Tuesday Jun 18, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Stars bado ina nafasi Kombe la Dunia 2014

4th June 2012
Print
Comments
Maoni ya katuni

Timu ya taifa ya soka, Taifa Stars ilianza vibaya kampeni zake za kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 katika mechi yao ya ugenini dhidi ya Ivory Coast iliyochezwa juzi kwenye Uwanja wa Houphouet Boigny mjini Abidjan.

Washambuliji Salomon Kalou na Didier Drogba ambao hivi karibuni waliisaidia Chelsea kutwaa taji la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, ndio waliofunga mabao ya wenyeji katika kila kipindi na kuwapa mwanzo mzuri katika kundi lao la C.

Katika mechi nyingine ya kundi hilo juzi, timu za mataifa ya Morocco na Gambia ziliishia kutoka sare ya 1-1, hivyo kuwapa Stars matumaini ya makubwa ya kuendelea kupambana ili kusaka nafasi moja wapo kati ya tano za Afrika kwenye michuano ijayo ya Kombe la Dunia itakayofanyika Brazil mwaka 2014.

Kutokana na matokeo ya mechi za juzi, sisi tunaamini kwamba licha ya kufungwa, Stars ambayo ilimaliza mechi hiyo ikiwa na wachezaji 10 uwanjani kufuatia beki wake wa kutegemewa, Aggrey Morris kutolewa nje kwa kadi ya pili ya njano, bado ina nafasi ya kufanya vizuri kama ilivyo kwa timu nyingine.

Hadi sasa, Stars na timu nyingine zote za kundi la C zimebakiza mechi tano kabla ya kumalizika kwa mechi za michuano hiyo ya awali.

Kinachotakiwa kufanywa ili kuhakikisha kuwa Watanzania wanatimiza ndoto ya kuiona timu yao ikifuzu kwa mara ya kwanza katika fainali za Kombe la Dunia zilizoanza mwaka 1930 ni kuhakikisha kuwa tunasaka mbinu muafaka za kutupatia matokeo mazuri katika mechi zote zilizobaki.

Stars inayotarajiwa kurejea nchini leo na kushuka tena dimbani Jumapili ijayo kucheza dhidi ya Gambia kwenye uwanja wa nyumbani wa Taifa, italazimika kufanya marekebisho makubwa kiuchezaji katika safu yake ya ulinzi.

Kocha Mdenmark Kim Poulsen anapaswa kuwapa mbinu mbadala mabeki wake ili waongeze umakini katika kuzuia na kuepukana na makosa ya kizembe yatakayowapa nafasi wapinzani kufunga mabao kirahisi; kama ilivyotokea juzi wakati Kalou alipofunga bao la kwanza baada ya mabeki wa Stars kupoteza mpira kwa namna ya kushangaza.

Washambuliaji wa Stars wanapaswa kuongeza umakini pia ili kuhakikisha kwamba wanatumia vyema kila nafasi watakayopata na mwishowe kuwapa raha Watanzania.

Tunatambua kwamba Gambia watakaovaana na Stars wiki ijayo na Morocco waliowahi pia kuwa katika kundi moja na Stars katika mechi za kuwania kufuzu kwa fainali zilizopita za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2012) hawana timu nyepesi.

Hata hivyo, kiwango kilichoonyeshwa na Stars katika mechi ya juzi dhidi ya Ivory Coast na pia katika mechi ya kujipima nguvu iliyomalizika kwa sare ya 0-0 dhidi ya Malawi vinatupa imani kuwa bado kuna matumaini makubwa ya kujirekebisha na kufika mbali.

Kipigo cha mabao mawili tu walichokipata wachezaji 10 wa Stars kutoka kwa kikosi cha akina Drogba kilichojaa nyota kama Gervinho wa Arsenal, Kolo Toure wa Manchester City na Tcheikh Tiote wa Newcastle United ni dalili kuwa wakiendelea kuungwa mkono, wachezaji Stars wanaweza kucharuka na kufanya vizuri katika mechi zote zilizosalia.

Tunaamini kuwa katika siku zilizobaki kwa ajili ya maandalizi kabla ya kucheza dhidi ya Gambia Jumapili, kocha Poulsen na benchi lake la ufundi watarekebisha makosa kadhaa ya wachezaji wao kama yale ya mabeki kuonekana wakikaba washambuliaji wa upinzani kwa macho na hatimaye kuruhusu mabao yasiyotarajiwa.

Aidha, tunawakumbusha mashabiki wa soka kuwa nao ni sehemu muhimu kwa mustakabali wa Stars.

Waache tofauti zao na badala yake watangulize maslahi ya taifa kwa kuishangilia Stars kuanzia mwanzo wa mechi hadi mwisho ili hatimaye tuvune matokeo mazuri.

Vitendo vya kuzomea hukatisha tama wachezaji, hivyo tusiruhusu vitokee katika kipindi hiki ambacho kila Mtanzania anataka kuona tukikomesha tabia ya kuwa wasindikizaji katika kila michuano ya kimataifa.

Tuendelee kuiunga mkono Stars huku tukijua kwamba bado tuna nafasi ya kujirekebisha na kufanya vizuri katika kampeni yetu ya kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2014.

 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment