Thursday May 23, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Wabunge waendelea kuipa serikali kichapo

25th April 2012
Print
Comments
  Wararua mpango wa maendeleo
  Yaambiwa miaka 15 hakuna jipya
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi, Dk. Abdallah Kigoda

Wabunge wamecharukia mapendekezo ya Mfumo wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2012/2013 kuwa hauna jipya na haulengi kumkomboa masikini.

Waliyasema hayo jana walipokuwa wakichangia mpango huo katika ukumbi wa Pius Msekwa, mjini Dodoma.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi, Dk. Abdallah Kigoda, alisema mpango wa maendeleo umekuwa ukitayarishwa kwa mfumo ule ule kwa zaidi ya miaka 15 iliyopita.

Alisema kamati imeshauri mfumo huo ubadilike ili uendane na wakati uliopo hivi sasa.

Kuhusu udhibiti wa matumizi mabaya ya fedha katika halmashauri, kamati ilisema halmashauri nyingi za wilaya ambazo matumizi yake ya fedha hayalingani na thamani ya fedha zinazotolewa.

“Usimamizi wa fedha ukoje pamoja na hatua gani ziagizwe na kuchukuliwa kupunguza matumizi mabaya ya fedha,” alisema Dk. Kigoda.

Alitoa mfano kuwa lipo tatizo sugu la kulipa mishahara hewa kwa kuweka waliofariki na waliostaafu kwenye orodha ya malipo ya mishahara.

Alisema kwa mwaka 2010/2011 takribani Sh. bilioni moja zilipotea kwa utaratibu huo na haya ni matumizi yasiyo na tija.

Pia alisema matokeo yake ni kuwa matumizi yanaendelea kuwa makubwa kwa upande wa matumizi ya kawaida (takribani Sh. trilioni 9.2) ikilinganishwa na matumizi ya maendeleo (takribani Sh. trilioni 4.1). Dk. Kigoda ambaye pia ni mbunge wa Handeni (CCM), alihoji mapendekezo hayo yanaagiza nini.

Kamati hiyo ilisema rasilimali chache za serikali zimekuwa zikisambazwa katika maeneo mengi hali ambayo imeleta matokeo hafifu.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, alisema haoni kitu kipya katika mpango huo ambacho wabunge wakichangia wananachi wataona kuna kitu kikubwa kimefanyika.

Zitto alisema mambo mengi yaliyomo katika mpango huo yanaongelewa kila siku.

Alisema utafiti uliofanywa na Marekani na Tanzania umebaini kuwa ili nchi ipate maendeleo serikali iwekeze katika umeme na barabara za vijijini.

Alishauri serikali kujikita katika mambo machache na baadaye katika utekelezaji wa mipango.

Alisema katika mpango huo takribani vipaumbele 15 vimeainishwa na kwamba katika mazingira yaliyopo haiwezekani kutekeleza mambo yote.

Zitto alisema Dk. Kigoda amezungumzia kila wakati kuhusiana na chakula, lakini hakuna jitihada ya kuzalisha.

Alisema kila siku serikali imekuwa ikitoa vibali vya kuagiza sukari nje ya nchi na hakuna jitihada za kujenga viwanda vipya.

“Kuna watu wanafaidika na vibali vya kuagiza sukari,” alisema Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC).

Mbunge wa Viti Maalum, (CCM), Easter Bulaya, alihoji kutokuwepo kwa mpango wa kusaidia wafugaji.

Alisema katika mpango kumekuwa na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kilimo, lakini wafugaji hawaelezewi kabisa katika mpango huo.

“Kwa kufanya hivyo, itasaidia kutatua migogoro kati ya wakulima na wafugaji,” alisema Bulaya.
Mbunge wa Viti Maalum (CUF), Magdalena Sakaya, alitaka kuwepo kwa muda wa Bunge kutathmini mipango inayotangulia.

Pia alisema alikuwa anategemea kuwepo na mpango wa kuthibiti na kusimamia mapato ya serikali.
Alitaka watendaji kuhakikisha muda wa kazi unatumiwa ipasavyo.

Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu, alisema lazima kuwe na ukomo wa bei licha ya kuwepo kwa mfumo wa soko huria. “Haiwezekani waagizaji wa chakula wako watano halafu hatuna usimamizi,” alisema.

Mbunge wa Mpanda Mjini (Chadema), Said Arfi, alisema katika mpango huo haoni mkakati wa kuwasaidia maskini.

Alisema pia katika mpango huo hakuna sehemu ambayo inamhakakishia mtu masikini matibabu.

“Bima ya Afya itolewe kwa raia wengine kama vile nchi nyingine zinazofanya kama vile kutoa sehemu ya kodi katika kuwawezesha watu wote kupata matibabu,” alisema Arfi.

Mbunge wa Manyovu (CCM), Albert Ntabaliba, alihoji ni mikakati gani iliyopo katika mpango huo inayozungumzia uzazi wa mpango.

“Mpango hauelezi kama idadi ya watu imetosha tusiongeze wengine wala haisemi kwamba haujatosha watu waongeze,” alisema na kuongeza kuwa mpango huo unapaswa kuja na majibu badala ya kulalamika.

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira, alitaja maeneo yaliyopewa kipaumbele katika mapendekezo ya mpango huo kuwa ni miundombinu na kilimo.

Maeneo mengine ni viwanda, teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama), majisafi na majitaka, maendeleo ya raslimali watu, utalii na huduma za kifedha.

Wasira alisema ili kufanikisha utekelezaji wa mpango wa maendeleo, itailazimu serikali itenge rasilimali za kutosha katika bajeti kila mwaka kwa ajili ta kugharimia miradi ya maendeleo.

“Katika mpango wa maendeleo wa miaka mitano ilikadiriwa kuwa Sh. trilioni 8.6 zitahitajika kila mwaka, kati ya hizo Sh. trilioni 2.7 zinatokana na fedha za ndani katika bajeti ya serikali,” alisema.

Alisema Sh. trilioni 5.9 zitatokana na uwekezaji wa sekta binafsi na washirika wa maendeleo.

Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, alisema mwaka jana serikali ilisema kipaumbele ni sekta ya nishati, lakini wizara yake ilitengewa katika bajeti Sh.  bilioni 400 wakati wizara nyingine zilipewa hadi zaidi ya Sh. trilioni moja.

Alisema kama haitatengwa bajeti ya kutosha kwa ajili ya miradi mbalimbali, wizara hiyo atakuwa akisulubiwa kwa kuwa haitafikia malengo yaliyokusudiwa.

Alisema pia miundombinu ya usafirishaji umeme imechoka, haina uwezo na kwa kuiboresha tutasaidia kupunguza upungufu wa nishati hiyo.

Aidha, Ngeleja alisema hali ya uchumi si ya kuridhisha na kwamba nchi haikopesheki.

Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, alisema Kituo cha Uwekezaji (TIC) ndicho kinachozalisha misamaha mingi ya kodi.

Alisema eneo jingine ambalo linazalisha misamaha ni misaada inayotoka nje ya nchi.
Mkulo alisema pia miradi yote inayotokana na wahisani haitozwi kodi.

Alisema serikali inazungumza na TIC ili warekebishe misamaha ya kodi ambayo alikiri kwamba ni mikubwa na inachukua karibu asilimia tatu ya bajeti nzima.

Alisema nchi za jirani misamaha ya kodi ni chini ya asilimia moja na hivyo mipango ni kuhakikisha misamaha ya kodi inafikia asilimia hiyo.

Aidha, alisema kuwa timu ya wataalamu inaangalia mikataba mipya ya madini.

Naye Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Juma Reli, alisema nchi hajafilisika na inakopesheka.
Alisema si kitu kigeni kwa serikali kukopa na kwamba serikali nyingi duniani zinakopa.

Akizungumzia kuhusiana na mfumuko wa bei, Reli alisema mchele ulisababisha mfuko wa bei.

Alisema mchele ulipanda kwa asilimia 65.6 kulinganisha na mahindi ambayo yalipanda kwa asilimia 16.

Alisema mchele wa Tanzania unapendwa sana na iwapo utazalishwa kwa wingi utazalisha fedha nyingi.

Alishauri kuwekeza katika kilimo cha mpunga ili kuongeza fedha za kigeni na chakula nchini.

Alisema pia wanaangalia upya hifadhi ya chakula nchini, ili kuwepo na akiba ya kutosha katika maghala kwa lengo la kukabiliana na mfumko wa bei ya mchele.
 
Alisema hawajafika hata asilimia 30 ya madeni waliyokopa na kwamba mwisho wa ukomo wa ukopaji ni asilimia 50. Hata hivyo, Reli alisema BoT imetahadharishwa kuepuka kudhamini mikopo.

Naye Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema baraza la mawaziri limesimamisha kwa muda wa mwaka mmoja kudhamini mikopo ili kuangalia upya udhamini.

Katibu wa Tume ya Mipango, Dk. Philip Mpango, alisema suala la mpango wa uzazi ni gumu kutokana na mila na utamaduni wa Mtanzania.

Alisema wameona hata kama watazifanya hazitaleta mabadiliko kwa kiasi kikubwa.

“Njia kubwa ni kusisitiza elimu hasa kwa wasichana. Watakuwa kwenye elimu ya sekondari kwa miaka minne kwa hiyo atakapotoka hatazaa watoto 10 tena,” alisema.

Alisema ni vema akasisitizwa kuwa kazi ya watu si kuuzaa pekee bali ni kuwatimizia mahitaji hao waliozaliwa.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment