


.jpg)
Huku kocha Mserbia Milovan Cirkovic akisaini mkataba mpya wa mwaka mmoja wa kuifundisha Simba juzi, mabingwa hao wa Tanzania Bara leo watawakabili Azam katika mechi ya pili ya makundi ya Kombe la Urafiki kuanzia saa 2:00 usiku kwenye Uwanja wa Amaan mjini Zanzibar.
Simba ilianza mashindano hayo juzi kwa ushindi wa magoli 2-1 dhidi ya mabingwa wa Ligi Kuu ya Zanzibar, Mafunzo, magoli yote mawili ya Wekundu wa Msimbazi yakifungwa na mshambuliaji mpya kutoka Ruvu Shooting, Abdallah Juma.
Azam yenyewe ilianza kwa sare ya 1-1 dhidi ya timu ya taifa ya vijana ya umri chini ya miaka 23 ya Zanzibar (Karume Boys). Kipre Tchetche ndiye aliyeisawazishia Azam katika kipindi cha pili cha mchezo huo uliofanyika juzi jioni.
Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema jana kuwa kikosi chao kiko vizuri na kimejipanga kuendeleza ushindi katika mashindano hayo huku kocha mkuu, Milovan Cirkovic, akipanga wachezaji chipukizi na wazoefu.
Kamwaga alisema kuwa kikosi chao kinatarajiwa kuongezwa nguvu na wachezaji wawili, Haruna Moshi 'Boban' na Felix Sunzu, ambao walitarajiwa kujiunga na wenzao kambini jana jioni.