Saturday May 25, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Dk. Mengi: Wajasiriamali tafuteni masoko

3rd July 2012
Print
Comments
Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi (kushoto), akizungumza jambo na mmoja wa akina mama wajasiriamali kwenye banda la Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF) wakati wa maonyesho ya 36 ya biashara ya kimataifa kwenye Uwanja wa Mwalimu Julius Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam jana.

Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, amewataka wajasiriamali nchini kutobweteka na badala yake wajenge utamaduni wa kutafuta masoko ya ndani kwa ajili ya bidhaa wanazozizalisha kuliko kusubiri masoko yawafuate.

Alisema hayo jana wakati akizungumza na wajasiriamali wa vikundi mbalimbali baada ya kutembelea banda la Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF) katika maonyesho ya 36 ya biashara ya Kimataifa yanayofanyika katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Dk. Mengi katika ziara hiyo alipata fursa ya kutoa ushauri na kusikiliza changamoto zinazowakabili wajasiriamali wa vikundi mbalimbali vya kutoka mikoa ya Singida, Tabora, Manyara, Mbeya, Rukwa, Dodoma, Zanzibar, Pwani, Tanga, Kagera, Lindi na Arusha ambavyo vinaonyesha bidhaa zao katika maonyesho hayo kwa ufadhili wa EOTF.

Alisema umefika wakati kwa wajasiriamali kuelekeza nguvu zao katika kutafuta masoko ya ndani ili waweze kuuza bidhaa wanazotengeneza na kuzizalisha badala ya kila wakati kulalamika kwamba hakuna masoko.

Dk. Mengi alisema tatizo lililopo ni kwamba watu wamejenga kasumba kuwa soko ni lazima liwe la nje tu na hivyo wamekuwa hawafanyi jitihada za kutafuta masoko ya ndani ambayo yanaweza kusaidia kwa kiwango kikubwa kuuza bidhaa zao.

“Soko haliwezi kupatikana kwa kuzalisha na kukaa, katafuteni masoko na siyo masoko yawafuate,”alisema Dk. Mengi wakati akizungumza na akina mama wa kikundi cha Millenium KT cha mkoani Kagera.
Aliongeza kuwa wajasiriamali pia waweke utaratibu wa kuwa na kitengo ambacho kazi yake itakuwa ni kujishughulisha na shughuli za uzalishaji na kingine cha kutafuta masoko.

Dk. Mengi akiwa katika kikundi cha Wakoro cha mkoani Lindi, alitaka wajasalimali kuzalisha bidhaa kulingana na mahitaji ya wateja badala ya kuwa na bidhaa ambazo haziwezi kununulika.

Mwenyekiti huyo pia aliwataka wajasiriamali kuachana na utamaduni wa kudhani kuwa kuuza bidhaa yeyote kwa bei ya chini wakati thamani yake inastahili kuwa kubwa haina maana kwamba kutawafanya wauze kwa wingi.

Alisema vipo vitu ambavyo vinahitajika sana na wananchi wenye kipato cha chini kama vile mahindi, unga, mchele na vitu vingine ambavyo hata vikiuzwa kwa bei ndogo siyo tatizo.

“Msidhani kuuza kwa mfano hii wine (mvinyo) kwa bei ndogo ya Sh.7,000 au Sh. 10,000 ndiyo mtauza kwa wingi hapana, mnachotakiwa ni kuongeza ubora wa bidhaa ili muuze kwa bei kubwa kulingana na thamani ya kitu chenyewe,” alisema Dk. Mengi.

Aliupongeza Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF) ambao Mwenyekiti wake ni Mama Anna Mkapa kwa jitihada za kusaidia wajasiriamali wanawake katika kukuza kipato chao.

Alisema EOTF umewakomboa akina mama wengi kutoka katika hali ya umaskini ambapo sasa baadhi yao wameboresha maisha yao kwa kumudu kusomesha watoto na kuhudumia familia zao kwa ujumla.



 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment