Friday May 6, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Papic: Nikilipwa nitabaki Yanga

27th April 2012
Print
Comments
Kocha wa Yanga, Mserbia Kostadin Papic

Kocha wa Yanga, Mserbia Kostadin Papic amesema kuwa hatakuwa tayari kuiongoza timu hiyo kwenye mechi ya funga pazia la msimu wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Simba hadi atakapolipwa fedha zake za mshahara anazoudai uongozi wa klabu yake.

Yanga watakutana na vinara Simba katika mechi ya watani wa jadi Mei 5 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es huku wapinzani wao wakiwa wanapigania ubingwa wakati wao watakuwa wakikamilisha ratiba tu baada ya kutema kombe lao na hawatashiriki katika mashindano ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kwa sababu hawataweza kufikisha pointi 53 walizonazo Azam katika nafasi ya pili hata wakishinda dhidi ya mahasimu wao.

Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga, alikiri katika kituo kimoja cha redio kwamba Papic anawadai mshahara wa mwezi uliopita na wa Aprili ambao unaelekea ukingoni.

Akizungumza na gazeti hili jana, Papic alisema kuwa endapo hatalipwa pesa zake atajiandaa kurudi kwao na kuanza kufuatilia malipo yake hayo kwa kushitaki kwenye vyombo vinavyohusika kama kanuni za soka zinavyoelekeza.

Papic alisema kuwa hatakubali kuendelea kuifundisha Yanga bila ya kulipwa fedha anazodai kwa sababu anajua msimu wa ligi ndio umemalizika na timu hiyo haitakuwa na jukumu lolote katika kipindi cha mwezi mmoja.

"Leo (jana) usiku ndio nakutana na mwenyekiti, nitajua hatma yangu, ila maamuzi yangu hayatakuwa tofauti kama hawatanilipa. Najua huu si wakati mzuri kwa pande zote mbili," alisema kocha huyo ambaye alitua Afrika kwa mara ya kwanza mwaka 2000 mjini Johannesburg, Afrika Kusini na kufundisha klabu za huko.

Aliongeza kuwa atakuwa tayari kuendelea kuifundisha klabu hiyo endapo nao watampa mkataba mpya ingawa anaweka wazi kuwa Yanga ya sasa si ile aliyoikuta wakati anakabidhiwa mikoba na Mserbia mwenzake, Dusan Kondic, mwaka 2009.

"Kufundisha ni taaluma yangu, wakinilipa na wakisema wananihitaji nitabaki, kinyume na hapo nimeshajiandaa kurejea kwetu," Papic aliongeza.

Aliweka wazi kuwa si kama ana mgomo wa kuifundisha timu hiyo bali kumalizika kwa kibali cha kufanyia kazi hapa nchini ni sababu nyingine iliyomfanya asimame kuiongoza Yanga kwenye mechi ya juzi dhidi ya JKT Oljoro ya Arusha ambapo mabingwa hao wa zamani walipata ushindi wa magoli 4-1.

Papic aliliambia gazeti hili hivi karibuni kuwa anaidai Yanga zaidi ya Dola za Marekani 15,000 (sawa na Sh. milioni 23) na mara ya mwisho kupokea sehemu ya malipo ya mshahara wake ilikuwa ni Februari 6 ambapo alilipwa fedha za utangulizi (Dola za Marekani 1,000).

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles