Monday May 2, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Tuna mengi ya kujifunza fainali za AFCON 2012

23rd January 2012
Print
Comments
Maoni ya katuni

Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2012) zimeanza juzi katika nchi za Equatorial Guinea na Gabon ambapo nchi 16 zilizofuzu fainali hizo zinawania kombe hilo lenye hadhi juu kwa ngazi ya mataifa barani Afrika.

Wakati fainali hizi zikiendelea, macho na masikio ya wafuatiliaji wa mchezo wa soka yameelekezwa kwa nchi wenyeji wa fainali hizo. Kwa bahati mbaya, kama ilivyo ada, Tanzania kwa mara nyingine imeshindwa kuzufu na hivyo watu wake kubaki kuwa washangiliaji wa timu za mataifa mengine.

Tangu Tanzania ilipopata nafasi ya kwanza ya kushiriki fainali za AFCON mwaka 1980, haijawahi kushiriki tena na mara kadhaa imejaribu na kuishia kutolewa katika hatua za awali.

Tumeshuhudia kwa mara nyinginbe tukizikosa fainali za mwaka huu, kama ilivyokuwa katika fainali nyingine kadhaa zilizopita. Kwa kuzingatia ukweli huo unaouma, tunadhani kwamba sasa ni wakati muafaka kwetu kujifunza kupitia fainali zilizoanza juzi ili nasi turekebishe tunapokosea na mwishowe kushiriki tena fainali hizo.

Wadau wa soka wanapaswa kuwasoma wenzetu na kujua ni njia gani wamepitia hadi kuwa na timu zinazoshiriki fainali hizo wmaka huu na nyingine kadhaa zilizopita.

Kuna baadhi ya nchi ambazo zimefuzu fainali hizo kwa namna ya kusisimua. Mfano ni Botwana ambayo kiasi imeshangaza dunia ya soka kwani si miongoni mwa mataifa vigogo ya mchezo huo barani.

Botswana haina wachezaji wenye majina makubwa katika soka la kulipwa barani Ulaya na kwingineko duniani. Hata hivyo, kwa kutumia vipaji walivyo navyo, walifanikiwa kuwa miongoni mwa timu za kwanza kabisa kufuzu fainali za mwaka huu za AFCON, kama ilivyokuwa kwa vigogo Ivory Coast, Senegal na Ghana.

Mbali ya Botwana nchi nyingine iliyofuzu fainali hizo na kushangaza wafuatiliaji wa soka ni Niger. Burkina Faso na  Libya pia hazikuwa zikizungumzwa hapo kabla, lakini zote zimefuzu huku mataifa makubwa ya soka barani kama Misri, Nigeria, Cameroon n Afrika Kusini zikishindwa.

Mikakati madhubuti ndio msingi wa mafanikio. Mathalan, Libya wamefuzu kutokana na mipango yao ya muda mrefu. Matatizo ya vita vya wenyewe kwa wenyewe yaliwafanya wacheze baadhi ya mechi za nyumbani wakiwa ugenini. Lakini pamoja na yote hayo, hatimaye wakafuzu na sasa ni miongoni mwa timu tunazoishia kuzishabiki kupitia matangazo ya televisheni.

Zambia ambayo ilipotea katika soka la kimataifa kwa muda mrefu, sasa imerudi katika fainali hizo kwa kishindo na juzi ilipata ushindi usiotarajiwa wa mabao 2-1 dhidi ya Senegal, taifa linalopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa mwaka huu wa AFCON.

Mifano ya nchi hizo chache zilizofuzu fainali za mwaka huu itaufanya tuwe na jambo moja kubwa la kufanya; nalo ni kujifunza juu ya kile walichofanya wenzetu hata wakafika kwenye fainali hizo huku sisi tukiwa ni wasindikizaji wazoefu.

Tunadhani kwamba sasa, hakuna namna ya mkato tunayotakiwa kuifanya zaidi ya kufuatilia fainali hizo kwa karibu na kujifunza mbinu na njia walizopitia wenzetu kwa vitendo. Kamwe tusiendeleze mipango hewa yam domo na kwenye makaratasi ambako imethibitika mara kadhaa kuwa huko tuna uwezo wa kutosha lakini hakuna tunachonufaika nacho kama hatubadili maneno kuwa vitendo.

Mradi wa kuendeleza soka la vijana uliosaniwa mwaka 2008 kati ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Peter Johnson ambaye alianzisha shule maalum kwa ajili ya kuendeleza soka (TSA), kutoa elimu na mafunzo kwa wachezaji nje ya nchi unapaswa kurejeshewa nguvu mpya ili matunda yake yaje kusaidia uundwaji wa timu za taifa za baadaye.

Shime, wachezaji wa soka, viongozi wa klabu za mchezo huo, mashabiki na wadau wengine wote wajitahidi kadri wanavyoweza kujifunza kupitia fainali zinazoendelea za AFCON kwa manufaa ya baadaye ya mchezo huo nchini.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles