Wednesday May 22, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Nagul amrithi kocha Stewart Hall Azam

2nd August 2012
Print
Comments

Kocha wa timu ya vijana ya Azam, Vivek Nagul, raia wa India na Kally Ongalla wataiongoza timu ya Azam katika maandalizi yake kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara inayotarajiwa kuanza Septemba Mosi mwaka huu kufuatia kutimuliwa kwa kocha Stewart Hall.

Bodi ya Wakurugenzi ya Azam ya jijini Dar es Salaam juzi ilitangaza  kumfukuza kazi Hall kutoka England baada ya kocha huyo kukaidi maagizo aliyopewa na bodi hiyo ya kutompanga mshambuliaji Mrisho Ngassa katika mechi yao ya fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) dhidi ya Yanga, ambayo walilala 2-0.

Uongozi wa Azam ulimtaka Hall kutompanga Ngassa baada ya kukasirishwa na kitendo cha mshambuliaji huyo kuonyesha mapenzi yake kwa Yanga wakati akishangilia goli alilofunga dhidi ya Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwenye mechi ya nusu fainali ya Kombe la Kagame.

Meneja wa Azam, Patrick Kahemele, alisema jana kwamba tayari wameshampa Hall haki zake zote na wakati wanajipanga kusaka kocha mwingine, timu yao itakuwa chini ya Nagul na Ongalla ambao walikuwa wasaidizi wa Hall wakati wote.

Kahemele alisema kuwa Hall alikuwa amemaliza mkataba wake tangu mwezi Mei mwaka huu lakini uongozi ulimuomba aendelee kuifundisha timu hiyo iliyokuwa inakabiliwa na mashindano ya Kombe la Kagame na hivyo ilimuongeza mkataba mfupi wa miezi mitatu ambayo ilikuwa inaelekea ukingoni.

"Kitendo cha Ngassa kuishangilia Yanga kwetu kilikuwa ni sawa na tusi, ndio maana tuliamua asimpange lakini mwalimu (Hall) alikaidi maagizo na kumuweka kwenye orodha ya wachezaji wa akiba," alisema meneja huyo.

Mbali na kuifundisha Azam, Hall pia alikuwa akiifundisha timu ya soka ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) na ndio ilikuwa timu ya kwanza kusaini nayo mkataba baada ya kukosa ajira ya kuinoa timu ya Tanzania (Taifa Stars).
 
Makocha wengine ambao waliwahi kuifundisha Azam ni pamoja na Wabrazil, Neider dos Santos ambaye aliwahi pia kuifundisha Simba, Itamar Amorim (Taifa Stars) na Mzalendo, Sylivester Marsh.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment