Saturday Apr 30, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Serikali yaokoa mil.400/- madai hewa ya walimu

20th May 2012
Print
Comments

Serikali imeokoa zaidi ya Sh milioni 400 zikiwa ni madai hewa yaliyokuwa yamewasilishwa kwa ajili ya kulipa stahili mbalimbali za walimu.

Fedha hizo zimeokolewa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kufuatia uhakiki wa vielelezo vya madai uliofanywa na Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa serikali anayechunguza, kuhakiki na kuidhinisha stahili za wanaoidai.

Naibu Waziri wa wizara hiyo , Phillipo Mulugo, alibainisha hayo wakati alipohojiwa na NIPASHE Jumapili juu ya tishio la walimu la kuipa Serikali wiki mbili iwe imewalipa madai ya Sh. bilioni 13 na pia kuwapa nyongeza ya mshahara kwa asilimia 100 utakaolipwa kuanzia Julai, mwaka huu.

Waziri Mulogo, alifafanua kuwa fedha za walimu zinalipwa kila wakati na uhakiki umewezesha kuokoa kiasi hicho cha fedha ambacho kingeishia mikononi kwa wadai hewa.

Aliongeza kuwa kinachochelewesha malipo ni uhakiki kwani baadhi ya viambatanisho vinavyotolewa si sahihi, vingine vina upungufu, wengine hawana vithibitisho na wakati mwingine wasio waadilifu wanawasilisha madai zaidi ya mara mbili.

Alitoa mfano kuwa mwaka 2009 malipo yalipoanza kutolewa baadhi ya walimu walilipwa lakini waliposikia suala la kulipwa mafao waliwasilisha madai ambayo kama yasingehakikiwa Serikali ingepata hasara kwa kulipa madai hewa.

Alisema licha ya kwamba alikuwa ng’ambo kikazi wiki nzima iliyopita, “tisho’’ hilo la walimu kwa Serikali linatolewa kipindi ambacho haijasimama kuwalipa stahiki zao japo ulipaji unachelewa kutokana na uhakiki ambao ni lazima ufanywe.’’

Aliwataka walimu wasiwe na hofu kwani fungu la kulipa stahiki na madai ya walimu lipo na pia zipo fedha za madai ya walimu walio chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Kuhusu hoja ya kulipwa nyongeza ya mishahara kwa asilimia 100 ifikapo Julai, Mulogo alisema anaichia Ofisi ya Rais Manejimenti ya Utumishi wa Umma na kwamba Wizara ya Elimu haijawahi kujadili suala la nyongeza hiyo ya mshahara kwa asilimia 100.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Ramadhani Kija, alipohojiwa juu ya uwezekano wa Hazina kuwalipa walimu nyongeza ya mshahara kwa asilimia 100 kuanzia Julai, alisema hilo ni suala linalofanyiwa maamuzi na ngazi za juu mathalani Baraza la Mawaziri.

Kija alisema kuongeza mishahara na kuanza kuilipa kwa mwezi mmoja utategemea maamuzi ya serikali lakini hata hivyo alisema hana ukakika kama walimu wamewasilisha maombi yao serikalini ya kupewa nyongeza hiyo.

Alisema mkaguzi huyo wa ndani anasimamia na kushughulikia wadai wa nchi nzima wanaoidai Serikali na kuwataka walimu wawe na vielelezo, wafuate taratibu ili walipwe.

Wiki hii Chama cha Walimu Tanzania (CWT), kiliipa serikali siku 12 kuanzia Ijumaa iwe imelipa madeni ya walimu yanayofikia shilingi bilioni 13. Pia kiliibana na kutaka kuwa mwaka ujao wa fedha ianze kuwalipa mshahara na nyongeza ya asilimia 100.

Kilitaka serikali kuweka posho ya kufundishia asilimia 55 kwa walimu wa sayansi na wa sanaa na pia iweke kwenye bajeti yake asilimia 30 ya mishahara ya walimu wanaofanya kazi kwenye mazingira magumu.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles