Monday Feb 8, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Waandishi watoa ushahidi kesi ya uchaguzi Igunga

8th May 2012
Print
Comments

Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, jana ilipokea ushahidi wa magazeti mawili, Mtanzania na Nipashe, ikiwa ni mwendelezo wa kusikiliza maelezo ya mashahidi kwenye kesi ya kupinga matokeo yaliyompatia ushindi Mbunge wa Igunga, (CCM), Dk. Dalaly Kafumu.

Shauri hilo lilifunguliwa na mlalamikaji Joseph Kashindye dhidi ya Dk. Kafumu, Mwanasheria Mkuu wa serikalina msimamizi wa uchaguzi.

Mwandishi wa Mtanzania, Arodia Peter, alitoa ushahidi kuhusu habari ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Willson Mukama, aliyedai kuwa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimepeleka makomandoo 33 Igunga ili wavuruge uchaguzi.

Arodia alitakiwa na mwanasheria wa upande wa mlalamikaji, Profesa Abdallah Safari, aieleze Mahakama ukweli kuhusu habari hiyo ambapo alidai  kuwa katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika ofisi za CCM Wilaya ya Igunga, Mukama alisema Chadema wamepeleka makomandoo hao waliopata mafunzo ya kigaidi katika nchi za Afghanistan , Pakstan na Libya.

Ushahidi mwingine wa gazeti la Mtanzania, ulihusu ahadi zilizotolewa na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, kwamba atatenga bajeti maalum ya kujenga daraja la mto Mbutu pamoja na barabara nyingine iwapo wananchi wangempigia kura, Dk. Kafumu wa CCM.

Mwandishi wa Nipashe, Sharon Sauwa, naye alidai kuwa Waziri Magufuli alitoa ahadi ya ujenzi wa daraja la Mbuntu endapo wananchi wa jimbo hilo watachagua mgombea wa CCM.

Awali, wakili wa serikali na wakili wa mjibu madai waliweka pingamizi kuwa nakala za magzeti hayo visipokelewe kama vielelezo mahakamani.

Hata hivyo, Jaji anayesikiliza kesi hiyo, Mery Shangali, alitupilia mbali pingamizi hilo, akisema vielelezi hivyo ni sahihi kwa kuwa waandishi walioandika habari hizo wapo mahakamani kuvitolea ushahidi.

Jaji Shangali pia aliwataka mawakili wa upande wa wajibu maombi, wazingatie muda na kuacha maswali ambayo hayahusiani na mada inayozungumuziwa mezani ili kuokoa muda wa shauri hilo hivyo ushahidi huo kupokelewa. 

Kesi hiyo itaendelea leo kwa mashahidi wa mlalamikaji kuendelea kutoa ushahidi wao.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment