


.jpg)
Beki Stephano Mwasika na mshambuliaji Jerry Tegete watakosa mechi zote za klabu yao ya Yanga katika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara utakaoanza Sepetmba Mosi ikiwa ‘Wanajangwani’ hawatalipa faini waliyotozwa nyota hao katika msimu uliopita wa ligi, imefahamika.
Mwasika na Tegete walikutwa na hatia katika mechi ya ligi kuu iliyoambatana na vurugu kali kati ya timu yao na Azam kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kuadhibiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutocheza mechi zote zilizokuwa zimebaki za ligi msimu uliopita na pia kila mmoja kutakiwa kulipa kulipa faini ya Sh. Milioni Mbili.
Taarifa kutoka TFF zimeeleza kuwa Tegete na Mwasika wamemaliza kutumikia adhabu yao ya kufungiwa mechi tatu, lakini hawataruhusiwa kucheza msimu ujao kwa vile faini waliyotozwa bado haijalipwa.
Nyota hao na wenzao Nadir Haroub 'Cannavaro' na Omega Seme, waliadhibiwa na Kamati ya Nidhamu ya (TFF) katika vurugu zilizoibuka dhidi ya Azam ambapo refa Israel Nkongo alipigwa.
Hata hivyo, wachezaji hao watapata nafasi ya kuitumikia Yanga katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) ambayo yataanza Julai 14 hadi 29 chini ya usimamizi wa Shirikisho la Soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Akizungumza jana, Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alifafanua kuwa licha ya Tegete na Mwasika kumaliza adhabu zao za mechi, lakini watatakiwa walipe faini kwanza ndipo waruhusiwe kucheza.
Wambura alisema vilevile kuwa, hata kama wachezaji hao wataachwa katika klabu hiyo, watatakiwa kulipa faini na ndipo wataruhusiwa kusajiliwa na timu nyingine za ligi kuu au daraja la kwanza.
"Yanaga wataruhusiwa kuwatumia katika mashindano ya Kagame kwa sababu usajili wa wachezaji katika michuano hiyo unaangalia leseni ya ndani, tunawakumbusha (Yanga) mapema na wote ambao wanatakiwa kukamilisha taratibu za usajili wafanye hivyo mapema," alisema Wambura.
Aliongeza kuwa TFF hufanya hivyo kwa kila timu ambayo wachezaji wake huadhibiwa kwa makosa mbalimbali na kuwakumbusha Yanga watekeleze wajibu wa kulipa kabla msimu mpya haujaanza.
Yanga iliyomaliza ligi kuu msimu uliopita ikiwa katika nafasi ya tatu, imeshaanza maandalizi ya msimu mpya na Jumamosi ilicheza mechi yake ya kwanza ya kirafiki dhidi ya mabingwa wapya wa Uganda, klabu ya Express ambapo Tegete aling’ara na kuwafungia mabao yote yaliyowapa ushindi wa 2-0.
Mabingwa hao watetezi wa Kombe la Kagame, wataanza kampeni za kutetea ubingwa wao kwa kuvaana na Atletico ya Burundi katika mchezo wa kwanza wa fungua dimba utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa huku watani zao wa jadi, Simba wakianza kampeni zao kwa kucheza dhidi ya URA ya Uganda.
Wakati huo huo, Kamati ya Uchaguzi ya TFF jana ilikuwa ikisikiliza pingamizi zilizofikishwa za wagombea wawili wanaowania nafasi za uongozi katika uchaguzi mdogo wa Yanga utakaofanyika Julai 15 jijini Dar es Salaam.
Mmoja wa wagombea waliowekewa pingamizi na kuhojiwa jana ni Yono Kevela anayewania cheo cha Makamu Mwenyekiti na Ujumbe wa Kamati ya Utendaji.