa wa ajira.
Kwa mujibu Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk. Honest Prosper Ngowi, mtafiti na mwelekezaji mshauri wa uchumi na biashara, japokuwa kuna ongezeko la ajira mpya kwa mwaka hasa katika sekta isiyo rasmi ya takribani, 630,000 ukosefu wa ajira unaendelea kuwa tatizo, hasa kwa vijana wenye umri kati ya miaka 18 hadi 34.
“Kwa ujumla, kiwango cha ukosefu wa ajira ni kikubwa zaidi kwa vijana wa kike ikilinganishwa na vijana wa kiume…inakadiriwa kuwa ukosefu wa ajira kwa vijana wa kike kwa mwaka 2006 ilikuwa asilimia 15.4
ikilinganishwa na asilimia 14.3 ya ukosefu wa ajira kwa vijana wa kiume,” anasema.
Anasema idadi ya wanawake katika ajira ni asilimia 24.7 tu na kwamba kiwango cha juu cha umaskini vijijini kinaelezwa kupitia vyanzo na njia za maisha.
Akizungumzia mipango ya mafunzo, Mashambo anasema watajikita pia kwenye maeneo maarufu kwa biashara haramu ya ukahaba mkoani hapa, kama vile, Mto wa Mbu, Karatu na Namanga.
Arusha ni moja kati ya miji ambayo, wasichana wake wengi hawana ajira huku ukikabiliwa na kasi ya uhamiaji kutoka vijijini wengi wao wakitafuta maisha, lakini baadhi yao wamejikuta wakijiingiza kwenye biashara haramu ya ukahaba, ili kupata riziki.
Hata hivyo, biashara hiyo inaimarika kila kukicha kutokana na baadhi ya wanaume kutumia uwezo wao kifedha kuwarubuni wasichana hao, na wakati mwingine wengine wakishindwa kuambulia cho chote, isipokuwa wakijiweka katika hatari ya kupata magonjwa ya kuambukizwa.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Alphonce Massaga, anasema programu hiyo imetengenezwa ili kuwahamasisha wanawake wanaoishi katika mazingira duni waweze kupata fursa za kupata ujuzi na hivyo kuwawezesha kuishi vizuri.
Massaga ambaye ni mfanyabishara na Mkurugenzi Mtendaji wa Alpha Associates, anasema: “Tunatumaini kwamba hatua hii itaboresha mbinu zao za kujipatia riziki kwa njia halali na kuachana na shughuli haramu za mitaani.”
“Ni matumaini yetu kwamba habari hii ya mafanikio itakuwa changamoto kwa wengine waweze kuwezeshwa na kupata mafunzo na ujuzi kwa manufaa yao,” anasema.
Arusha ikiwa ni kitovu cha utalii imekuwa ikipata watalii wengi wanaokuja kutembelea vivutio vya utalii katika Hifadhi za Wanyamapori za Manyara, Arusha, Tarangire, Serengeti na Hifadhi ya Ngorongoro.
Uchunguzi wa NIPASHE Jumpaili, umebaini kuwa biashara ya ukahaba haiwezi kukoma pasipo wanaume kubadili tabia kwa kuheshimu ndoa zao na kuacha kuwafuata `machangu doa’.
‘Machangu papa’ wakiacha kuwa wateja wa biashara hiyo, machangu doa watakosa soko.
Mwandishi wa makala haya anapatikana kwenye simu namba 0768411003.