Monday Feb 8, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Suala la Nassari mikononi mwa DPP

10th May 2012
Print
Comments
Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari

Hatima ya Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari, kushtakiwa au la kwa maneno yanayodaiwa kuwa ya uchochezi, imo mikononi mwa Mkurugenzi wa Mashataka  (DPP).

Naibu Kamishina wa Jeshi la Polisi (DCP), Isaya Mngulu, alisema hayo jijini hapa jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha.

“Katika mahojiano ya jana (juzi), kifupi (Nassari) alieleza kwamba hayo maneno alitamka ila alitoa maana aliyokuwa nayo,” alisema.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi jioni baada ya mahojiano na Jeshi la Polisi, Nassari, alisema kauli yake ilikuwa ni kuwapa hamasa mikoa mingine ya Tanzania ili ipate wivu wa kuwa na mabadiliko kama ilivyo kwa mikoa ya Kanda ya Kaskazini na mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Nassari anadaiwa kuwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika Jumamosi jijini hapa, alitamka kauli kwamba atatangaza uhuru wa Meru kwa kushirikiana na mikoa ya Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa.

Pia anadaiwa kuwa alitamka kama polisi hawatawakamata wauaji wa aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema tawi la Usa River, watampiga marufuku Rais pamoja na Waziri Mkuu kutembelea Arusha.

Maneno mengine ni iwapo atapata vijana 500 kama yeye wataweza kwenda Magogoni, kauli ambayo aliifafanua kwamba haina maana ya kwenda kukaa Ikulu bali kwenda kuonana na Rais.

Nassari alifafanua kwamba yeye ni mtu mdogo na hana nguvu wala mamlaka ya kutangaza sehemu yoyote ya nchi kuwa huru na pia hawezi kumzuia Rais au Waziri Mkuu kutembelea sehemu yoyote ya nchi.

“Matarajio ya kosa wanalotakiwa kushtakiwa nayo ni  mpaka hapo itakapopata ridhaa ya DPP na hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 63(b) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Cap 16,” alisema DCP Mngulu.

Alisema jana walielezwa mpaka hapo watakapohitajika watajulishwa na kwamba hawakufanya mahojiano yoyote kwa kuwa yalimalizika juzi.

“Kamanda Mngulu alisema kisheria mtuhumiwa anatambulika kuwa anahojiwa pale anapoanza kuandika maelezo na muda wa mahojiano ni saa tatu…kama mahojiano bado yanaendelea ni lazima waahirishe ili kupata muda wa mapumziko,” alisema.

Hata hivyo, alisema upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika, na wamemwachilia hadi hapo watakapomhitaji tena.

Mbunge Nassari alihojiwa juzi na makachero wa polisi kuanzia saa 8:20 alasiri hadi saa 11:15 jioni kufuatia kauli aliyoitoa kwenye mkutano wa hadhara wa Chadema Jumamosi iliyopita katika viwanja vya Unga Ltd, jijini hapa.

Mgeni rasmi katika mkutano huo wa ‘Vua gamba, vaa gwanda,’ alikuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, ambapo pamoja na mambo mengine uliandaliwa kwa lengo la kuwapokea wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) waliohamia Chadema.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment