Thursday May 5, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

`Ndoa za kukurupuka zina machungu yake`

11th March 2012
Print
Comments

Wiki iliyopita mpenzi msomaji wangu nilikumegea kituko cha harusi ambayo haikufungwa baada ya bibie kuzua kiroja kwa kuugua ghafla kiaina na hatimaye kukataa kufunga ndoa siku moja baada ya kufanyika sherehe kabambe ya send-off.

Kituko kile kilivuta hisia za wengi kiasi wengine walishindwa kuvumilia na kutoa maoni yao kuhusiana na tukio hilo. Je, baadhi ya ujumbe wa simu za kiganjani toka kwa wasomaji wetu zinasemaje? Fuatilia hapa chini;-

…“Huyo binti aliyekataa ndoa ni wazi kwamba alikuwa ameshaolewa. Jambo linalonipa uhakika kwamba Katavi alikuwa na mume ni pale alipomzuia mumewe mtarajiwa kwenda mapumziko ya wiki Katavi. Pia uwongo aliotumia wakati anaomba ruhusa kazini”. (Josephat Manyenye wa Chato, Mwanza).

…“Huyo mwanamke aliyekataa kufunga ndoa, kwanza inaonekana huko Katavi alikuwa na mwanaume mwingine aliyempya ujauzito. Inaonekana hakuwa na mapenzi ya kweli na huyo bwana harusi”. (Celestine Joseph wa Sengerema, Mwanza)

…“Habari, kilichomfanya binti agome ni ujauzito na mamake itakuwa alikuwa anajua. Kwa mtazamo wangu hiyo ndoa haitafungwa”. (Nenetwa, Mwanza)

…“Siku hizi ndoa nyingi zinafungwa kama maonyesho tu, mtu anafunga ndoa kwa kuwa watu wamesema haoi au kuolewa kwa hiyo hajali anayetokea yukoje, je, kampenda? Anachojua ni kuonyesha watu anaweza. Matokeo yake anaolewa huku ana bwana mwingine. Pia kutopata muda wa kujuana vizuri ni tatizo matokeo yake mnajikuta mnaigiza ninyi ni wapenzi na pia kwenye ndoa”.(Justine Mtasiwa simu 0752242039)

…“Ni jambo la kusikitisha sana lakini limetokea. Ni kushukuru kwa Mungu pia tujifunze kutafuta wenza ambao ni wacha Mungu na wanaojielewa na wanaojua hatari ya usaliti na unafiki.

Tusikurupuke na kuvamia watu ambao historia zao hazieleweki vyema. Na mwisho nawapa pole wote walioguswa na kadhia hii, wamejifunza mengi katika hili hivyo liwe darasa kwao na kwetu. Ieleweke wazi kila achumaye janga huchuma na watu wake?(Msomi wa Zanzibar).

…“Hongera Aunty kwa kuelimisha umma. Ukweli huyo bibi harusi mtarajiwa siyo mtu mzuri, na pia siyo mwaminifu kwa mwenzake. Na hata huyo mama yake si mtu mzuri inaonekana yeye anajua kila kitu kuhusu mtoto wake.

Kwanini asimkemee mtoto wake kwa udhalimu alioufanya. Je, haoni kuwa yeye ndiye kigezo cheche? Inasikitisha sana. Hayo ndiyo maoni yangu”.(Omar Kasongo, Wete, Pemba)

…“Kwanza nampa pole huyo bwana harusi kwa kutapeliwa na mpenziwe. Hapo tatizo ni huyo binti. Ni tapeli na hamjui Mungu. Inawezekana ana bwana mwingine ana maslahi naye binafsi na mamake hilo analijua.

Ugonjwa wa ghafla hilo ni zuga tu. Namshauri bwana harusi aachane na huyo mwanamke laghai akijaribu kulazimisha kumuoa ajue anakaribisha aibu kwake na familia yake na huenda akajutia uamuzi wake. Amuombe Mungu amchagulie mke mwema”.(Ngwambi Ngwambi, Dar). …“Tatizo dada zetu wa sasa ni tamaa zimewatawala kiasi kwamba anakuwa na msururu wa wanaume wengi. Sasa inapofikia mwisho huwa anaangalia maslahi zaidi tofauti na upendo wa dhati yaani mwanaume mwenye mali, fedha na utajiri ndiye anayemkubali yaani sasa wako kimaslahi zaidi.

Kilichotakiwa kufahamika na huyo binti angemfahamisha mapema huyo mwenzake kama hakumpenda toka awali, angemweleza mapema kuliko kumwacha jamaa katika wakati mgumu ikiwa ni pamoja na kuwachangisha watu michango ya harusi.

Na imekuwa vizuri huyo binti amekatalia nje ya kanisa kuliko kukatalia altareni ingekuwa aibu kubwa.

Ni mambo ya hatari sana na jambo la ajabu kila binadamu ana mipangilio yake katika moyo wake. Huyo dada amefanya kosa kubwa sana la kimaadili”.(Denis Njalambaya simu 0763630421).

Mpenzi msomaji, bila shaka umewapata wenzetu hao katika michango yao ya maoni kuhusiana na kituko kile cha bibi harusi kukamilisha send-off lakini katika hali isiyotarajiwa akakataa kufunga ndoa siku inayofuata. Hakika ni tukio lililowaacha wengi midomo wazi.

Na naamini kwamba kwa kuweka hadharani kituko kile, itakuwa fundisho kwa wengine wanaonyemelea anga za ndoa kuwa makini zaidi wanapochagua mwenza wa kufunga pingu za maisha. Au siyo msomaji wangu? Maisha Ndivyo Yalivyo. Mwenzako akinyolewa, wewe tia maji.

Kwa leo nilitaka tu sauti za wasomaji wetu zisikike kuhusiana na jinsi walivyolipokea tukio lile na maoni yao kwa manufaa ya wasomaji wetu wengine ambao walibahatika kusoma lakini hawakuweza kuchangia kwa sababu mbalimbali. Wote nawashukuru kwa kuwa pamoja katika safu yetu hii inayotuelimisha.

Kama msomaji wangu unacho kituko, tukio linalohitaji majadiliano, kuwa huru kunitumia ili tulichambue kwa pamoja kwa manufaa ya familia na jamii yetu kwa ujumla.

Ukiwa tayari kuwa huru kuwasiliana nami kwa kutuma ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 0774268581(usipige), au barua pepe; [email protected]

.Kumbuka kama hutapenda jina au simu yako itajwe gazetini tamka hivyo na hilo litaheshimiwa.

Wasalaam.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles